ASKARI MAGEREZA 11 WASIMAMISHWA KAZI



Jeshi la Magereza Tanzania limewasimamisha kazi askari wake 11 waliofikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji ya Aloyce Makalla (41) mkazi wa Kijiji cha Kerenge wiki iliyopita.

Taarifa kutoka ndani ya jeshi hilo zinaeleza kuwa askari hao walisimamishwa kazi na Kamishna Jenerali wa Magereza,Dk Juma Malewa juzi.
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga,John Masunga alithibitisha kusimamishwa kwa askari hao lakini hakutaka kuzungumzia suala hilo kwa undani zaidi akisisitiza kuwa msemaji wa jeshi hilo ni Kamishna Jenerali pekee.
Askari waliosimamishwa ambao walishafikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Korogwe mwishoni mwa wiki mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Kassim Mkwawa ni Jonas Makere,Shadrack Lugendo,Lazaro Stephen,Mussa Zuberi,Ramadhan Yusuf,Robert Alfred,Fhidirish Osmas,Alfonce Revocatus,Mbesha Naftari,Hamis Msola na Michael Elias.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa hatua ya kuwasimamisha kazi askari hao imechukuliwa ikiwa ni kupisha vyombo vya sheria kufanya kazi yake kwa uhuru zaidi na kwamba hatima yao itategemea uamuzi wa mahakama hiyo.
Askari hao wa Wilaya ya Korogwe walifikishwa katika mahakama hiyo wakikabiliwa na shtaka la kumuua mwanakijiji huyo.
Ilidaiwa mahakamani hapo na mwanasheria mwandamizi wa Serikali,Saraji Iboru kuwa Januari 22 mwak ahuu saa 9.30 katika kitongoji cha Mapangoni Kijiji cha Kerenge, washtakiwa hao kwa pamoja walimuua mwanakijiji huyo.
Iboru ambaye alikuwa akisaidiana na mwendesha mashtaka kiongozi,Shosa Naiman alidai kwamba siku ya tukio,washtakiwa hao walikwenda nyumbani kwa Makalla wakimtuhumu kwamba Januari 15 alimjeruhi askari mwenzao aitwaye Sajenti Stephen.
Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na uwezo kisheria wa kusikiliza kesi za mauaji ambapo Hakimu Mkwawa aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 15 itakapotajwa tena.

Habari zaidi ni P5TANZANIA LIMITED


Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA FUPI YA ABDULRAHMAN KINANA ALIYEJUZULU UKATIBU MKUU CCM

FAHAMU HISTORIA YA JOKETI ALIYETUMBULIWA NA UVCCM

HISTORIA FUPI YA LAZARO NYALANDU ALIYEIBWAGA CCM NA KUHAMIA CHADEMA