MATUKIO YA WIKI MKOANI KATAVI NA TANZANIA KWA UJUMLA DESEMBA 21-26,2015 NA P5 TANZANIA YA ISSACK GERALD BATHROMEO



 NA.ISSACK GERALD BATHROMEO


Posted By:Issack Gerald | At:Monday, December 21, 2015

Na.Issack Gerald- Katavi
Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la  KAZIMIRI MASUMBUKO(49) MKAZI NA MKULIMA WA MISANGA aliuawa kwa kuchomwa kitu chenye ncha kali sehemu za mgongoni, mkononi, mkono wa kushoto na kidevuni na watu wasiofahamika
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo,Kmanda wa Polisi Mkoani Katavi Dhahiri Kidavashari,amesema tukio hilo limetokea jana Jumapili tarehe 20.12.2015 majira ya saa katika kitongoji cha Misanga Kata na Tarafa ya Mwese Wilayani Mpanda Mkoani Katavi.
Kamanda Kidavashari amesema kuwa, siku ya tukio hilo,watuhumiwa wasiofahamika kwa sura wala idadi yao walifika nyumbani kwa marehemu wakakuvunja mlango na kuingia moja kwa moja hadi chumbani kwa marehemu na kumpeleka sebureni kwake kisha kutekeleza mauaji hayo na kutokomea kusikojulikana .
Mpaka sasa chanzo cha tukio hilo bado hakijafahamika. Hata hivyo Upelelezi wa shauri hili unaendelea kwa kufanya msako kwa kushirikiana na wakazi wa kata ya Misanga kuhakikisha watuhumiwa wanakamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayowakabili.
Wakati huo huo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi anatoa agizo kwa wananchi kuachana na vitendo vya kujichukulia sheria mikononi dhidi ya migogoro ya kijamii miongoni mwao, badala yake wajenge tabia ya kuheshimu na kutumia mamlaka za kisheria katika kutafuta ufumbuzi.
Amesisitiza kuwa ataendelea kuchukua hatua kali za kisheria kwa wale watakaoendelea kubainika kukiuka maagizo hayo kutokana na visingizio mbalimbali.

Posted By:Issack Gerald | At:Monday, December 21, 2015

Na.Issack Gerald- Katavi
Jeshi la Polisi Mkoani Katavi linawashikilia watu wawili akiwemo  ASHURA MSAGUSI(30) Karani wa chuo cha Maendeleo Msaginya Mkazi wa Kata ya Makanyagio na AISHA SUNGURA (28) Mkazi wa mtaa wa Mji wa Zamani kwa tuhuma za shambulio la mwili.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo,Kmanda wa Polisi Mkoani Katavi Dhahiri Kidavashari,alisema kuwa tukio hilo limetokea Mnamo tarehe 17.12.2015 majira ya saa 5 asubuhi katika Mji wa Zamani Kata na Tarafa ya  Kashaulili Wilayani Mpanda Mkoani Katavi.
Alimtaja aliyeshambuliwa kuwa ni JENEROZA ROBA(60 Mkazi wa Nsemulwa kwa Mkumbo ambapo alishambuliwa kwa kupingwa  ngumi sehemu mbalimbali za mwili wake na kusababishiwa maumivu makali.
Kamanda Kidavashari alisema kuwa,siku ya tukio inasemekana kuwa mtuhumiwa ASHURA MSAGUSI alijifanya kupandisha mashetani na kuanza kumtaja Mtendewa JENEROZA ROBA kuwa anajihusisha na shughuli za uchawi ambazo zinaathiri familia zao. Kitendo hicho cha kupandisha mashetani kilimshawishi AISHA SUNGURA na hivyo kuungana na ASHURA MSAGUSI na kuanza kumshambulia mtendewa.

Watuhumiwa wote wawili ambao wanaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi na wanatarajia kufikishwa mahakamani baada ya Upelelezi kukamilika.
Kufuati matukio ya kujichukulia sheria mkononi,Kamanda wa Polisi anatoa onyo wa watu wenye matukio hayo,ambapo amesema ataendelea kuchukua hatua kali za kisheria kwa wale watakaoendelea kubainika kukiuka maagizo hayo kutokana na visingizio mbalimbali.
Posted By:Issack Gerald | At:Monday, December 21, 2015

Na.Agness Mnubi-MPANDA.
WAZAZI na Walezi mkoani Katavi wametakiwa kutambua umhimu wa haki za watoto na kuepuka Mazingira yanayopelekea ukatili na unyanyasaji kwa watoto hao.

Akizungumza na P5 TANZANIA MEDIA na Mpanda Rdaio Mwenyekiti wa Asasi ya Faraja na  Urafiki kwa Wanandoa na Ushauri kwa Vijana (FUNUVI ) Bi. Neema Kidima amesema Maelewano mabaya katika ndoa na kutalikia ni miongozni mwa vyanzo vinavyopelekea   kutotambua haki za watoto na kusabaisha mazingira ya ukatili na unyanayasaji.
Bi. kidima  ameomba Wadau wanaojihusisha na kupinga ukatili ,Haki za binadamu, pamoja na serikali kushirikiana kutoa elimu katika jamii juu ya haki za watoto.
Desemba 18        Mwaka huu, watoto 62 wakiwemo wawili wenye ulemavu wa ngozi (albino) walifichuliwa Wilayani Mpanda na  kamati ya baraza la watoto, wakiwa katika mazingira yanayowanyima haki zao ikiwemo kupatiwa  elimu, kwa kipindi cha mwezi Juni hadi Desemba.
Posted By:Issack Gerald | At:Monday, December 21, 2015

NA:OFISI YA WAZIRI MKUU -DAR ES SALAAM
SERIKALI imekwishatenga kiasi cha sh. bilioni 137 kwa ajili ya kugharamia utoaji wa elimu ya bure kuanzia Januari hadi Juni, mwakani.
Kauli hiyo imetolewa jana jioni (Jumapili, Desemba 20, 2015) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akizungumza na mamia ya wananchi waliofika kumsikiliza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa uwanja wa mikutano wa Likangala wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
“Kazi ya utumbuaji majipu imezaa matunda kwani tumeweza kupata fedha za kugahrimia elimu ya bure ambayo iliahidiwa na Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli wakati wa kampeni. Fedha hiyo tunayo, na tumeshaanza kuisambaza kwa sababu tunataka shule zikifunguliwa Januari, 2016 watoto waanze kufaidika,” alisema huku akishangiliwa.
“Atakayezigusa fedha hizi na kuzitumia vibaya ni lazima tutamtumbua tu! Tumeshawapa maelekezo Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Maafisa Elimu wao na kuwaonya kuhusu matumizi ya fedha hizo,” alisema.
“Hatuhitaji mwanafunzi achangishwe hela ya mitihani, na zile shilingi 10,000/- kwa ajili ya wanafunzi wanaosoma Sekondari nazo pia tutazipeleka. Na huu ni mpango wa dharura ambao haukuwemo katika bajeti ya mwaka 2015/2016, kwa hiyo tutalazimika kuziombea kibali,” alisema.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema Serikali imekwishafanya hesabu za kubaini kiasi kinachohitajika kwa ajili ya milo ya watoto shuleni kwa wale walioko bweni na wale wa kutwa. Hesabu tunazo na tumebaini kuwa tutazimudu,” alisema huku akishangiliwa.
“Serikali ilitoa ahadi kwa wananchi na sisi tumedhamiria kuzitekeleza. Tuliahidi elimu bure nasi tutaitekeleza,” alisema.
Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Bw. Nape Nnauye amewataka madiwani wa jimbo la Ruangwa kuhakikisha wanamsaidia Waziri Mkuu Majaliwa kusimamia kazi za jimboni ili aweze kuwa huru kutekeleza majukumu ya kitaifa.
“Madiwani wa jimbo hili msaidieni Waziri Mkuu kusimamia shughuli za maendeleo ili wakati yeye anaendelea kutekeleza majukumu ya kitaifa, ya jimbo naye yawe shwari. Msaidieni kusimamia fedha za umma ziende kwenye miradi iliyokusudiwa ili wakati akitumbua majipu huko kwingine na huku pia yasiote,” aliongeza.

 WAZIRI MKUU ASEMA HANA KINYONGO NA MTU YEYOTE,ASEMA ITIKADI ZA SIASA ZILIISHIA OKTOBA 25

Posted By:Issack Gerald | At:Monday, December 21, 2015

Na.OFISI YA WAZIRI MKUU.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hana kinyongo na mtu yeyote kwa sababu alitangaza msamaha siku aliyokabidhiwa cheti kuwa mbunge wa jimbo la Ruangwa na kusisitiza kuwa siasa ziliisha tangu Oktoba 25, mwaka huu.
Ametoa kauli hiyo jana jioni wakati akizungumza na mamia ya wananchi waliofika kumsikiliza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa mikutano wa Likangala wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
“Sina kinyongo na mtu yeyote na roho yangu iko huru, hivi ndiyo nilivyo. Nilikwishatangaza msamaha kwa hiyo ninawaomba wale niliowakwaza nao pia wanisamehe… lakini ninawasihi kuwa milango iko wazi, wawe huru kurudi wakati wowote,” alisema huku akishangiliwa na wananchi hao.
“Ninawataka twende pamoja ili tulete maendeleo ya Ruangwa, huku nikisisitiza kaulimbinu yangu ya kampeni kwamba Ruangwa kwa Maendeleo Inawezekana. Wao warudi tu, nitawahudumia wote bila kujali itikadi zao.”
Aliwaeleza wakazi hao wa Ruangwa na vitongoji vyake kwamba amekuja kuwashukuru kwa kumchagua na kumpa kura nyingi la sivyo asingefanikiwa kuwa mbunge wao. “Kikubwa ninamshukuru Mungu aliyemuongoza Mheshimiwa Rais pamoja na Makamu wake hadi wakanipa jukumu hili,” alisema.
“Kipekee ninamshukuru Mungu aliyemuongoza Mheshimiwa Rais na kutupa sisi wana Ruangwa tusaidiane kulibeba jukumu hili. Ninawahakikishia kuwa pamoja na jukumu hili la kitaifa, sitawaacha wala sitawaangusha. Nitakwenda mikoa mingine hapa nchini ili kuwasikiliza na kuwahudumia Watanzania huku nikijua kwamba mpo salama,” alisema.
Aliwaeleza wananchi hao kwamba bila kujali itikadi za vyama, ameunda timu ya madiwani 22 kutoka kata zote za jimbo hilo ambayo atafanya nayo kazi kwa karibu ili kuhakikisha matarajio ya wana-Ruangwa yanatimia. Madiwani wanane kati hao 22 wanatoka UKAWA na 14 wanatoka Chama cha Mapinduzi (CCM).
Akigusia mipango ya maendeleo kwa jimbo hilo, Waziri Mkuu alisema ameamua kuweka umeme wa nishati ya jua kwenye shule zote na zahanati zote ambazo hazitafikiwa na umeme wa gridi ya Taifa kwa sababu ziko pembezoni mwa jimbo hilo.
“Nafanya hivi kwa sababu sipendi watoto wetu wakose masomo ya jioni kwa sababu ya kukosa umeme au washindwe kufanya mafunzo kwa vitendo (practicals) kwa vile wamekosa umeme,” alisema.
Mapema, akiwa njiani kuelekea Ruangwa, Waziri Mkuu alisimama kwa muda kijijini kwao Nandagala katika kata ya Mnacho, na kuwasalimia wananchi waliojitokeza kumpokea kwa nderemo na hoihoi kibao.
Katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa kijijini hapo, Waziri Mkuu alikabidhiwa zawadi mbalimbali yakiwemo mavazi ya kimila pamoja na silaha za jadi.
Aliwataka wakazi hao wamvumilie kwa sababu ratiba sasa itabadilika na hawatamuona mara kwa mara kama ilivyokuwa awali kwa vile anapaswa awahudumie Watanzania wote. “Zile safari za jimboni zitapungua sana lakini mjue ni kwa sababu niko kwa ajili ya Watanzania wote wa nchi hii,” alisema.
“Ninaomba dua zenu ili niendelee kuwa mwadilifu na muwajibikaji,” aliwaomba na kususutiza kwamba waendelee kumuombea yeye pamoja na viongozi wengine wa kitaifa ili waweze kutimiza yale ambayo Watanzania wanatamani yatokee.
Posted By:Issack Gerald | At:Tuesday, December 22, 2015

Na.Meshack Ngumba-MPANDA
SERIKALI imeombwa Kuharakisha Mchakato wa Kuibadilisha hospitali ya Wilaya Kuwa hospitali ya halmashauri ya Manispaa ya Mpanda ili Kusogeza huduma za afya kwa wakazi wa Manispaa hiyo.
Ombi hilo limetolewa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mpanda ambaye pia ni diwani wa Kata ya Majengo Mh,William Philip Mbogo Katika Mahojiano maalum na Mpanda Radio na P5 TANZANIA MEDIA
Katika hatua nyingine Mh Mbogo ameahidi Kushirikiana na Madiwani wa Kata zote za Manispaa ya Mpanda Kutatua Kero za wananchi ikiwemo Kusimamia Miradi ya Maendeleo inayoanzishwa Kwa Maslahi ya wananchi.
Mh,Mbogo anakuwa Meya wa Kwanza wa Manispaa ya Mpanda Kihistoria tangu halmashauri ya Mpanda ilipopandishwa daraja Kutoka halmashauri ya Mji mwezi July mwaka huu.

 MKURUGENZI HALMSHAURI YA WILAYA YA KALAMBO,ASIKITISHWA NA HALI YA ELIMU MKOANI RUKWA

Posted By:Issack Gerald | At:Tuesday, December 22, 2015

Na.Issack Gerald-SUMBAWANGA
MKURUGENZI  Mtendaji wa  Halmashauri ya wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa Bw. Bensoni Kilagi,amesema hajaridhishwa na matokeo ya darasa la nne na darasa la saba kwa mwaka 2015 mkoani humo.
Akizungumza na P5 TANZANIA MEDIA Kwa njia ya simu,Bw. Kilagi  amesema matokeoa yameendelea kuwa mabaya ambapo kwa mwaka  2014 ufaulu ulikuwa asilimia thelathini huku mwaka 2015 ufaulu huo ukipanda kwa salimia 10 na kufikia asilimia 40.
Aidha amesema ili kunusuru hali ya elimu Mkoani humo,wamekusudia kuitisha vikao vya mara kwa mara vinavyohusisha wadau wa elimu wakiwemo wazazi,walezi,watendaji na wataalamu wengine wa masuala ya elimu ili kuongeza kiwango cha ufaulu.
Hata hivyo Bw.Kilangi amezitaja baadhi ya changamoto zinazopelekea kufanya vibaya katika suala zimala elimu  ni kutofanya mazoezi ya mitihani mara kwa mara ,madawati pamoja na nyumba za walimu.

Posted By:Issack Gerald | At:Wednesday, December 23, 2015

Na.OFISI YA MAWASILIANO YA IKULU.
Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dk.John Magufuli amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), Benhadard Tito.
Rais Magufuli amesema,amemsimamisha Bw. Tito kupisha uchunguzi wa kina kutokana na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za manunuzi, yaliobainika katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya ujenzi wa Reli ya Kati.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, Dk Magufuli,amefikia uamuzi huo baada ya kuitisha kikao cha wataalamu kutoka wizara na taasisi mbalimbali za serikali, ambazo zinahusika katika utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kisasa.
Aidha Rais Magufuli ameivunja Bodi ya Rahco baada ya kujiridhisha kuwa haikutekeleza ipasavyo wajibu wake katika kusimamia mchakato wa zabuni hiyo na badala yake imeonekana kutetea kilichofanyika.
Posted By:Issack Gerald | At:Wednesday, December 23, 2015

Na.Ofisi ya Waziri-DAR ES SALAAM.
Kaimu mkurugenzi wa taasisi ya saratani ya Ocean Road Dk.Diwani Msemo amesimamishwa kazi.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu amesema,Dk.Msemo amesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi pamoja na mambo mengine ikiwa ni pamoja na kubaini kama kuna mgongano wa kimaslahi ambao umeathiri utendaji chini ya Kaimu Mkurugenzi.
Wakati huo huo Mh.Ummy,ameiagiza bodi ya taasisi ya saratani ya Ocean Road kuteua mkurugenzi atakayekaimu nafasi ya Mkurugenzi mtendaji.
Katika hatua nyingine,watendaji wote wa serikali katika sekta ya afya wakiwemo wafamasia,wauguzi na waganga wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma,wameagizwa kukiri kwa maandishi ikiwa wanamiliki zahanati,vituo vy afya,kliniki na maduka ya dawa ndani ya siku 21 kuanzia leo Desemba 23.
Amesema kuwa agizo hili,halimwondolei wajibu kiongozi yeyote wa serikali ambaye anapaswa kujaza tamko la viongozi wa Umma kuhusu rasilimali na madeni kwa mjibu wa kifungu namba 9 na 11 cha sheria ya maadili ya viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995 na namba 5 ya mwaka 2001
Posted By:Issack Gerald | At:Wednesday, December 23, 2015

Na. OFISI YA WAZIRI MKUU,
 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa wanaongeza udhibiti na usimamizi wa migogoro ya  ardhi kwenye maeneo yao husika.
Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumatano, Desemba 23, 2015) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Lindi kwenye Ikulu ndogo mara baada ya kuwasili akitokea jimboni kwake Ruangwa.
 “Ardhi ni mali ya Serikali lakini maeneo yanayotwaliwa kwa sababu mbalimbali za maendeleo yasiwe chanzo cha migogoro na wananchi tunaowaongoza,” alisema.
 Akitoa mfano, Waziri Mkuu alisema anatambua kuna mgogoro wa eneo la mgodi katika wilaya ya Ruangwa baina ya wananchi na wawekezaji wa kampuni ya Uranex. Na hii ni kwa sababu wao ndiyo waliamua kufanya tathmini (evaluation) ya eneo hilo. Yale ni makosa kwa sababu aliyepaswa kufanya tathmini ni Halmashauri na siyo mwekezaji,” alisema.
 Alisema wawekezaji wanaruhusiwa kisheria kufanya tathmini lakini sheria waliyoitumia ni sheria namba 8 peke yake. “Kama Halmashauri ingefanya kazi hiyo ni lazima wangetumia sheria ya ardhi ya vijiji pamoja na sheria ya madini na wananchi wangepata thamani halisi ya ardhi yao,” alisema.
 “Ninaagiza Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa ikahakiki lile eneo na kubaini kama ni la kilimo au la madini na kama ni la kilimo, wananchi wamelima mazao gani na kwa muda gani kisha wafanye tathmini upya. Yuko valuer wa Halmashauri mwenye dhamana hiyo na siyo wao,” alisema.
 “Nasisitiza tena ni vema Wakurugenzi wote, Wakuu wa Wilaya chini ya uongozi wa Wakuu wa Mikoa mjiridhishe kuwa hakuna migogoro kwenye maeneo yenu. Kama ipo, imalizeni kwa kukaa mezani na kuzungumza na pande husika, inawezekana kabisa,” alisisitiza.
Posted By:Issack Gerald | At:Thursday, December 24, 2015

Na.Issack Gerald-MPANDA
Miundombinu mibovu ya barabara hususani kipindi hiki cha masika imeathiri uchumi wa waendesha pikipiki katika Manispaa ya Mpanda Mkoani Matavi.

Hayo yamebainishwa na waendesha pikipiki hao wakati wakizungumza na P5 TANZANIA MEDIA na mpanda redio ambapo wamesema kuwa barabara nyingi hasa vijijini hazipitiki kutokana na mabonde hali inayowafanya kufanya shughuli hiyo  mjini pekee.
Katika hatua nyingine madereva hao wamesema,katika kuzua ajali za barabarani hasa kipindi hiki cha msimu wa sikukuu wamejipanga kuendesha pikipiki kwa umakini mkubwa kutokana ongezeko la vyombo vingi vya moto barabarani.
Takwimu zinaonyesha kuwa katika kipindi cha sikukuu matukio ya ajali huongezeka kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo madereva kuendesha kwa mwendokasi pamoja na ulevi.
Posted By:Issack Gerald | At:Thursday, December 24, 2015

Na.Issack Gerald-Mpanda
Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina Mateo Robert(33) mchimbaji mdogo mkazi wa Mbeya-Songwe,amefariki dunia baada ya kuangukiwa na lundo la udongo akiwa kwenye shimo (LONG BASE) wakati akichimba madini ya dhahabu.

 Kamanda wa polisi Mkoani Katavi Dhahiri Kidavashari amesema kuwa tukio hilo limetokea Mnamo tarehe 23.12.2015 majira ya saa 09:00 kwenye Machimbo ya dhahabu ya wachimbaji wadogo ya Nsimbo yaliyopo kijiji cha Katuma, Kata ya Katuma, Tarafa ya Mwese Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi.
Kamanda amesema kuwa marehemu akiwa na wenzake wawili ambao ni Edson David Akiba(25 mchimbaji Mkazi wa Kigoma pamoja na Tungu Thomas(30) mchimbaji Mkazi wa mkoa wa Shinyanga walielekea mgodini hapo kufanya shughuli zao za uchimbaji kama ilivyo kawaida yao ambapo wakati wa uchimbaji huo marehemu na mwenzake aitwaye Tungu Thomas walikuwa wameingia shimoni na nje shimo walimuacha mwenzao ambaye ni Edson David Akiba ambapo baada ya muda mfupi kilisikika kishindo kutoka ndani ya shimo.
Kutokana na hali hiyo  Edson David alijaribu kuwaita wenzake waliokuwa shimoni hawakuitika ndipo harakati za kuwasaidia zilipofanyika kwa kuwaita wachimbaji wengine wa maeneo jirani ambapo baada ya kuingia marehemu alikutwa kafunikwa na udongo akiwa tayari kafariki dunia huku mwenzake Tungu Thomas akiwa amejeruhiwa kichwani.
Aidha Kamanda Kidavashari amesema,kwa mujibu wa uchunguzi wa kitabibu kifo cha marehemu kilitokana na majeraha aliyoyapata kichwani (HEAD INJURY) na mwili wake ulikabidhiwa kwa ndugu zake kuendelea na taratibu zingine za mazishi, huku Tungu Thomas  akipatiwa matibabu katika hospitali ya Katuma na kuruhusiwa kwenda kujiuguzia nyumbani.
Hata hivyo si mara ya kwanza matukio kama haya kutokea ikizingatiwa kuwa hivi karibuni wachimbaji wadogo walifukiwa katika mgodi wa Nyangalata uliopo Wilayani Kahama.
Posted By:Issack Gerald | At:Thursday, December 24, 2015

Na.Issack Gerald-Mpanda
Jeshi la polisi Mkoani Katavi linamtafuta mtu mmoja aliyekimbia akikwepa kukamatwa na polisi kutokana na kumiliki silaha aina ya gobore  kinyume na sheria.

Kamanda wa Polisi Mkoani Katavi Dhahiri Kidavashari amethibitisha mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Malugumba Nzinza kukamatwa na silaha aina ya gobore ambayo imepatikana ikiwa imefichwa katika nyumba yake.
Kamanda kidavashari amesema mtu huyo alikamatwa,mnamo tarehe 12.12.2015 majira ya saa 12:00  katika kijiji cha Mpembe Kata na Tarafa ya  Mwese Wilayani Mpanda Mkoa wa Katavi.
Kamanda amesema kuwa katika tukio hilo,Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na askari wa wanyama pori (TANAPA) walipata taarifa toka kwa raia wema kuwepo kwa mtu anayehisiwa kumiliki silaha kinyume na utaratibu.
Mpaka sasa mtuhumiwa bado hajakamatwa na misako mbalimbali inaendelea katika kuhakikisha mtuhumiwa anatiwa nguvuni na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayomkabili.
Posted By:Issack Gerald | At:Thursday, December 24, 2015

NA.Mwandisi wetu-MWANZA

Askari mmoja  wa jeshi la Polisi mkoani Mwanza  jana amefyatua risasi na kumuua asikari mwenzake kisha nayeye kujipiga risasi na kufariki dunia katika lindo la benki ya posita jijini mwanza huku chanzo cha tukio hilo kikiwa hakija julikana.

 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza  kamishina msaidizi wa Polisi Justus Kamugisha amethibitisha kutokea kwa tukio na kwamba limetokea majira ya saa nane na nusu mchana katika lindo la Banki ya Posta tawi la Pamba  jijini Mwanza.
 Kamanda Kamugisha amewataja askari hao kuwa ni Konstebo H 852 Daud Masunga Elisha aliyempiga risasi Pc Petro Simoni Matiko H5950 eneo la begani na baadae Pc Masunga kujipiga risasi eneo la paji la uso na kufariki pao hapo, wote ni askari wa wilaya ya Nyamagana
Aidha Kamanda Kamgisha amesema jeshi la Polisi lina endelea na uchunguzi juu ya tukio hilo  ili kubaini chanzo cha mauaji hayo.
Posted By:Issack Gerald | At:Friday, December 25, 2015

Na.Issack Gerald-Mpanda
Jeshi la polisi Mkoani Katavi linawashikilia watu watatu kutokana na kukamatwa na nyara za serikali ambazo wamezipata kinyume na sheria.

Kamanda wa Polisi Mkoani Katavi Dhahiri Kidavashari amewataja wanaoshikiliwa na polisi kuwa ni Leonard Mbegele(38) mkazi wa Migazini na Anastazia Bernad(38) mkazi wa kichangani ambao walikamatwa mnamo tarehe 22.12.2015 majira ya saa 13:00 maeneo ya Mikocheni Tarafa ya Kashaulili Wilayani Mkoani Katavi wakiwa na nyama ya Kongoni kilo moja.
Kamanda amesema kuwa Jeshi la Polisi baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema lilifanya upekuzi nyumbani kwa Anastazia Bernard ambapo nyama hiyo ilikutwa ikiwa imewekwa kwenye Hotpot iliyokuwa ndani ya kabati.
Katika upelelezi wa awali wa tukio hiliAanastazia alidai kuwa nyama hiyo ni ya Malack Jonas ambapo hata hivyo Jonas naye aliikana nyama hiyo.
Mpaka sasa watuhumiwa wote wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi na watafikishwa mahakamani baada ya Upelelezi kukamilika.
Wakati huo huo Leornard Mbegele (38) Mkazi wa migazini Kata ya Nsemulwa, Tarafa ya Kashaulili, Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi Mnamo tarehe 22.12.2015 majira ya saa 14:00  anashikiliwa na alikamatwa akiwa na nyama ya Kongoni kilo 15.
Mtuhumiwa anatarajiwa kufikishewa mahakamani upelelezi utakapokamilika.

 DAR ES SALAAM
KUKAMILIKA KWA IDADI YA MAWAZIRI WANAOUNDA BALAZA LA MAWAZIRI.
RAIS John Magufuli amemalizia kujaza nafasi za uteuzi wa Mawaziri na Naibu Waziri alizobakiza wakati akitangaza Baraza la Mawaziri la Kwanza katika awamu ya tano ya utawala wake.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu, Gerson Msigwa kwa vyombo vya habari, Dar es Salaam jana, katika uteuzi wake Rais Magufuli amemteua Profesa Jumanne Maghembe kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.
Aidha, Dk Philip Mpango aliyekuwa Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ameteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango. Amemteua kuwa Mbunge na kumteua pia kuwa Waziri.
Rais Magufuli pia amemtangaza Profesa Makame Mbarawa kuwa Waziri mpya wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, akimhamisha kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Naibu Waziri wa zamani wa Ujenzi, Gerson Lwenge ameteuliwa kuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji.
Aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi ni Dk Joyce Ndalichako ambaye mapema jana aliteuliwa kuwa Mbunge. Dk Ndalichako aliwahi kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza na Mitihani la Taifa (NECTA).
Katika uteuzi wake mwingine, Rais Magufuli amemteua Hamad Masauni kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. Waziri wake ni Charles Kitwanga. Rais Magufuli, Desemba 9 mwaka huu alitangaza kuunda wizara 18 zenye mawaziri 19. Mawaziri hao na wizara zao kwenye mabano ni George Simbachawene na Angela Kairuki (Ofisi ya Rais-Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora) wakati Naibu wa wizara hiyo na Selemani Jaffo.
Wengine ni Mwigulu Nchemba (Kilimo, Mifugo na Uvuvi) na Naibu wake ni William ole Nasha, Jenista Mhagama (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Balozi Augustine Mahiga (Mambo ya Nje na Afrika Mashariki). Naibu wake ni Dk Suzan Kolimba.
William Lukuvi (Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi) ambaye Naibu wake ni Angelina Mabula, Ummy Mwalimu (Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto) na Naibu wake ni Dk Hamisi Kigwangalla.
Waziri wa Nishati na Madini ni Profesa Sospeter Muhongo ambaye Naibu wake ameteuliwa Dk Medard Kalemani. Waziri wa Katiba na Sheria ni Dk Harison Mwakyembe na Waziri wa Ulinzi ni Dk Hussein Mwinyi.
Aidha, Nape Nnauye aliteuliwa kuwa Waziri wa Habari na Michezo na Naibu wake ni Anastazia Wambura. January Makamba aliteuliwa Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na Naibu wake ni Luhaga Mpina.
Katika uteuzi wa awali, Rais Magufuli alimteua Charles Mwijage kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Wengine walioteuliwa kuwa Naibu Mawaziri, wakati wizara zao zikisubiri mawaziri kamili ni Edwin Ngonyani (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano), Ashantu Kijaji (Wizara ya Fedha), Ramo Makani (Maliasili na Utalii) na Stella Manyanya (Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi).
Naibu Waziri mwingine ni Isack Kamwela wa Maji na Umwagiliaji. Wakati huo huo, Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Alphayo Kidata ameteuliwa kuwa Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA.
“Mbali ya kukamilisha uteuzi wa Baraza lake la Mawaziri, Rais Magufuli pia amewatakia heri Watanzania wote katika Sikukuu za Maulid, Krismasi na Mwaka Mpya na kuwataka washerehekee kwa amani na utulivu,” ilieleza taarifa hiyo ya Ikulu.

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA FUPI YA ABDULRAHMAN KINANA ALIYEJUZULU UKATIBU MKUU CCM

FAHAMU HISTORIA YA JOKETI ALIYETUMBULIWA NA UVCCM

HISTORIA FUPI YA LAZARO NYALANDU ALIYEIBWAGA CCM NA KUHAMIA CHADEMA