TANZANIA YATAKIWA KUUNGA MKONO MGOGORO WA URUSI NA UINGEREZA


Serikali ya Uingereza imeitaka Tanzania na Jumuiya ya Kimataifa kuiunga mkono katika kupinga kitendo cha Urusi kutumia sumu aina ya novichok katika jaribio la kumuua jasusi wa Kirusi Sergei Skripal na binti yake Yulia.
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, Balozi wa Uingereza hapa nchini Sarah Cooke alisema nchi yake haitavumilia majaribio yoyote ya mauaji ya watu wasio na hatia ndani ya ardhi yake.
Cooke alisisitiza kuwa ni wazi Urusi ilihusika katika jaribio hilo na walipewa nafasi ya kueleza kwa nini waliamua kutumia sumu hiyo ndani ya Uingereza licha ya kwamba matumizi ya kemikali kama silaha ni kinyume cha sheria za kimataifa. Hata hivyo,alisema mpaka sasa hawajatoa maelezo kuhusu suala hilo.
Alipoulizwa kuhusu msimamo wa Tanzania kuhusu suala hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje,Dk Susan Kolimba alisema hawezi kulizungumzia kwa sasa ambapo hata Waziri wa Mambo ya Nje,Dk Augustine Mahiga hakupatikana ili kuzungumzia suala hilo .
Mpaka sasa Uingereza inaungwa mkono na Marekani, Ufaransa,Ujerumani,Austalia na Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (Nato) ambapo pia imeripoti suala hilo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Kufuatia hatua hiyo,Waziri Mkuu wa Uingereza,Theresa May ametangaza kwamba hakuna waziri yeyote au mtu kutoka familia ya kifalme atakayehudhuria Fainali za Kombe la Dunia zinazotarajiwa kufanyika Juni huko Urusi.
Tukio hilo la matumizi ya kemikali za sumu lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita huko Salisbury Uingereza na kwa sasa Skripal na Yulia wana hali mbaya hospitali.
Hata hivyo Uingereza tayari imewatimua maofisa 23 wa intelijensia wa Urusi na imefuta ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergey Lavrov.
Habari zaidi ni P5TANZANIA.BLOGSPOT.COM

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA FUPI YA ABDULRAHMAN KINANA ALIYEJUZULU UKATIBU MKUU CCM

FAHAMU HISTORIA YA JOKETI ALIYETUMBULIWA NA UVCCM

HISTORIA FUPI YA LAZARO NYALANDU ALIYEIBWAGA CCM NA KUHAMIA CHADEMA