WAZIRI MKUU MAJALIWA AZINDUA MBIO ZA MWENGE WA UHURU MWAKA 2018 ATAJA MIKOA INAYOONGOZA KWA UTORO SHULENI


WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Kassim Majaliwa amezindua mbio za mwenge wa uhuru kwa mwaka 2018.
Akizindua mbio hizo kitaifa Mkoani Geita,amewataka viongozi wa mikoa ya Tabora,Geita,Mtwara na Shinyanga ambayo inaongoza kwa utoro wa wanafunzi kwa shule za sekondari wahamasishe umuhimu wa elimu na mahudhurio endelevu shuleni.
Akizungumzia kuhusu utoro kwa shule za sekondari nchini,Waziri Mkuu amesema mkoa wa Tabora unaongoza kwa utoro kwa kuwa na silimia 9.7,Geita asilimia 8.1,Mtwara asilimia 6.4 na Shinyanga asilimia 6.3.
Kuhusu utoro wa wanafunzi wa shule za Msingi nchini, Waziri Mkuu amesema mkoa unaoongoza ni wa Rukwa kwa asilimia 3.2,Geita asilimia 3.1,Tabora asilimia 2.9, Simiyu asilimia 2.0 na Singida asilimia1.9.
Aidha Waziri Mkuu amesema dhamira ya Serikali ni kuwashirikisha wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo kuwekeza katika elimu na kuzalisha rasilimali watu yenye ujuzi na stadi zitakazowezesha kuchochea mapinduzi ya viwanda ili nchi iwe ya uchumi wa kati ifikapo 2025.
Awali,Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera,Bunge, Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu Bi.Jenista Mhagama alisema Mwenge wa Uhuru utakimbizwa umbali wa takribani kilomita 103,440.7 kwa siku 195 katika mikoa yote 31 nchini na halmashauri za wilaya 195.
Aidha Bi.Mhagama Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 zinaongozwa na Bw.Charles Kabeho kutoka mkoa wa Dar es Salaam akishirikiana na Bw.Issa Abasi Mohamed (Kusini Pemba),Bi. Agusta Safari (Geita),Bw.Ipyana Mlilo (Tanga),Bw.Dominick Njunwa (Kigoma) na Bi. Riziki Hassan Ali (Kusini Unguja).
Kwa upande wake Waziri wa Vijana,Utamaduni,Sanaa na Michezo - Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Balozi Ali Abeid Karume alisema atahakikisha ujumbe wa Mwenge wa Uhuru unawafikia wananchi wote pamoja na kupita katika miradi yote ya maendeleo iliyopangwa.
Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2018 zimezinduliwa katika uwanja wa Magogo mkoani Geita ambapo Kaulimbiu ya mbio za mwenge kwa mwaka huu ni ‘Elimu ni ufunguo wa maisha,wekeza sasa kwa maendeleo ya Taifa letu.’
Kwa mwaka uliopita mbio za mwenge wa uhuru ambao ulianzishwa Desemba 9,1961 zilikuwa zimezinduliwa Mkoani Katavi Aprili 2,2017 na Kuzimwa Okt 14,2017 visiwani Zanzibar.
Habari zaidi ni www.p5tanzania.blogspot.com

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA FUPI YA ABDULRAHMAN KINANA ALIYEJUZULU UKATIBU MKUU CCM

FAHAMU HISTORIA YA JOKETI ALIYETUMBULIWA NA UVCCM

HISTORIA FUPI YA LAZARO NYALANDU ALIYEIBWAGA CCM NA KUHAMIA CHADEMA