AFISA MTENDAJI WILAYANI MPANDA AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KWA TUHUMA ZA RUSHWA


Na.Boniface Mpagape-Mpanda
TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa mkoani Katavi, imemfikisha katika mahakama ya wilaya ya Mpanda  Afisa mtendaji wa mtaa wa Kawajense akikabiliwa na shtaka la kushawishi na kupokea rushwa ya shilingi elfu thelathini.

Taarifa ya TAKUKURU Mkoa wa Katavi kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo na Kaimu mkuu wa TAKUKURU Mkoani Katavi Bw. Christopher Nakua imesema kuwa afisa mtendaji huyo Bi. Catherine Kipeta, mnamo Jumatatu ya tarehe 18 mwezi huu aliomba rushwa ya shilingi elfu thelathini kutoka kwa mwananchi ili asimpeleke kwenye baraza la kata kwa kosa la kufungua sehemu ya biashara,muda wa kufanya usafi.
Amesema TAKUKURU Mkoa wa Katavi ilifanya uchunguzi wa awali na kuandaa mtego na kumkamata mshtakiwa baada ya kupokea rushwa kutoka kwa mwananchi huyo.
Mshtakiwa amefikishwa katika mahakama ya wilaya tarehe 19 mwezi huu na kusomewa mashtaka mawili yanayomkabili ambayo ni kuomba rushwa ya shilingi elfu thelathini na kosa la pili ni kupokea rushwa, kinyume na matakwa ya mwajiri wake na kifungu cha 15 (1)  (a) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
TAKUKURU mkoa wa Katavi inatoa wito kwa wananchi wote kujiepusha na vitendo vya rushwa ambavyo husababisha kutopatikana kwa haki, kutowajibika kwa watumishi wa umma, kwenda kinyume na maadili, kanuni na viapo vya utumishi, uvunjaji wa haki za binadamu, wananchi kukosa imani na idara, taasisi, mashirika mbalimbali ya serikali.
Aidha,Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa mkoani Katavi imesema kila mwananchi ana wajibu wa kutoa taarifa ya vitendo vya rushwa katika ofisi hiyo iliyopo Mpanda mjini, au kupitia simu ya bure namba 113.
Wananchi wanapaswa kutetea haki, kuzuia rushwa kwani rushwa ni adui wa haki, na penye sheria pana haki, penye haki pana amani, penye amani pana maendeleo.

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA FUPI YA ABDULRAHMAN KINANA ALIYEJUZULU UKATIBU MKUU CCM

FAHAMU HISTORIA YA JOKETI ALIYETUMBULIWA NA UVCCM

HISTORIA FUPI YA LAZARO NYALANDU ALIYEIBWAGA CCM NA KUHAMIA CHADEMA