RAIS MAGUFULI AZINDUA UKUTA KUZUNGUKA MADINI YA TANZANIATE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli amezindua ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite wilayani Simanjiro mkoani Manyara uliojengwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa lengo la kudhibiti utoroshaji wa madini na ukwepaji wa kodi.
Ukuta huo wenye urefu wa kilometa 24.5 umejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 5 na Milioni 646 ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa tarehe 20 Septemba,2017 na Mhe.Rais Magufuli alipokuwa akizindua barabara ya KIA – Mirerani.
Mhe.Rais Magufuli ameipongeza JWTZ kwa kukamilisha kazi hiyo kwa haraka na kwa gharama nafuu na amewapongeza maafisa,askari na vijana 2,356 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) walioshiriki katika ujenzi kwa uzalendo wao na kujituma ili kulinda rasilimali hiyo muhimu kwa Taifa.
Mhe.Rais Magufuli amelikubali ombi la Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Venance Salvatory Mabeyo na ameagiza vijana wa JKT walioshiriki katika ujenzi wa ukuta huo waajiriwe katika vyombo vya ulinzi na usalama vikiwemo Polisi na JWTZ ilimradi wawe na sifa zinazostahili.
Aidha,Mhe.Rais Magufuli amewahakikishia wananchi wa Mirerani kuwa watanufaika zaidi na hatua ambazo zinachukuliwa kudhibiti utoroshaji na ukwepaji wa kodi za madini ya Tanzanite na amekabidhi gari jipya la wagonjwa aina ya Toyota Land Cruiser “Hard Top” alilowaahidi wakati akiagiza kujengwa kwa ukuta huo.
Wakati huo huo Mhe.Rais Magufuli amemshukuru Mzee Jumanne Ngoma aliyevumbua madini ya Tanzanite mwaka 1967 na kutambuliwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl.Julius Kambarage Nyerere mwaka 1980, na amempa Shilingi Milioni 100 kwa kutambua mchango mkubwa alioutoa kwa Taifa kuvumbua madini hayo,yanayopatikana Tanzania pekee kote duniani.
Amesema utafiti uliofanywa katika kitalu C umebaini kuwa kuna mashapo ya Tanzanite yatakayochimbwa hadi mwaka 2042 na kwamba lipo eneo jingine lenye Tanzanite nyingi zaidi na ambalo Serikali italizungushia ukuta ili kulinda na kudhibiti utoroshaji madini na ukwepaji wa kodi.
Mhe.Rais Magufuli amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi za Serikali kuinua uchumi,kutekeleza miradi ya maendeleo na kudhibiti rasilimali za nchi na amewasihi kujiepusha na watu wanaoshabikia mabaya kwa nchi wakiwemo wanaowaunga mkono wanyonyaji na uvunjifu wa amani.
Kwa upande wake Mzee Jumanne Ngoma amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutambua mchango wake wa kuvumbua madini ya Tanzanite na amesema anaamini sasa madini hayo yatapata thamani inayostahili.
Nae Waziri wa Madini Mhe.Angellah Kairuki amemshukuru Mhe.Rais Magufuli kwa maelekezo yake ya kujengwa kwa ukuta na kulisimamia vizuri soko la Tanzanite ambapo malipo ya mrabaha kutoka kwa wachimbaji ukiondoa Tanzanite One na STAMICO kwa miezi mitatu tu ya kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu yamefikia Shilingi Milioni 714 na hivyo kuzidi malipo ya mwaka mzima wa 2015 (Shilingi Milioni 166.8),2016 (Shilingi Milioni 71.8) na 2017 (Shilingi Milioni 147.1).
Katika sherehe hizo Mhe.Rais Magufuli amekabidhi tuzo na vyeti kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen.Mabeyo,maafisa na askari wa JWTZ na vijana wa JKT walioshiriki ujenzi huo.
Habari zaidio ni www.p5tanzania.blogspot.com

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA FUPI YA ABDULRAHMAN KINANA ALIYEJUZULU UKATIBU MKUU CCM

FAHAMU HISTORIA YA JOKETI ALIYETUMBULIWA NA UVCCM

HISTORIA FUPI YA LAZARO NYALANDU ALIYEIBWAGA CCM NA KUHAMIA CHADEMA