WANAWAKE WAANDAMANA KUPINGA UBAKAJI KATIKA HOSPITALI KENYA
Makundi ya wanawake kutoka mashirika
tofuati nchini Kenya yameandamana hii leo kushinikiza serikali kuchukua hatua
kuhusiana na madai kuwa akina mama waliojifungua wamekuwa wakidhulumiwa kingono
katika Hospitali kuu ya Taifa Kenyatta National Hospital.
Maandamano hayo yanafanyika wakati ambapo ripoti ya uchunguzi
iliyoagizwa na waziri wa afya nchini humo ikitarajiwa kutolewa rasmi.
Waziri wa afya nchini Kenya Dkt.Cleopha Mailu aliagiza
uchunguzi kufanywa katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta baada ya wanawake
waliojifungua kudai kwamba wanadhalilishwa kingono.
Taarifa zilizoenezwa kwenye mitandao siku ya Ijumaa zinadai
kina mama waliojifungua wamekuwa wakishambuliwa na baadhi ya wafanyikazi wakati
wakienda kwenye chumba cha watoto wachanga kuwanyonyesha watoto wao.
Wanaotuhumiwa ni wahudumu katika vyumba vya maiti,
wanaonyooshewa kidole pia kwa kutumia maiti kuwashutua akina mama waliojifungua
katika hospitali hiyo.
Wanaharakati
wa kutetea haki za wanawake wanaoandamana leo katika mji mkuu, wanasema dhamira
yao kuu kumiminika barabarani ni kutaka mabadiliko yafanyike, na kwamba usalama
wa wanawake ni jambo linalopaswa kutiliwa umuhimu.
Mildred
Atty ambaye ni miongoni mwa waandaaji wa maandamano hayo amesema tatizo hilo limekuwa
likiendelea kwa muda usiojulikana na amesisitiza kuwa ni lazima liishe.
Hospitali
ya taifa ya Kenyatta,Nairobi huwahudumia akina mama wajawazito 100 wanaojifungua
kila siku.
Chanzo:bbc Swahili
Habari zaidi ni P5TANZANIA LIMITED
Comments