TAMISEMI YAAGIZWA KUSIMAMIA VIZURI HALMASHAURI


Na.Issack Gerald-Katavi
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ndiyo kitovu cha nchi na kwamba kila Mtanzania ameelekeza jicho lake pale kwa sababu anasubiri kupata huduma ya msingi.

Ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na wakurugenzi, wakuu wa taasisi na watumishi wa Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwenye mkutano uliofanyika ofisi ya TAMISEMI mjini Dodoma.
Waziri Mkuu ameitaka ofisi hiyo ihakikishe inaisimamia vizuri mikoa na halmashauri ili Serikali iweze kupata matokeo mazuri na tarajiwa.
Waziri Mkuu alisema jukumu kubwa lililopo hivi sasa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ni kuhakikisha kuwa zinabuni vyanzo vipya vya mapato na kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imekusudia kuwahudumia ipasavyo Watanzania wenye uelewa tofauti na matakwa tofauti na kwa kuanzia Serikali imeanza kuwajenga watumishi wa Serikali kutambua kuwa wao ni wahudumu wa wananchi hivyo inawapasa kuwahudumia vema.
Awali akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na watumishi hao, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Bw. George Simbachawene alisema TAMISEMI wapo tayari kubadilika na kufanya kazi kama kauli ya Rais John Pombe Magufuli inavyotaka, yaani HAPA KAZI TU.
Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Bernard Makali alimpongeza Waziri Mkuu Majaliwa kwa kusimamia vizuri masuala ya elimu nchini wakati akiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya elimu.
 Chanzo cha Habari : Ofisi ya Waziri Mkuu

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA FUPI YA ABDULRAHMAN KINANA ALIYEJUZULU UKATIBU MKUU CCM

FAHAMU HISTORIA YA JOKETI ALIYETUMBULIWA NA UVCCM

HISTORIA FUPI YA LAZARO NYALANDU ALIYEIBWAGA CCM NA KUHAMIA CHADEMA