RAIS MAGUFULI ATOA AHGIZO LA KIUCHUMI KWA BOT

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli ameitaka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kudhibiti matumizi ya fedha za kigeni katika biashara na huduma hapa nchini ili kulinda nguvu ya fedha ya Tanzania na kukabiliana na uhalifu wa kifedha.
Mhe.Magufuli ametoa agizo hilo leo wakati akifungua tawi la benki ya CRDB-LAPF Dodoma na kubainisha kuwa hatua hiyo itasaidia kuimarisha uchumi wa nchi.
Aidha,Mhe.Rais Magufuli ameitaka BOT kuongeza usimamizi wa benki zinazoendesha shughuli zake hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha zinajiunga na mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki na kufuatilia kwa ukaribu utendaji wake wa kila siku ili ziwe na manufaa kwa nchi.
Wakati huo huo Mhe.Rais Magufuli ameipongeza benki ya CRDB kwa kuendeshwa kwa ufanisi tangu ilipobinafsishwa kutoka Serikalini ambapo katika kipindi cha miaka 10 imelipa kodi serikalini kiasi cha Shilingi Bilioni 800,imetoa ajira kwa Watanzania 3,200,imetoa gawio Serikalini la Shilingi Bilioni 19.5 mwaka huu na imetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi Trilioni 3.5 ambapo Shilingi Trilioni 1 kati yake zimeelekezwa katika sekta ya viwanda na kilimo.
Rais Magufuli akizungumzia kuhusu kupungua kwa kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi Mhe.Rais Magufuli amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali zitakazoongeza kasi hiyo zikiwemo kupunguza kiwango cha kisheria cha sehemu ya amana za benki za biashara kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu kutoka asilimi 10 hadi 8,kushusha riba ya Benki Kuu mara mbili kutoka asilimia 16 hadi 9,kutoa mikopo maalum kwa benki za biashara,pamoja na Benki Kuu kununua fedha za kigeni kwenye soko la jumla la benki ili kuongeza ukwasi wa shilingi kwenye uchumi.
Mhe.Rais Magufuli ametoa wito kwa benki zote nchini kuanzisha matawi ya benki vijijini na kuwakopesha wajasiriamali ili waongeze uzalishaji hasa kilimo na viwanda na pia ametaka wananchi wanaopata mikopo wazingatie kurejesha.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Dkt.Charles Kimei amempongeza Mhe.Rais Magufuli kwa juhudi kubwa za kuimarisha uchumi zikiwemo ujenzi wa viwanda,ununuzi wa ndege,ujenzi wa reli ya kisasa (SGR),ujenzi wa barabara za juu (Flyover) ambapo ameahidi kuwa CRDB yenye matawi 469 na wateja 3,500,000 ikiwa ndio benki inayoongoza kwa mtandao mkubwa nchini,itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuwawezesha wajasiriamali na uwekezaji katika viwanda na kilimo.
Dkt. Charles Kimei na Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB Bw. Ally Laay wamekabidhi hundi ya Shilingi Milioni 100 kwa Mhe.Rais Magufuli kwa ajili ya kuchangia huduma za kijamii na Mhe.Rais Magufuli amekabidhi hundi hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt.Binilith Satano Mahenge kwa ajili ya ujenzi wa wodi katika hospitali ya Mkoa Dodoma.

Habari zaidi ni P5TANZANIA LIMITED

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA FUPI YA ABDULRAHMAN KINANA ALIYEJUZULU UKATIBU MKUU CCM

FAHAMU HISTORIA YA JOKETI ALIYETUMBULIWA NA UVCCM

HISTORIA FUPI YA LAZARO NYALANDU ALIYEIBWAGA CCM NA KUHAMIA CHADEMA