DAKTARI MTANZANIA AFUTWA KAZI NA MADIWANI
Daktari mmoja wilayani Kisarawe amefutwa kazi baada ya kukutwa na makosa mbalimbali yanayotia hofu juu ya utendaji kazi katika majukumu yake ya kila siku. Uamzi huo wa kumfuta kazi Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Mtakayo Emmanuel Shumbusho,umefikiwa na Baraza la Madiwani halmashauri ya Kisarawe mkoani Pwani. Dkt Emmanuel Shumbusho anatuhumiwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo uzembe,utoro kazini ambapo hajaonekana kazini kwa takaribani siku tisa bila taarifa yoyote kwa mwajiri wake. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Hamis Dikupatile akitoa maamuzi amesema,wamefikia hatua hiyo baada ya kubaini mapungufu mengi kutoka kwa mtumishi huyo. Madiwani wote kwa pamoja walikubaliana na uamzi huo kutokana na uzembe wa daktari huyo katika suala zima la utoaji wa huduma ya afya kwa wananchi na kusababisha kuibuka kwa usumbufu mkubwa kutokana na kutopatiwa matibabu kwa wakati.