MATUKIO YA WIKI KATAVI NA TANZANIA KWA UJUMLA FEBRUARI 8—13,2016.


Posted By:Issack Gerald | At:Tuesday, February 09, 2016

Na. Agness Mnubi-Nsimbo
MAAFISA tarafa,Watendaji wa kata na vijiji wa Halmashauri za Nsimbo,Mlele na Mpimbwe wamepewa siku 4 za kutembelea shule za Msingi na Sekondari zilizopo katika Halmashauri zao ili kubaini upungufu wa madawati.
                                                 



Agizo hilo limetolewa jana na  Mkuu wa Wilaya ya Mlele Kanali Mstaafu Issa Suleiman Njiku katika kikao cha kamati ya ushauri ya Wilaya ya Mlele kilichofanyika katika Halmashauri ya Nsimbo,na kuwataka ifikapo February 12 kutoa taarifa za upungufu wa madawati.
Amesema wanatakiwa kushirikiana ili kuzunguka katika shule za sekondari na msingi  kufahamu idadi ya madawati yaliyopo na pungufu .
Amesema ifikapo february 28 Halamashauri hizo zinatakiwa kuwa zimetatua changamoto ya upungufu wa madawati, huku Mkoa ukizitaka Halmashauri zote kutataua tatizo hilo ifikapo mwishoni mwa   mwezi machi mwaka huu.
Halmashauri zote nchini zinatakiwa  kutekeleza agizo la Serikali kuwa hakuna mwanafuzi anayetakiwa kukaa chini ifikapo juni 30.

 

Posted By:Issack Gerald | At:Wednesday, February 10, 2016

Na.Issack Gerald-Mpanda
Chama cha walimu Tanzania (C.W.T) Mkoani Katavi,kimetoa tahadhari kwa wanachama wa chama hicho na watumishi wengine kuwa makini kutokana na utapeli kwa kimtandao ambao umejitokeza ukifanywa na watu wasiofahamika.

Tahadhari hiyo imetolewa na leo na Mwenyekiti wa C.W.T Mkoani Katavi Mwalimu Gerigori John Mshota wakati akizungumza na P5 TANZANIA MEDIA sambamba na Mpanda Radio Fm Ofisini kwake.
Amesema kuwa kumezuka makundi ya watu wanaojitambulisha kuwa ni Viongozi wa C.W.T  kikanda wakiwataka walimu wawape namba za akaunti za benki ili walipwe mishahara yao.
Aidha amesema kuwa Takribani watu wanne wakiwemo walimu walitapeliwa  milioni kadhaa na watu wasiowafahamu kwa kutumia mitandao ya mawasiliano.
Kati ya walimu wawili ambao wamepokea mawasiliano kutoka kwa matapeli mwezi Februari mwaka huu wakiwa katika harakati za kutapelewa yumo mmoja wa Shule ya Sekondari Mwangaza iliyopo Manispaa ya Mpanda.
Amesema kuwa amekuwa akijitambulisha kuwa yeye ni mlezi wa chama cha Walimu Tanzania C.W.T katika mikoa ya Rukwa,Katavi na Kigoma.
Kwa upande mwingine chama kimeliomba jeshi la polisi kusaidia kuwakamata watu wanaojihusisha katika wizi wa kutumia mitandao.
 Mwaka jana mbali na walimu kudai kutapeliwa wengi wa wananchi walisema kuwa walitapeliwa fedha zao ambapo wimbi hilo limeendelea kuwakumba waliowengi.
Katika hatua nyingine mwenyekiti wa C.W.T amewataka walimu waliokuwa wakifanya kazi kwa mkataba kutoka yaliyokuwa makazi ya wakimbizi na sasa makazi mapya,kuwa wavumilivu wakati madai yao ya kupatindishwa madaraja na stahiki nyingine zikiendelea kufanyiwa kazi na mamlaka husika.
Posted By:Issack Gerald | At:Tuesday, February 09, 2016

Na.Issack Gerald-Dodoma
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imebuni na kuanza kutekeleza Sera ya Uwekezaji ili kufikia lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi.
“Taarifa zilizopo zinaonyesha ni asilimia 10 tu ya Watanzania ndio wanaomiliki uchumi wa nchi na sera hiyo ndiyo inatoa mwongozo wa jumla unaohakikisha kwamba wananchi wanapata fursa mbalimbali za kiuchumi ambazo zitawawezesha kujenga na kufaidika na uchumi wa mchi yao,” alisema.
Waziri Mkuu amesema maeneo yanayolengwa na sera hiyo ni yale yenye kuleta matokeo ya haraka na yanayogusa maisha ya wananchi hasa katika sekta za kilimo, ufugaji, uvuvi, misitu, ujenzi, biashara, utalii, madini, viwanda na usafirishaji.
Ametoa kauli hiyo leo mchana wakati akizungumza na washiriki wa Mkutano wa Kwanza wa Wadau wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi nchini uliofanyika kwenye ukumbi wa kituo cha kimataifa cha mikutano cha mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Alisema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 inalenga kuhakikisha kuwa sehemu kubwa ya uchumi wa nchi yetu inamilikiwa na Watanzania wenyewe. Waziri Mkuu pia alizindua Mwongozo wa Utekelezaji Mkakati wa Taifa wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kufungua mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na Walemavu, Bibi Jenista Mhagama alisema hadi sasa mikoa 20 imekwishatenga maeneo ya uwekezaji kwenye halamhashauri zake  na imeanza kuweka miundombinu ya kuvutia wawekezaji.
Naye Mweyekiti wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Prof. Omari Issa alisema katika dunia ya sasa imebainika kuwa haina maana kumpatia mtu mkopo bila kumtafutia masoko au kumuunganisha wadau wa masoko. Kwa hiyo wamejipanga kuwasaidia Watanzania kwa kuwaunganisha na masoko.

Posted By:Issack Gerald | At:Wednesday, February 10, 2016


Na.Issack Gerald
WANAFUNZI wapatao 21 wanaosoma Shule ya Msingi Kilambo cha Mkolechi, Kata ya Kala mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi, wamefukuzwa shule kwa muda usiojulikana kwa kuvaa viatu maarufu yeboyebo.

Imeelezwa kwamba yeboyebo hizo zilikusanywa na kuchomwa kwa kile kilichoelezwa kwamba ni kunatokana na waraka uliotolewa na Ofisa Elimu Halmashauri ya Nkasi (Msingi) ukipiga marufuku wanafunzi kuvaa aina hiyo ya viatu shuleni.
Hata hivyo,akizungumza kwa njia ya simu akiwa mjini Namanyere wilayani Nkasi mkoani Rukwa, Ofisa Elimu Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi (Msingi), Misana Kwangula, alikanusha kutoa waraka huo kwa shule hiyo.
“Sina taarifa rasmi ila (Jumatatu) jioni  alinipigia simu mkazi mmoja akinitaarifu kwamba kuna mwalimu wa shule ya msingi Kilambo cha Mkolechi amechoma moto viatu vya wanafunzi kwa madai kuwa ofisa elimu (msingi) ametoa waraka kwamba wanafunzi hawatakiwi kuvaa yeboyebo shuleni…
“Hakuna waraka wala marufuku yoyote iliyotolewa, isitoshe sio sahihi hata kidogo wala sio kitu kizuri kuchoma vifaa walivyonavyo wanafunzi…. Sasa kama amewachomea wanafunzi hao viatu hivyo vya yeboyebo basi awanunulie viatu vya ngozi,” alisema Kwangula.
Mkasa huo wa wanafunzi hao kufukuzwa shule na kuchomewa yeboyebo walizovaa ulitokea juzi wakati wanafunzi hao walipofika shuleni wakiwa wamevaa viatu hivyo. Inaelezwa kwamba mwalimu wa zamu, Baraka Mwakasege aliwazuia kuingia darasani, badala yake akawaamuru wavue viatu vyao.
Taarifa kutoka shuleni hapo zinaeleza kuwa, baada ya hatua hiyo, mwalimu huyo wa zamu alizikusanya yeboyebo na kuzitia kiberiti kisha akawafukuza wanafunzi hao kwa muda usiojulikana hadi wazazi na walezi watakapowanunulia viatu vya ngozi.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Posian Ally alikanusha kumtuma mwalimu wa zamu kuwafukuza wanafunzi hao shule kwa muda usiojulikana wala kuteketeza kwa moto yeboyebo zao. Alisema ataitisha kikao ili kujadili suala hilo na kwamba mwalimu huyo akibainika kutenda kosa hilo ataamriwa kuwanunulia watoto hao viatu vingine.
Akizungumza mmoja wa wazazi wa wanafunzi hao, Privatus Yoram, alithibitisha kutokea kwa mkasa huo. “Jana jioni nilimwona mwanangu anayesoma darasa la tano shuleni hapo akirudi nyumbani akiwa peku.
Nikamuuliza kulikoni, akanieleza kuwa mwalimu wa zamu (Mwakasege) amewafukuza shule na kuchoma yeboyebo zao kutokana na waraka wa Ofisa Elimu Nkasi unaopiga marufuku yeboyebo shuleni,” alisema Yoram.

Posted By:Issack Gerald | At:Thursday, February 11, 2016
Na.Issack Gerald-Mpanda
Bweni la wavulana la Shule ya Sekondari ya Sanny inayomilikiwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) limeteketekea kwa moto na kuteketeza mali zote za wanafunzi.

Mkuu wa Shule ya Sanny Sisiter Anna Usiri amesema kuwa tukio hilo ambalo limetokea leo majira ya saa 12 Alfajiri hakuna mwanafunzi aliyepatwa madhara  kiafya mbali na mali zao zote kuteketea.
Aidha,Mkuu huyo wa shule,ametoa hofu wazazi wa wanafunzi hao kuwa hawatakosa  mahali pa kulala licha ya bweni lao kuungua ambapo pia wataendelea na masomo kama kawaida.
Amesema kuwa katika bweni hilo,vitu ambavyo vimetketea ni magodoro,sare za shule,baadhi ya daftari na vitabu.
Kwa upande wake kiongozi wa bweni hilo ambaye pia ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule hiyo Bw. Ansel Felisian amesema kuwa waliamka alfajiri ya saa 12 na kwenda darasani kusoma ambapo tukio hilo lilijulikana baada ya mwanafunzi wa kidato cha kwanza kutoa taarifa kwa kiranja huyo baada ya mlinzi wa shule kumwagiza akatoe taarifa juu ya hali hiyo.
Kwa upande wake Kamanda wa jeshi la Zimamoto na uokoaji Mkoani Katavi  Mrakibu Nestory Kisenya Konongo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema wamesaidia kuzima moto huo baada ya kupata taarifa za tukio hilo.
Shule hiyo ina wanafunzi 31 waliokuwa wakiishi katika bweni hilo huku shule hiyo change yenye kidato cha kwanza hadi cha tatu ikiwa na jumla ya wanafunzi 66 pekee.
Hata hivyo chanzo cha ajali hiyo ya moto hakijafahamika na uchunguzi unaendelea kufanyika

Posted By:Issack Gerald | At:Thursday, February 11, 2016

Na.Issack Gerald-Katavi
Miili 5 ya watu waliozama katika mto Koga uliopo mpakani mwa Mkoa wa Tabora na Katavi baada ya gari walilokuwa wakisafiria kusombwa na maji tarehe Januari 26 ,2016 hawajapatikana pamoja na gari walilokuwa wakisafiria.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama Mkoani Katavi ambaye pia ndiye Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dk.Ibrahim Hamis Msengi wakati akizungumza na P5 TANZANIA MEDIA Ofisini kwake.
Dk Msengi amesema kuwa mpaka sasa hakuna gari linaloweza kupita kutokana na maji yanayozidi kuongezeka kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na maji kujaa kwa wingi.
Katika hatua nyingine Dk Msengi amesema kuwa ukarabati wa barabara ya kutoka Mpanda hadi Tabora unaendelea kufanyika kwa kiwango cha lami isipokuwa eneo lilipo daraja la mto Koga ndipo bado kuna utata kutkana na wingi wa maji hayo.
Hata hivyo katika hali ya ukiukwaji wa onyo linalotolewa na viongozi,kuna watu wanaoendelea kusombwa na maji hayo kutokana na kudharau katazo hususabi wanaotoka Tabora kuja mpanda.
Posted By:Issack Gerald | At:Friday, February 12, 2016

Na.Issack Gerald-Rukwa
ASKARI wa kike wa Usalama Barabarani, Attuganile Mwakibete (37) na mpenzi wake Sunday Mhagama (36), wameteketea kwa moto baada ya nyumba walimokuwa ndani kuungua.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda amesema tukio hilo lilitokea Februari 2, mwaka huu saa 7:15 mchana katika kitongoji cha Maporomoko, Kata na Tarafa ya Laela Wilaya ya Kipolisi ya Laela.
Inadaiwa kuwa nyumba hiyo iliyoteketea kwa moto ambayo askari Attuganile alikuwa amepanga vyumba viwili, ni mali Yaiyela Mwamahonje aliyokuwa akiishi na watoto wake wawili wadogo ambao wamenusurika kufa, licha ya kuwemo ndani ya nyumba hiyo wakati wa ajali hiyo.
Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa Mhagama aliyekuwa rafiki wa trafiki huyo wa kike, ni mkazi wa Mbeya ambako mkewe anaishi, na alikuwa na mazoea ya kumtembelea mpenzi wake huyo mara kwa mara.
Inadaiwa askari Attuganile alikuwa ameachana na mumewe wa ndoa. “Vyumba viwili yaani sebule na chumba walimokuwemo Attuganile na Mhagama viliwaka moto baada ya jenereta lililokuwa likifanya kazi likiwa sebuleni humo kulipuka na kuwajeruhi vibaya,” alieleza.
Kwa mujibu wa Kamanda Mwaruanda,Attuganile alifariki dunia Februari 8, mwaka huu saa 2:30 asubuhi akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga.
Mhagama alikimbizwa na kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya jijini Mbeya ambako alifariki dunia Februari 9, mwaka huu ambapo hata hivyo kamanda Mwaruanda alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.
Chanzo:Jeshi la Polisi Rukwa,endelea kufuatilia P5 TANZANIA MEDIA

Posted By:Issack Gerald | At:Friday, February 12, 2016

Na.Issack Gerald-Katavi
Mtandao wa Radio za Jamii Tanzania (COMNETA) umetoa rai kwa viongozi wa ngazi mbalimbali kuanzia ngazi ya seriklai za mitaa mpaka ngazi ya taifa,kutumia radio mara kwa mara kwa lengo la kuelimisha na kufikisha ujumbe katika jamii kuliko kiongozi kutumia radio kwa wakati Fulani kwa maslahi binafsi.
Rai hiyo imetolewa leo na viongozi wa mtandao huo Tanzania na umoja wa Mataifa,wakati wa mahojiano na Shirika la Utangazaji Tanzania TBC kuhusu siku ya radio duniani ambayo inatarajia kuadhimishwa kesho duniani kote.
Katika mahojiano hayo, Mwenyekiti wa Mtandao huo Bw.Joseph Sekiku amesema kuwa redio za jamii Tanzania zimesaidia katika utatuzi wa migogoro baina ya wakulima na wafugaji  kwa kuelimisha jamii matumizi bora ya ardhi pamoja na kuunganisha watawala na watawaliwa kwa lengo la kudumisha amani na kutatu migogoro hiyo kwa mazungumzo.
Amewaasa viongozi wa umma katumia vyombo mbalimbali vya habari za kijamii kufikisha ujumbe kwa kuwa radio zipo kwa ajili kuelimisha,kuburudisha,kuasa na kuhabarisha.
Kwa upande wake Meneja wa Mpanda Radio Fm ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa  mtandao wa Radio  za jamii (COMNETA) Bw.Prosper Laurent Kwigize amesema kuwa vyuo mbalimbali vinavyoendesha mafunzo ya uandishi,utangazaji na taaluma yote ya habari kwa ujumla,vinatakiwa kuwa na wakufunzi wenye weledi wa taaluma ya habari  ili kupata watalaamu wa taaluma hiyo wenye uwezo wa kusaidia jamii na kuepuka kuendelea kuwa wanafunzi wanapopata kazi katika taasisi.
Aidha Bw.Prosper amesema kuwa wanasiasa wanatakiwa kutambua umuhimu wa radio hata baada ya kampeni za uchaguzi kufanyika kuliko kutambua vyombo vya habari wakati wa kampeni za kusaka kura pekee na baada ya hapo kutorejea kuzungumza na waliompigia kura ili watambue ni kitu gani kinachoendelea katika kushughulikia ahadi zake.
Katika mahojiano hayo,Bi.Stela Vuzo ambaye ni Afisa Habari kutoka umoja wa Mataifa aliyeko hapa nchini mbali na kuvitaka vyombo vya habari kufuata miongozo ya vyomvo vya habari kuepuka uvunjifu wa amani nchini.
Wakati huo huo,amewataka wanawake na vijana kutumia vyombo vya habari ikiwemo radio kwa ajili ya kutatua changamoto zinazowakabili na masuala ya kijasiliamali.
Kwa mjibu wa Shirika la kimataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni UNESCO limesema kuwa jumla ya watu milioni 20 duniani Kote wanasikiliza na kutegemea radio katika kuzungumzia masuala mbalimbali ya kijamii.
Maadhimisho ya siku ya Radio Duniani huadhimishwa ila mwaka ifikapo Februari 13,ambapo kwa mara ya kwanza maadhimisho haya yalifanyika mwaka 1946 kote duniani.
Kauli mbiu ya siku ya Radio Duniani REDIO  KAMA CHOMBO CHA HABARI WAKATI WA MAJANGA”.

Posted By:Issack Gerald | At:Friday, February 12, 2016

Na.Issack Gerald
SERIKALI imeamua kuwasimamisha kazi watendaji wawili kutoka Wakala wa Vipimo nchini (WMA) kuanzia leo ili kupisha uchunguzi wa upotevu wa mafuta bandarini kutokana na zuio la kufunga kwa mita kwa zaidi ya miaka mitano.
Waliosimamishwa kazi ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini (WMA), Bi. Magdalena Chuwa na Meneja Vipimo Kitengo cha Bandari, Bi. Bernadina Mwijarubi. Bi. Mwijarubi ndiye anashughulikia kitengo cha mafuta bandarini.
Akitangaza uamuzi huo kwenye kikao cha Makatibu Wakuu kilichofanyika leo Februari 12, 2016) ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Adelhelm Meru awaandikie barua za kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi huo.
 “Katibu Mkuu Viwanda, waandikie barua za kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi. Katika kipindi hiki hawatatakiwa kusafiri kwenda popote hadi uchunguzi utakapokamilika. Pia utafute mtu wa kukaimu nafasi hiyo ili kazi ziendelee,” alisema.
 Waziri Mkuu pia amesema ofisi yake itawaandikia barua ofisi ya TAKUKURU na polisi ili wafuatilie suala hilo mara moja na ikithibitika kuwa walihusika hatua rasmi zitachukuliwa na itathibitika hawakuhusika basi watarudishwa.
Waziri Mkuu pia aliagiza mfumo wa upimaji mafuta kwa kutumia flow meters uendelee kutumika na ule upimaji wa kukadiria uache kutumiwa mara moja.
Jana (Alhamisi, Februari 11, 2016) Waziri Mkuu alifanya ziara kukagua flow meters za zamani zilizopo Kurasini (Kurasini Oil Jetty) na kisha akatembelea na kukagua flow meters mpya ambazo zinajengwa Kigamboni. Mita hizo zimegharimu dola za marekani milioni 6 (sawa na sh. bilioni 12.96/- za sasa).
Pia Waziri Mkuu alitembelea sehemu ya kuchukulia mafuta yanayotoka bandarini (TPA Manfold) iliyoko Kigamboni na kukagua mitambo ya kusambazia mafuta kwenye matenki ya mafuta ya kampuni ya TIPER yaliyoko Kigamboni yanayomilikiwa kwa ubia baina ya Serikali na kampuni ya Oryx Energies.
Katika ziara hiyo ilibainika kuwa Kampuni ya TIPER imejiunganishia bomba la moja kwa moja kutoka kwenye bomba kubwa la mafuta linalotoka bandarini hali iliyomlazimu Waziri Mkuu kuagiza kwamba bomba hilo litolewe kwenye maungio hayo ndani ya mwezi mmoja.
“Jana niliagiza kuwa bomba hilo ling’olewe. Nimetoa mwezi mmoja ili kurekebisha mfumo huo. Simamieni vizuri na kuhakikisha kuwa na wao pia wanarudi kwenye manfold kama ilivyo kwa wengine,” alisema Waziri Mkuu.

 Saturday, 13 February 2016

IDARA YA ELIMU YATOA TAARIFA RASMI MFUMO MPYA WA WANAFUNZI SHULE ZA MSINGI KUFANYA MITHANI MWAKA 2016 MPANDA,SHULE ZISIZOSAJILIWA NJIAPANDA

Posted By:Issack Gerald | At:Saturday, February 13, 2016

Na.Issack Gerald-Mpanda
Idara ya elimu Shule za Msingi katika Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi,imewataka wazazi na walezi wa watoto wanaosoma katika shule ambazo hazijasajiliwa mkoani katavi ikisema kuwa kuna uwezekano wa wa kupoteza pesa nyingi na wanafunzi kukosa nafasi ya kufanya mitihani mbalimbali ya shule ya msingi inayotambuliwa na Wizara ya elimu,Sayansi,Teknolojia na ufundi.

Rai hiyo imetolewa jana na Afisa elimu Taaluma Elimu ya msingi Manispaa ya Mpanda Bw.Rashid Pili katika taarifa yake ambayo ameitoa kwa vyombo vya habari.
Amesema kuwa huenda wanafunzi wengi wakakosa kufanya mtihani yao kutokana na wengi wa wanafunzi kujiunga na shule ambazo hazijasajiliwa katika Manispaa ya Mpanda na hata Mkoa wa Katavi kwa ujumla.
Aidha Bw.Pili amesema kuwa mfumo mpya wa kufanya mitihani unaoanza mwaka 2016 unahusisha wanafunzi wa darasa la pili,la nne na la saba ambapo mithani hiyo itasimamiwa na balaza la mtihani la taifa(NECTA).
Hata hivyo wazazi wameshauliwa kuwahamisha watoto wao katika shule ambazo hazijasajiliwa na kuwapeleka katika shule za serikali zilizosajiliwa au zile za binafisi.
Kwa mjibu wa taarifa hiyo,katika Manispaa ya Mpanda kuna shule 34 za serikali zitakazokuwa na vituo vya kufanyia mtihani huku shule 2 pekee zinazofundisha Kiingereza za Reimeta English Medium School na Nzera English Medium Schoolsnazo pia zikiwa zimesajiliwa wanafunzi wake kufanya mtihani.
Katika hatua nyingine,Bw.Pili amesema kuwa usajili wa wanafunzi watakaofanya mtihani ngazi ya shule ulikwishakamilika mwaka huu ambapo usajili unaoendelea kwa sasa ni kwa ngazi ya Halmashauri wakati huo huo mchakato wa kuyaingiza majina ya wanafunzi hao katika mtandao wa balaza la Mtihani NECTA ukiendelea.
Miongoni mwa shule ambazo hazijasajiliwa kwa mjibu wa Afisa elimu huyo ni pamoja na shule ya msingi Motherland ambapo mpaka sasa ina wanafunzi wanaosomea katika shule hiyo.
Usikose kitachozungumzwa na shule zenye wanafunzi zikisemekana kutsajiliwa na wanafunzi kutofanya mitihani,endelea kuwa na P5 TANZANIA MEDIA na Mpanda Radio Fm

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA FUPI YA ABDULRAHMAN KINANA ALIYEJUZULU UKATIBU MKUU CCM

FAHAMU HISTORIA YA JOKETI ALIYETUMBULIWA NA UVCCM

HISTORIA FUPI YA LAZARO NYALANDU ALIYEIBWAGA CCM NA KUHAMIA CHADEMA