WATOTO PASUA VICHWA SUMBAWANGA
BARAZA la madiwani la halmashauri
ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa limeviomba vyombo vya usalama
vishirikiane na idara ya uhamiaji kuwakamata na kuwarudisha nchini
kwao watoto wa nchi jirani za Zambia na Congo DRC wanaoishi katika
mazingira magumu.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya
Sumbawanga Justine Malisawa alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akiongoza
kikao cha baraza hilo baada ya wajumbe kulalamikia kuongezeka kwa watoto ambao wamekuwa
kero na kujihusisha vitendo vya uporaji wa mali za raia pamoja na ubakaji.
Mmoja wa madiwani hao Vitalis Ulaya
alisema watoto hao wanazidi kuongezeka kila kukicha katika mji wa Sumbawanga
hali ambayo ni hatari kwa kuwa hakuna jitihada za kutosha za kuweza kukabiliana
na wimbi la ongezeko hilo.
Alisema kuwa wengi wa watoto hao
wanazurula nyakati za mchana wakiokota vitu majalalani na kuomba
hela kwa wapita njia na nyakati za usiku wamekuwa wakifanya vitendo vya uhalifu
hali inayosababisha amani kutoweka.
Kwa upande wake Ester Mpelele
mjumbe wa baraza hilo alisema watoto hao wamekuwa ni changamoto kubwa kwa
wanawake kwani hivi sasa hawawezi kutembea peke yao nyakati za jioni na usiku
hali ambayo aliiomba serikali kuingilia kati jambo hilo.
Aliwaomba wazazi katika Manispaa
hiyo ya Sumbawanga kuwajibika katika malezi ya watoto wao kwani kitendo cha
kuwaacha bila kuwapa huduma za msingi ikiwemo elimu wanawaandalia maisha mabaya
ya baadaye na watakuja kuisumbua jamii kutokana na kushindwa kuwajibika kwao.
Habari zaidi ni www.p5tanzania.blogspot.com
Comments