WAZIRI MKUU AELEZA MIKAKATI YA SERIKALI KUFUNGUA VIWANDA VYA NGOZI DAR, GEITA NA SHINYANGA


Issack Gerald-DAR ES SALAAM
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema,Serikali imepanga kufungua viwanda vya kusindika ngozi kwenye mikoa ya Shinyanga, Geita na Dar es Salaam ili kutoa soko kwa ngozi za wanyama wanaochinjwa kwenye machinjio ya mikoa hiyo.
                                            
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Watanzania waishio Botswana baada ya kuhudhuria mkutano wa SADC mjini Gaborone Januari 18, 2016. Waziri

Majaliwa ametoa kauli hiyo jana jioni wakati akizungumza na baadhi ya Watanzania waishio Botswana kwenye kikao kilichofanyika kwenye kituo cha mikutano ya kimataifa (GICC), jijini Gaborone, Botswana.
Waziri Mkuu amekuwa nchini Botswana kwa ziara ya siku moja kumwakilisha Rais Dk. John Pombe Magufuli kwenye mkutano wa SADC Double Troika yaani kikao maalum cha Wakuu wa Nchi na Serikali na Wakuu wa Nchi wanaounda Chombo cha Ushirikiano wa Siasa,Ulinzi na Usalama.
Amesema Serikali imeamua kuongeza viwanda nchini, kama njia mojawapo ya kukuza uchumi,kuacha kuuza mali ghafi lakini pia ni fursa ya kuongeza ajira kwa Watanzania.
Wakati huo huo akijibu hoja zilizoainishwa kwenye risala yao, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali bado ina nia ya kuhamia Dodoma na kwamba itaendelea kutenga fedha zaidi ili wizara nyingi zijenge ofisi zao Dodoma.
Aidha Waziri Mkuu Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwataka Watanzania waishio ughaibuni kutafuta fedha za mitaji ambapo fedha hizo zinaweza kuwa zao au kupitia kwa marafiki zao ili waweze kuwekeza nyumbani Tanzania.
Awali akisoma risala yao kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa Chama cha Watanzania waishio nchini Botswana Bw. Neiman Kissasi amesema chama hicho kilianzishwa mwaka 1992 kikiwa na lengo la kuwaunganisha Watanzania waishio Botswana pamoja kujenga undugu wao na kusaidiana.
Katika risala yao, wameshauri wafugaji wa Tanzania waelimishwe na kuwezeshwa kufuga kisasa na kuondokana na ufugaji wa kurandaranda.
Vilevile, wameiomba Serikali ifungue fursa za kiuchumi kwenye mikoa mingine ya Tanga, Lindi, Mtwara, Pwani, Kigoma, Mbeya, Mwanza na Arusha badala ya kuziacha ziwe Dar es Salaam peke yake.
Waziri Mkuu amerejea jijini Dar es Salaam jana usiku.
 Chanzo cha habari : Ofisi ya Waziri Mkuu

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA FUPI YA ABDULRAHMAN KINANA ALIYEJUZULU UKATIBU MKUU CCM

FAHAMU HISTORIA YA JOKETI ALIYETUMBULIWA NA UVCCM

HISTORIA FUPI YA LAZARO NYALANDU ALIYEIBWAGA CCM NA KUHAMIA CHADEMA