WATOTO PASUA VICHWA SUMBAWANGA
BARAZA la madiwani la halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa limeviomba vyombo vya usalama vishirikiane na idara ya uhamiaji kuwakamata na kuwarudisha nchini kwao watoto wa nchi jirani za Zambia na Congo DRC wanaoishi katika mazingira magumu. Mstahiki Meya wa Manispaa ya Sumbawanga Justine Malisawa alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akiongoza kikao cha baraza hilo baada ya wajumbe kulalamikia kuongezeka kwa watoto ambao wamekuwa kero na kujihusisha vitendo vya uporaji wa mali za raia pamoja na ubakaji. Mmoja wa madiwani hao Vitalis Ulaya alisema watoto hao wanazidi kuongezeka kila kukicha katika mji wa Sumbawanga hali ambayo ni hatari kwa kuwa hakuna jitihada za kutosha za kuweza kukabiliana na wimbi la ongezeko hilo. Alisema kuwa wengi wa watoto hao wanazurula nyakati za mchana wakiokota vitu majalalani na kuomba hela kwa wapita njia na nyakati za usiku wamekuwa wakifanya vitendo vya uhalifu hali inayosababisha amani kutoweka. ...