CUBA YAENDELEA KUSAIDIA TANZANIA KUPAMBANA NA MALARIA


Na.Issack Gerald-Katavi
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Cuba nchini, Bwana Jorge Luis Lopez Tormo ambaye ameahidi kuendelea kusaidia Tanzania katika mapambano dhidi ya malaria. 
                                                                        
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Balozi wa Cuba nchini, Mhe. Jorge Luis Lopez Tormo,  ofisini kwake jijini Dar es slaam Januari 11, 2016. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)

Akizungumza na Balozi  Tormo leo ,ofisini kwake ,Magogoni jijini Dar es salaa, Waziri Mkuu amemshukuru Balozi huyo, kwa Serikali ya Cuba kuendelea kusaidia Tanzania katika  mapambano  dhidi malaria  kwa kusaidia ujenzi wa kiwanda cha  kwanza Afrika cha  viuadudu vya kuua viluwiluwi wa mbu wanaoeneza ugonjwa wa malaria kilichopo, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani  kinachosimamamiwa na Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC).
 “Nawashukuru sana kwa namna mnavyosaidia kupambana na malaria, kupitia mradi huo mkubwa Afrika ambao unalenga kumaliza ugonjwa wa malaria,unaosababisha idadi kubwa ya vifo katika nchi yetu.” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Pia, ametumia fursa hiyo kuwakaribisha  raia wa Cuba kuja kuwekeza nchini hasa   katika  teknolojia. Na ameahidi kuendeleza uhusiano mwema ulipo baina ya nchi hizi mbili.
Waziri  Mkuu ameendelea kwa kusema kuwa Cuba ni nchi  iliyoendelea katika biashara, viwanda na uwekezaji  na imefanikiwa  kutoa bure huduma za kijamii ikiwemo afya, hivyo Serikali ya Tanzania haina budi kujifunza kutoka kwao ili kutimiza azma yake ya kutoa bure huduma mbalimbali za kijamii kama ambavyo sasa  inatolewa elimu bure.
Kwa upande wake, Balozi Tormo   amesema kuwa pamoja na Serikali ya Cuba kusaidia kutoa wataalamu katika kujenga kiwanda hicho cha   viuadudu vya kuua viluwiluwi wa mbu wanaoeneza ugonjwa wa malaria ambao utanufaisha pia nchi za jirani siku za usoni, wanapenda  kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika kuzalisha wataalamu kupitia programu mbalimbali  ikiwemo afya na elimu. Mfano progamu inayoendelea ya kubadilishana  wataalamu katika kitivo cha madawa cha Chuo Kikuu Cha Zanzibari (SUZA).
“Tunaweza kuendeleza program za kujifunza lugha ya Kiswahili, kama hapo awali, hii ni njia nzuri na muhimu ya kuendeleza uhusiano wetu na watu kuelewa lugha zetu”, alisema Balozi Tormo.
Chanzo cha habari : Ofisi ya Mwasilisno ya Waziri Mkuu.Endelea kuhabarika na P5 TANZANIA.

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA FUPI YA ABDULRAHMAN KINANA ALIYEJUZULU UKATIBU MKUU CCM

FAHAMU HISTORIA YA JOKETI ALIYETUMBULIWA NA UVCCM

HISTORIA FUPI YA LAZARO NYALANDU ALIYEIBWAGA CCM NA KUHAMIA CHADEMA