SERIKALI KUAJIRI WATUMISHI 3100 WA SEKTA YA AFYA KABLA YA SEPTEMBA 30 MWAKA HUU-Agosti 16,2017



Waziri wa Afya Ummy Mwalimu
SERIKALI imesema inatarajia kuajiri watumishi wa sekta ya Afya 3100 wakiwemo 35 katika Halamshauri tano za Mkoani Katavi kabla ya Septemba 30 mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wazee na Watoto Mh.Ummy Mwalimu wakati akizindua zoezi la siku tano la upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza katika viwanja vya Polisi Mpanda Mjini.
Aidha Waziri Ummy pamoja na mambo mengine amesema kwa sasa nchi ina uhaba wa watumishi katika sekta ya afya kwa asiliamia 49 huku Mpanda pekee ikiabiliwa na Uhaba wa watumishi katika sekta hiyo kwa asilimia 69 ambapo serikali imeahidi kutoa kipaumbele kwa mikoa tisa ya pembezoni mwa nchi Ukiwemo mkoa wa Katavi yenye uhaba mkubwa wa watumishi.
Katika hatua nyingine Waziri Ummy amesema serikali itachukua hatua kali dhidi watendaji wa serikali watakaoiba fedha au kuzitumia vibaya fedha zilizotengwa kwa ajili ya dawa na kusababisha dawa hizo kukosekana katika hospitali.
Kwa upande wao Wabunge Mh.Sebastian Kapufi wa Jimbo la Mpanda Mjini na Mh.Anna Lupembe wa viti maalumu Mkoani Katavi wameiomba serikali kutatua changamoto za Hospitali ya Wilaya Mpanda ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu ambapo Waziri Ummy amesema serikali itaongeza bajeti ili hospitali iwe na uwezo wa kuhudumia wagonjwa kulingana na idadi ya wagonjwa katika Mkoa wa Katavi.
Bajeti ya dawa hapa nchni imeongezwa kutoka Shilingi Bilioni 31 kabla ya utawala wa Rais Magufuli na kufikia shilingi bilioni 269 tangu mwaka 2015 ambapo kwa mkoa wa Katavi bajeti imeongezwa kutoka Shilingi milioni 280 na kufika bilioni 1.3 zikiwemo Shilingi milioni 220 za hospitali ya Wilaya ya Mpanda ambazo ziliongezeka kutoka Shilingi milioni 106 kabla ya mwaka 2015 .
Wakati huo huo Waziri Ummy amesema pesa yoyote itakayopatikana atailekeza mkoani Katavi kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Katavi na ujenzi wa wodi ya wazazi na watoto ili kutatua changamoto ya zaidi ya mgonjwa mmoja kulala katika kitanda kimoja.
Kuhusiana na Mgao wa madaktari 258 waliotakiwa kwenda nchini Kenya kufanya kazi,kati ya hao madaktari 5 wameletwa Mkoani Katavi ambapo Manispaa ya Mpanda imepokea-watumishi 3,Halmashauri ya Nsimbo mtumishi -1 na Halmashauri ya Mlele mtumishi aliyepangiwa akiwa bado hajaripoti.
Nao baadhi ya wananchi Mkoani Katavi wameeleza kero zao ikiwemo ukosefu wa baadhi ya dawa pamoja kuuziwa vifaa tiba na walinzi wa getini katika hosiptali ya Wilaya ya Mpanda suala ambalo Waziri Ummy amelipiga Marufuku.
Wakati huo huo katika zoezi la upimaji wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele lilianza jana na kuzinduliwa leo na Waziri wa Afya,maendeleo ya Jamii,Jinsia Wazee na watoto Mh.Ummy Mwalimu,Zaidi ya wagonjwa 500 Mkoani Katavi wamejitokeza kupima afya zao na wengine kupatiwa matibabu katika zoezi la siku tano linaloendeshwa na madaktari bingwa wapatao 25 kutoka Dar es Salaam likisimamiwa na mbunge wa viti maalumu Mkoani Katavi Mh.Anna Lupembe.
Waziri Ummy anatarajia kuhitimisha ziara yake ya siku mbili kesho Mkoani Katavi ambapo anatembelea pia vituo vya huduma za afya Wilayani Tanganyika.

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA FUPI YA ABDULRAHMAN KINANA ALIYEJUZULU UKATIBU MKUU CCM

FAHAMU HISTORIA YA JOKETI ALIYETUMBULIWA NA UVCCM

HISTORIA FUPI YA LAZARO NYALANDU ALIYEIBWAGA CCM NA KUHAMIA CHADEMA