MATUKIO YA WIKI KUANZIA JUMATATU JANUARI 04— IJUMAA JANUARI 09,2015 MKOANI KATAVI NA TANZANIA KWA UJUMLA



NA.ISSACK GERALD BATHROMEO

Posted By:Issack Gerald | At:Monday, January 04, 2016

Na.Issack Gerald-MPANDA
Watu wawili wamekutwa wakiwa wameuawa na watu wasiojulikana Wilayani Mpanda Mkoani Katavi baada ya kukatwa na vitu vyenye ncha kali Januari Mosi Mwaka huu.
Mratibu wa Jeshi la Polisi Mkoani Katavi SSP Focas Malengo amesema,katika tukio la kwanza mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Tiho Robert (40) mkazi wa kitongoji cha Center John kijiji na kata ya Mwamkulu Wilayani Mpanda Mkoani Katavi,aliauawa majira ya saa tano za usiku.
Katika tukio hilo,marehemu alivamiwa na wauaji hao akiwa amelala nyumbani kwake baada ya kuvunja mlango na kuanza kumshambulia ambapo baada ya kutekeleza mauaji hayo walikimbia na kutokomea kusikojulikana.
SSP Malengo amesema,katika tukio lingine,mwanaume aliyekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25-30 aliuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali kichwani na shingoni na watu wasiofahamika ambapo alikutwa katika maeneo ya mtaa na kata ya Nsemulwa amjira ya saa mbili asubuhi.
Hata hivyo chanzo cha mauji ya watu ahawa hakijajulikana na Jeshi la Polisi limesema Linaendelea na upelelezi ili kuwabaini wahusika na kuwafikisha katika vyombo vya kisheria.

MLELE
Posted By:Issack Gerald | At:Monday, January 04, 2016

Na.Issack Mlele-Katavi
Mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Chalya Kichosha(60) mkazi wa mkazi wa kijiji cha Ibindi alikutwa akiwa ameuawa na watu wasiojulikana kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu za kichwani na shingoni.

Mratibu wa Polisi Mkoani Katavi SSP Focas Malengo amesem akuwa tukio hilo limetokea Mnamo tarehe 02/01/2016 majira ya saa sita usiku katika kitongoji cha Ipilito Ibindi kata ya Ibindi Tarafa ya Nsimbo Wilayani Mlele Mkoa wa Katavi.
SSP Malengo amesema,siku ya tukio,wauaji walifika nyumbani kwa marehemu majira ya usiku na kuvunja mlango kisha kuingia ndani na kisha kuanza kumshambulia  kwa kumkata sehemu za kichwani na shingoni hadi kupelekea umauti wake.
Chanzo cha mauaji hayo bado kujulikana. aidha, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wanakijiji cha ibindi linafanya msako ili kuweza kuwabaini wahusika wa tukio hilo.
Hata hivyo,Kamanda wa Polisi Mkoani Katavi anatoa wito kwa wananchi kuacha mara moja tabia ya kujichukulia sheria mikononi kwa kutoa uhali wa binadamu wenzao badala yake wafate taratibu za kisheria katika kuwasilisha jambo au malalamiko dhidi yao katika vyombo vya kisheria ili kushughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi. Aidha, anaitaka jamii iendelee kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kufanikisha operesheni na misako ya kuwabaini na kuwakamata wote wa mauaji haya ili kuendelea kutokomeza vitendo vya namna hii ndani ya jamii
MPANDA
Posted By:Issack Gerald | At:Monday, January 04, 2016

Na.Issack Gerald-MPANDA
Mahakama ya Mwanzo mjini Mpanda imemhukumu Bi. Agnes George (30) mkazi wa Kawajense mjini Mpanda kwenda jela kwa siku kumi na nne,  baada ya kupatikana na hatia ya kumkatakata kwa nyembe nyuma ya viganja mtoto wake mwenye umri wa miaka sita, akimtuhumu kuiba fedha.

Akitoa ushahidi mahakama hapo, askari polisi wa kata, WP 3207 Copral Regina, ameiambia mahakama kuwa tukio hili lilitokea tarehe 25 Mwezi Novemba mwaka 2015 majira ya saa 3 asubuhi, alipigiwa simu na mwenyekiti wa mtaa wa Kawajense Bw. William Richard maarufu maka Jumapili akimtaarifu kuwa mtaani kwake kuna mama amekatakata mwanaye kwa wembe na alienda kwenye eneo la tukio la kumkuta mtuhumiwa akiwa amewekwa chini ya ulinzi na mama wneye nyumba, pamoja na akina mama wengine watano.
Amesema alimweka chini ya ulinzi na alishuhudia mtoto aliyejeruhiwa akiwa anatokwa na damu nyuma ya viganja vya mikono yake huku nyama nyeupe ikiwa inaonekana.
Mtuhumiwa alibebwa kwenye bajaji kwa ushirikiano na mwenyekiti wa mtaa, hadi kituo cha polisi mjini Mpanda kwa hatua zaidi za kisheria.
Copral Regina ameiambia mahakama hiyo kuwa, baada ya kugundua mtoto aliyejeruhiwa ana umri mdogo na hawezi kujieleza aliamua kumfungulia Agnes George shtaka la kujeruhi na hati ya matibabu ilitolewa na mtoto huyo alipelekwa hospitali na mshtakiwa baada ya kupewa dhamana.
Taratibu za kumfikisha mahakamani mtuhumiwa zilifanyika na hatimaye leo amefikishwa katika mahakama ya mwanzo mjini Mpanda ili kujibu mashtaka yanayomkabili.
Mshtakiwa amekiri kutenda kosa hilo mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Bw. David Mbembela na kwamba ushahidi uliotolewa ni wa kweli.
Hakimu  Mbembela amesema mshtakiwa ametiwa hatiani chini ya kifungu cha sheria namba 228 namba 2. Akijitetea mahakamani hapo Mshitakiwa Agnes George aliiomba mahakama imsamehe kwa kosa la kujeruhi mtoto wake na kwamba hatarudia tena hata kama mtoto huyo akirudia kuiba fedha atamfikisha polisi.
Akitoa hukumu Hakimu Mbembela amesema kulingana na kosa alilotenda mshtakiwa adhabu yake ni kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela, lakini kwa kuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza ingawa mazingira yanaonesha alifanya kosa la unyanyasaji na hakupaswa kujichukulia sheria mkononi, hivyo mahakama imezingatia maslahi na umri wa mlalamikaji kwa kuwa bado anamtegemea mshtakiwa.
Mahakam hiyo imemhukumu kifungo cha siku 14 gerezani ili iwe fundisho kwa watu wenye tabia za unyanyasaji na kuagiza polisi ishirikiane na maafisa ustawi wa jamii kuhakikisha mhanga anapata uangalizi na pindi akitoka gerezani itabidi alipe gharama zitakazotumika kwa matunzo ya mtoto wake wakati akiwa gerezani. 


Posted By:Issack Gerald | At:Monday, January 04, 2016

Na.Issack Gerald.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefurahishwa na hali ya chakula mkoani Ruvuma, ikiwa kati ya mikoa inayotegemewa kwa uzalishaji wa chakula kwa wingi nchini.
 Akizungumza na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali jana jioni (Jumapili, Januari 3, 2016) katika ukumbi uliopo Ikulu ndogo Songea, Waziri Mkuu  ameutaka  uongozi wa mkoa kuhakikisha kuna  upatikanaji wa masoko kwa mazao mbalimbali pamoja na kuendelea kutoa msukumo kwa wananchi.
Pia, amewapongeza viongozi wa mkoa huo kwa kutoa msukumo kwa wananchi na kufanyakazi, na kusema ni jambo linalosaidia kupanda kwa pato la mtu mmoja  mmoja, hata hivyo hakusita kuwashukuru kwa mapokezi makubwa aliyopata.
“Nawapongeza sana wana Ruvuma kwa kuongeza pato la ndani kutoka kutoka shilingi 654,227, hadi kufikia shilingi 1,800,000 kwa kipindi cha mika 4 tuendelee kujiweka vizuri kwa kuongeza pato la mtu mmoja mmoja” alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu Majaliwa pia amesisitiza  kilimo cha umwagiliaji katika maeneo yote yenye mabonde ili wakulima waweze kuvuna bila kutegemea sana kipindi cha masika. Amesema ni lazima kuimarisha huduma muhimu na kusisitiza matumizi mazuri ya fedha zinazopatikana  katika mazao hayo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Thabit Mwambungu amesema  zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wa Ruvuma hutegemea kilimo cha mazao  mbalimbali ya chakula na biashara  yakiwemo mahindi, mpunga ambao unalimwa sehemu za Tunduru na Songea vijijini, korosho  ambazo zinalimwa sehemu za Tunduru, Namtumbo, Nyasa, Mbinga na Songea vijijini na tumbaku  maeneo ya Namtumbo,Mbinga na Songea vijijini.
Alisema, Ruvuma imekua ikizalisha chakula kwa kiwango cha utoshelezi na ziada kwa kipindi cha mwaka 2012 - 2013, 2013 - 2014 hali hiyo imeendelea kuwa nzuri hadi kipindi cha mwaka 2015 - 2016. Mahitaji yakiwa ni tani 469,172 na ziada ikiwa tani 1,950,111, ametaja baadhi ya sababu za ongezeko hilo la tani  ni pamoja na matumizi ya dhana  bora za kilimo, matumizi ya pembejeo za kisasa na urahisi wa upatikanaji wa pembejeo, aliongeza Mkuu wa Mkoa.
Waziri Mkuu Majaliwa ambaye jana (Jumapili, Januari 3, 2016) ameanza ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Ruvuma, kesho  siku ya jumatatu  atakuwa na shughuli za kufungua  tawi la Benki ya Posta mjini Songea, kukagua  maghala ya Wakala wa Taifa wa  Hifadhi ya chakula  (NFRA) kanda ya Songea na kukagua  Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Kupitia ziara hii Serikali ina lengo la kuona hali halisi ya utendaji wa shughuli za maendeleo kutoka kwa watendaji mbalimbali, kuwatia moyo na kuweka msisitizo  katika maeneo yaliyopewa kipaumbele hasa katika sekta ya Afya.



Posted By:Issack Gerald | At:Tuesday, January 05, 2016

Na.Issack Gerald-Geita
Viongozi wa Mkoa wa Geita wametakiwa wasiwaonee aibu kuwafungia wafanyabiashara wasiofuata kanuni za usafi wa mazingira na hivyo kupelekea mlipuko wa kipindupindu.

Hayo yamesema na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati alipotembelea kambi ya wagonjwa ya kipindupindu iliyopo kwenye kituo cha afya Nyankumbuli mjini Geita.
Waziri Ummy alisema mlipuko wa  kipindupindu upo hivyo kuwafumbia macho wale ambao wanafanya biashara katika mazingira yasiyo safi na salama lazima watu hao wafungiwe
“ Wanasiasa wenzangu inabidi mtuelewe ,hivi  sasa kuna mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika mikoa ishirini na moja na ni haki ya kuhakikisha afya za wananchi zipo safi na salama hivyo tutaruhusu biashara zilizopo kwenye mazingira safi na salama na endapo tutakua tumejiridhisha kwamba  wafanyabiashara wamezingatia kanuni za usafi wa mazingira”
 Aidha, ameupongeza mkoa wa Geita kwa jitihada za kudhibiti wagonjwa wapya kwa wiki hii kuliko wiki iliyopita ambapo kwa wiki hii kuna wagonjwa wapya wanne,ukilinganisha na wagonjwa nane wa wiki iliyopita,hivyo  ameutaka mkoa kuendelea kutoe elimu kwa wananchi kuhusu ugonjwa huu.
Wakati huohuo waziri Ummy amewataka watumishi wote wa kada za afya nchini kufanya kazi kwa mujibu wa maadili na kwa kuzingatia viapo vya fani zao wakati wanapotoa huduma kwa wananchi
Ummy alisema serikali haitowaonea aibu  kuwachukulia hatua kali kwa kila mtumishi atakayetoa lugha mbaya na kukiuka maadili ya kazi zao wakati wa kutoa huduma kwa wananchi.
“Hatua kali tutachukua kwa yule atakayebainika ametoa lugha isiyostahiki na inayomdhalilisha  mgonjwa, hatutomvumilia kwakweli na hili tutashirikiana na wenzetu wa Tamisemi kulifanyia kazi.
Awali, akisoma taarifa ya Mkoa wa Geita kuhusu hali ya kipindupindu ,Mganga Mkuu wa mkoa Dkt. Joseph Kilasa alisema Mgonjwa wa kwanza alipatikana mwezi wa tisa mwaka jana ambapo  walipata mgonjwa wa kwanza toka mji wa katoro ambaye alitokea jijini dare es salaam.Hadi sasa wamepata jumla ya wagonjwa 116 na watu saba  7 walipoteza maisha
Posted By:Issack Gerald | At:Tuesday, January 05, 2016

Na.Issack Gerald-SUMBAWANGA
Jeshi la Polisi Mkoani Rukwa limesema kuwa,hakuna matukio matukio ya uharifu yaliyotokea katika kipindi chote cha msimu wa sikukuu za kuuaga mwaka 2015 na kuukaribisha mwaka 2016.
Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Polisi Mkoani  Rukwa SACP Jacob Mwaruanda wakati akizungumza na P5 TANZANIA MEDIA Kwa nji aya simu,kuhusu Tathmini ya hali ya usalama katika sikukuu za krismas Desemba 25 na mwaka mpya 2016.
Amesema kuwa tukio pekee lililotokea msimu wa sikukuu ni linamhusisha mtu mmoja mtembea kwa mguu aliyekufa baada ya kugongwa na pikipiki Mjini Sumbawanga.
Aidha Kamanda Mwaruanda amesema,matukio makubwa yalitokea kwa mwaka 2015 ni pamoja na Mauaji ya mtoto mwenye ulemavu wa ngozi Albino na kuchomwa vifaa vya kupigia kura pamoja na gari wakati wa uchaguzi wa mwaka jana wa urais,ubunge na udiwani.
Katika matukio ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi albino Mkoani Rukwa,ni pamoja na tukio la mwezi machi mwaka 2015 ambapo Mtoto mwenye ulemavu wa ngozi albino Baraka Cosmas (6) aliyekuwa akiishi na wazazi wake kijijini Kipeta, Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga alishambuliwa na kujeruhiwa vibaya kwa kukatwa kiganja cha mkono wake wa kulia na watu wasiojulikana kisha kutokomea nacho kusikojulikana.
Hata hivyo Kamanda Mwaruanda amesema mashauri ya watuhumiwa wa ukatiri kwa mtoto huyu mwenye albino yanaendelea mahakamani.
Wakati huo huo wakazi wa Mkoa wa Rukwa,wametakiwa kushirikiana na Polisi kwa kuripoti matukio ya uharifu kabla hayajasababisha madhara kwa watu.
Posted By:Issack Gerald | At:Wednesday, January 06, 2016

Na.Issack Gerald-MPANDA
JUMLA ya Walimu  120 wa Shule za msingi kutoka halmashauri 8 za  Mikoa ya Rukwa, Kigoma na Katavi wanashiriki mafunzo ya kuwajengea uwezo walimu na wanafunzi katika ufundishaji na ujifunzaji ili kuboresha taaluma na kuongeza kiwango cha  Ufaulu kitaifa.

Akifungua Mafunzo hayo katika Shule ya Sekondari Mwangaza Manispaa ya Mpanda Mgeni rasmi, Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Katavi Said Mwapongo, amewataka walimu walioshiriki mafunzo kuhakikisha wanawajengea uwezo walimu wenzao ambao hawakushiriki mafunzo hayo.
Mafunzo hayo yanalenga walimu wa masomo ya Kiswahili, kingereza na hisabati, ikiwa Sehemu ya mpango wa Matokeo makubwa sasa (BRN), yalioandaliwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, na yameanza  Januari 4 na yatamalizika Januari 8 mwaka huu.
Baadhi ya wajumbe wa semina hiyo wamesema kuwa,walimu hao kupatiwa mafunzo hayo kutaongeza ufanisi katika kutekeleza haraka mpango wa Mtokeo Makubwa sasa na kupunguza idadi ya wanafunzi wanaoshinwa kufaulu mithani kwa kiwango kikubwa.
Hivi karibuni Wakati Mkoa wa Katavi ukishika nafasi ya kwanza kitaifa katika matokeo ya darasa la saba,Mkoa jirani wa Rukwa kwa mjibu wa Mkuu wa Mkoa wa mkoa huo Magalula Said Magalula,amesema mkoa huo umeshika nafasi ya tatu kutoka mwisho katika shule za msingoi zilizofanya mtihani wa darasa la saba kwa mwaka 2015.


Posted By:Issack Gerald | At:Wednesday, January 06, 2016

Na.Issack Gerald
Waziri wa Maliasili na Utalii Prof.Jumanne Maghembe amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Bw.Mohammed Kilongo na Maofisa wa Misitu wa Mikoa nchi nzima kupisha uchunguzi wa upotevu wa mapato ya Serikali.
Akizungumza jana na Waandishi wa Habari Makao Makuu ya Wizara hiyo Dar es Salaam, Prof. Maghembe amesema agizo hilo limekuja kutokana na ubadhilifu unaofanywa na Maofisa wa ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali yanayotokana na rasilimali za misitu katika Mikoa na Wilaya kwa kutowasilishwa katika mfuko Mkuu wa Serikali.
Ameagiza pia maofisa hao wote wanaokusanya mapato ya Serikali katika Wilaya watumie muda wa siku kumi kuanzia
jana kuhakikisha mapato yote yaliyokusanywa yanapelekwa benki ikiwa ni pamoja na kukabidhi vitabu vya kukusanyia mapato kinyume cha hapo watachukuliwa hatua
kali za kisheria.
Kwa mujibu wa Waziri Maghembe Bw.Mohammed Kilongo ambaye Idara yake ndiyo inatoa vitabu kwa ajili ya kukusanya
maduhuri ya Serikali katika Mikoa yote na Wilaya zote nchini analazimika kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi ambapo  ukikamilika sheria itachukua mkondo wake bila uonevu wowote.  
Katika hatua nyingine Waziri huyo wa Maliasili na Utalii amewaagiza pia Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS)
kutumia muda wa siku saba kurudi katika jengo la Wizara ya Maliasili na Utalii maarufu kama Mpingo House ambalo walihama mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka
jana na kwenda kupanga katika jengo la NSSF Mafao House lililopo Ilala.
Ameitaka pia Idara ya Misitu na nyuki kupitia Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kuhakikisha kuwa inaongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa kuziba mianya yote ya ubadhilifu pamoja na kuanzisha vyanzo vipya vya mapato na kuboresha vyanzo vilivyopo.
Akizungumzia mchango wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kwenye pato la taifa Mtendaji Mkuu, Bw. Juma Mgoo
amesema katika mwaka huu wa fedha,TFS imeweka makisio ya kukusanya Tsh.Bilioni 88 ambapo mpaka hivi sasa wameshakusanya zaidi ya asilimia 20 na makisio hayo.
Aidha Waziri Maghembe akizungumzia kuhusu uvamizi kwenye hifadhi za taifa na mapori ya akiba,amewataka wananchi
wote waliovamia maeneo ya hifadhi za taifa kwa ajili ya kuchunga mifugo kuondoka ndani ya siku saba zijazo, hku waliovamia mapori ya akiba kwa shughuli za kilimo na ufugaji wakitakiwa ndani ya miezi mitatu ijayo.
RUVUMA
Posted By:Issack Gerald | At:Wednesday, January 06, 2016

Na.Issack Gerald-Ruvuma
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametembelea kiwanda cha kusindika  tumbaku  cha mkoani Ruvuma na kuwasimamisha kazi viongozi wa Chama Cha Kikuu Cha Ushirika cha SONAMCU.
Akizungumza  jana katika ukumbi wa mikutano wa Ikulu Ndogo ya Songea, wakati alipokutana na wakulima wa zao la tumbaku wa Wilaya ya Namtumbo, Wananchama wa Vyama Vya Ushirika vya Mkoa wa Ruvuma, viongozi wa Mkoa pamoja na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Edwin Ngonyani ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini.
Waziri Mkuu amesema, Serikali ina dhamira ya kufufua kiwanda cha kusindika tumbaku cha SONAMCU, na lengo la kutembelea kiwanda hicho ni katika utekelezaji wa agizo la Rais John Pombe Magufuli la kufufua viwanda nchini.
Waziri Mkuu Majaliwa, ametembelea maeneno mbalimbali ya kiwanda hicho na kukagua mitambo iliyokua ikitumika kusindika tumbaku, kabla kiwanda hicho kuzimwa miaka kadhaa iliyopita  baada ya kukosa malighafi za kuendelea na uzalishaji.
Pia, amemtaka Afisa Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Bibi. Stela Lugongo kuandaa na kuwasilisha kwake mkakati wa kufufua kiwanda hicho cha kusindika tumbaku, na baadae kuwasimamisha kazi viongozi wote wa Chama Kikuu cha Ushirika cha SONAMCU waliohusika na tuhuma hizo na kutaka wafikishwe Mahakamani.
“Serikali imeazimia kufufua viwanda, hasa vile ambavyo havina wawekezaji vimebaki vyenyewe, Tunahitaji kujua namna ya kuvifufua”. Alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa.
Waziri Mkuu Majaliwa pia, amesikiliza  na kujibu kero mbalimbali za wakulima wa tumbaku wa Mkoa huo, ambao walilalamikia  mfumo wa Vyama vya Ushirika na namna ambavyo vyama hivi vimekua vikiwaibia fedha zao  hadi kushindwa kuendelea kulima zao la tumbaku na kukosa masoko ya mazao yao.
Aidha, Waziri Mkuu amewasihi wakulima kuwa watulivu na kusubiri maamuzi ya Mahakama baada ya kuwa viongozi wa Chama cha Ushirika SONAMCU ambao wamehusika na wizi wa fedha za wakulima kiashi cha Shilingi milioni 800 kwa kipindi cha mwaka 2011 hadi 2014 tayari wamefikishwa Mahakamani na uchunguzi unaendelea. Pia, amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu kukutana na wakulima hao ili kupatia ufumbuzi matatizo yao.
Aidha, ametoa wito kwa wakulima kuendelea kulima zao la tumbaku kwa kuwa linaongeza pato la mtu mmoja mmoja, linasaidia kuchangia pato la Mkoa na kukua kwa uchumi wa nchi. Amewashauri wakulima kuunda  na kuviendesha Vyama Vya Ushirika kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Waziri Mkuu amemaliza ziara yake mkoani Ruvuma, atafanya majumuisho ya ziara hiyo leo, kabla ya kuagana na viongozi wa Chama na Serikali na kurejea jijini Dar es Salaam.
Posted By:Issack Gerald | At:Wednesday, January 06, 2016

Na.Issack Gerald-Mlele Katavi
Watu watatu wamekufa katika matukio mawili tofauti Wilayani Mlele Mkoani Katavi likiwemo tukio la baba na mwanae kuliwa na samba jike mzee.
Katika tukio la kwanza,akithibitisha kutokea kwa tukio hilo,Kamanda wa Polisi Mkoani Katavi Dhahiri Kidavashari amesema kuwa tukio hilo limetokea mnamo Januari 4 mwaka huu majira ya saa ya saa 3 usiku katika maeneo ya kitongoji cha makaburi wazi kata ya Starike Tarafa ya Nsimbo Wilayani Mlele Mkoa wa Katavi.
Kidavashari amesema,wawili waliofahamika kwa majina ya  John Jeremiah (41) mkazi wa Matandarani na Patrick John (05) ambaye ni mtoto wa marehemu John Jeremiah wote kwa pamoja waliuawa kwa kushambuliwa vikali na simba jike mzee.
Kamanda Kidavashari amesema,katika tukio hilo,simba huyo alifika katika nyumba ya marehemu ya  John Jeremiah  ambayo ni kambi ya muda kwa ajili ya uangalizi wa mashamba na kuanza kushambulia kuku wawili, ambapo punde aliingia ndani ya kaya ya marehemu John Jeremiah na kumshambulia vibaya sehemu za siri, shingoni na kichwani ambapo licha ya kupiga kelele za kuomba msaada ziliweza kusikika kwa majirani hakupata msaada wa haraka kuokoa maisha yake.
Baada ya hapo simba huyo alimchukua marehemu Patrick John mpaka vichakani na kuanza kumla nyama ambapo Mpaka kufikia alfajiri ya siku ya tukio kabla ya simba huyo kuuawa,alikuwa amembakiza marehemu kichwa na mikono.
Kuhusiana na tukio hilo,Kamanda Kidavashari amesema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na askari wa wanyama pori TANAPA walifanya msako na kufanikiwa kumkuta simba huyo akiendelea kumla nyama Patrick John ambapo hata hivyo samba huyo aliuawa.
Katika tukio la Pili,mtu mwingine aliyefahamika kwa jina la Heleni Malelemba(40) mkazi wa kitongoji cha Uzumbura aliuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni na kichwani na watu wasiojulikana.
Aidha Kamanda wa Polisi Mkoani Katavi Dhahiri Kidavashari amesema kuwa tukio hilo,limetokea Januari 4 mwaka huu majira ya saa saba usiku katika kitongoji cha Uzumbura kijiji cha Ikuba, Tarafa ya Mpimbwe, Wilayani Mlele.
Amesema kuwa,siku ya tukio,marehemu alikuwa anaendesha pikipiki aina ya TOYO rangi Nyekundu isiyokuwa na namba za usajili akitokea senta ya usevya kuelekea nyumbani kwake Uzumbura, ambapo akiwa njiani ndipo alipoviziwa na watu wasiojulikana na kufanyiwa mauaji hayo kisha watuhimiwa kutokomea kusikojulikana pasipo kuchukua pikipiki ya marehemu.
Chanzo cha tukio hili bado hakijafahamika na upelelezi unaendelea kwa kushirikiana na wakazi wa eneo la Tarafa ya Mpimbwe ili kubaini sababu iliyopelekea mauaji haya ambapo Mpaka sasa hakuna watu walioshukiwa na kukamatwa kuhusiana na tukio hili ili sheria iweze kuchukua mkondo kwa wahusika wote.
Kufuatia matukio hayo,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi anatoa wito kwa wananchi hasa wakulima na wafugaji ambao shughuli zao huzifanya au hutegemea porini au mazingira karibu na mbuga za wanyama,kuzingatia usalama wao kwanza kwa kuhakikisha wanakuwa makazi imara na salama dhidi ya wanyama wakali wa porini.Pia, anaendelea kuwaonya watu wanaopenda kujichukulia sheria mikononi kuwa hatua kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa dhidi yao.

MWANZA
Posted By:Issack Gerald | At:Wednesday, January 06, 2016

Na.Issack Gerald-Mwanza
Watu wawili  akiwemo askari wa Jeshi la Polisi wanashikliwa  na jehi la polisi kwa makosa ya mauaji katika maeneo tofauti Mkoani Mwanza.
Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza Justus Kamugisha amesema katika tukio la kwanza,Askari wa Jeshi la Polisi PC F.4965 Joel Francis (41)wa kambi ya polisi Mabatini  wilayani Nyamagana mkoani Mwanza anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za mauaji dhidi ya Rafiki yake.
Kamanda wa Polisi Mkaoni humo SACP Justus Kamugisha amemtaja aliyeuwawa kuwa ni Donald Magalata(30)aliyekuwa milinzi wa Mwanza hoteli ambapo amesema,tukio hilo limetokea Januari mosi mwaka huu.
Kamanda Kamugisha ameeleza kuwa PC Francis, januari mosi mwaka huu majira ya saa 7:00 usiku alimfunga pingu miguuni ndani mwake na kumpiga kwa madai kuwa pochi yake  iliyokuwa na vitu vyake haikuonekana na kuhisiwa kuwa aliiba.
Hata hivyo Marehemu alijaribu kuomba msaada kwa majirani ambapo walifika eneo la tukio na kumpeleka hospitali ya Rufaa ya Bugando na kufariki dunia usiku wa kuamkia januari 02 mwaka huu.
Aidha  Kamanda Kamgisha ameeleza kuwa Mtuhumiwa anashikiliwa na polisi na atafikishwa mahakani pindi uchunguzi wa tukio hilo utakapo kamilika.
Wakati huo huo katika tukio la pili,Kamanda Kamgisha amesema,Mwana mme moja mkazi wa Izunge Bwiro wilayani Ukerewe mkoani Mwanza anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za mauaji  baada ya kugombania mwanamke katika ukumbi wa disco kijijini humo.
Kamanda wa polisi mkoani Mwanza SACP Justus Kamugisha amesema kuwa tukio hilo limetokea January 2 mwaka huu majira ya saa 6 usiku na kumhusisha Bw Michael Charles(26) aliyemuua  Ngereja Mashenene(30).
Kamanda Kamugisha ameeleza kuwa Bw Michaele Charles alimchoma kisu kifuani Bw  Ngereja baada ya kugombania mwanamke katika ukumbi wa Disko jina lake limehifadhiwa na baadae akafariki dunia wakati akipelekwa Hospitalini.
Aidha Mtuhumiwa amekamatwa na upelelezi wa shauri hili utakapo kamilika atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazo mkabuili.
MWANZA
Posted By:Issack Gerald | At:Wednesday, January 06, 2016

Na.Issack Gerald-Mwanza
Muuguzi wa Kituo kinacho toa huduma kwa watu wanaoishi na maambukizi ya Virus Vya UKIMWI na Yatima Shalom Care House Jijini Mwanza  Bi Edna Evarist amesema uelewa mdogo  wa watu wanaoishi Na VVU ni changamoto katika kudhibiti UKIMWI nchini.
Bi Evaristi ameyasema hayo wakati  akizungumza na Redio Kwizera Juu ya kauli mbiu ya taifa chini ya wizara ya afya na usitawi wa jamii kufikia sufuri tatu  katika kudhibiti maambukizi mapya ya VVU, vifo vitokanavyo na VVU Na unyanyapaa.
Amesema kuwa watu wenye virusi vya UKIMWI wengi wao wamekuwa wakiendeleza maambukizi hayo kwa kuoa na kuolewa au kuanziasha mahusiano mapya bila kuwahusisha wenzi wao huku wakijua hali zao kiafya na kusababisha maambukizi  ya UKIMWI nchini kuendelea.
Aidha mratibu wa kituo hicho Bw Msafiri Wana amesema kuwa Idadi ya watoto yatima kutokana na vifo vianavyo sababishwa na Ukimwi imepungua baada ya jamii kujua umuhimu wa matumizi sahihi ya dawa za punguza  makali ya VVU.
Posted By:Issack Gerald | At:Wednesday, January 06, 2016

Na.Issack Gerald-Dar es Salaam
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali haijaridhia viwango vipya vya nauli ya mabasi yaendayo kasi vilivyopendekezwa na waendeshaji wa huduma ya mabasi yaendayo kasi Dar es salaam (UDART).
Akizungumza  leo na waandishi  wa habari, mara baada ya kuwasili katika  Uwanja wa Ndege wa Kimataifa  wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam akitokea mkoani Ruvuma kwa ziara ya siku 3, Waziri Mkuu amesema  Serikali haijaridhia viwango vipya vya nauli ya mabasi yaendayo kasi ambapo nauli ya kutoka Mbezi hadi Kimara shilingi 700, Mbezi hadi Kariakoo shilingi 1200, na nauli ya kutoka Mbezi hadi Mwenge shilingi 1400 na wanafunzi watatozwa nusu ya viwango hivyo vya nauli.
Waziri Mkuu amesema gharama hizi ni kubwa mno kwa wananchi na watumishi huku mradi huo ukiwa umelenga kumrahisishia mtumishi wa Serikali anayeishi nje ya jiji, “Serikali iliwekeza katika mradi huu ili kusaidia watumishi na wananchi ambao hawana vipato vikubwa” alisema Waziri Mkuu.
Aidha, ameagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa George Simbachawene  na  Waziri wa Ujenzi , Uchukuzi, na Mawasiliano pamoja na wadau wakutane  kupanga upya  viwango hivyo na kama watashindwa basi Serikali  itaendesha mradi huo.
Tarehe  25, Novemba 2015, Waziri Mkuu alimuagiza aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya TAMISEMI na waendeshaji wa  mradi wa mabasi yaendayo kasi Dar es salaam (UDART) kupitia misuada yote na kurekebisha miundombinu  ili mradi huo wa mabasi uanze kufanya kazi ifikapo tarehe 10, Januari 2016, imebainika kwamba  UDART hawakuandaa mpango wa biashara  wala kuanisha gharama za uendeshaji.
Posted By:Issack Gerald | At:Wednesday, January 06, 2016

Na.Issack Gerald-Dar es Salaam
Jengo la Wizara ya mambo ya ndani makao makuu ya jeshi la Polisi,limenusulika kuteketea kwa moto na kusababisha kazi za jeshi hilo kusimama kwa muda,kutokana na wafanyakazi na viongozi wa jeshi hilo kutoka nje ya jengo kufuatia ya tahadhari ya moto kutolewa.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Mratibu Mwandamizi wa Polisi, Tanzania Advera Bulimba,amesema kuwa cheche za moto zilianza kuonekana Ghorofa ya nne,ambapo hata hivyo moto huo umedhibitiwa na kikosi jeshi la uokozi na zimamoto.

MPANDA

 AFIKISHWA MAHAKAMANI MPANDA KWA TUHUMA ZA UHARIBIFU WA MALI NA KUTELEKEZA FAMILIA.

Posted By:Issack Gerald | At:Thursday, January 07, 2016

Na.Issack Gerald-MPANDA
Mtu mmoja mkazi wa mtaa wa Kasimba manispaa ya Mpanda jana amefikishwa katika mahakama ya mwanzo mjini Mpanda akikabiliwa na shtaka la kuharibu mali na kutelekeza familia.

Hakimu wa mahakama ya mwanzo mjini Mpanda Bw. David Mbembela amemtaja mshtakiwa kuwa ni Juma Balison mwenye umri wa miaka 27, na kwamba alitenda kosa hilo tarehe 30 mwezi desemba mwaka 2015.
Amemtaja mlalamikaji katika kesi hiyo kuwa ni Magreth Joseph, na inadaiwa kuwa mshtakiwa aliharibu vyombo vya ndani ambavyo ni ndoo sita za plastiki na masufuria manne kwa kuviponda ponda kwa nyundo.
Inadaiwa pia kuwa mshtakiwa alikataa kutunza watoto aliozaa na mlalamikaji Bi. Magreth Joseph. Hata hivyo, mshtakiwa Juma Balison amekana shtaka hilo na kesi hiyo imeahirishwa na itatajwa tena tarehe 17 mwezi huu.
Posted By:Issack Gerald | At:Saturday, January 09, 2016

Na.Lutakilwa-Lutobeka-Katavi
MAAFISA 15 wa jeshi la polisi mkoani Katavi wametunukiwa vyeti maalum vya utendaji kazi katika maadhimisho ya siku ya polisi yaliyofanyika leo mjini Mpanda.

Akitunuku vyeti hivyo Kamishna msaidizi wa jeshi la polisi  kamanda Dhahiri Kidavashali amesema kutokana na kazi kubwa waliyofanya maafisa hao, kubaini matukio mbalimbali ya kiuharifu ni bora wakawapa vyeti hivyo kama motisha.
Mbali na kutunuku vyeti kamanda Kidavashali ametumia sherehe hizo kama sehemu ya kutathmini kazi zilizofanywa na jeshi kwa mwaka mzima wa 2015 ili kubaini mafanikio na mapungufu.
Wananchi waliohudhuria sherehe hizo wameelezea kufurahishwa na utendaji kazi wa jeshi la polisi kwa mwaka 2015, kwani askari wamekuwa marafiki wa wananchi.
Sherehe hizo za POLICE DAY ambazo zimefanyika katika viwanja vya polisi Wilayani Mpanda, zilihusisha michezo mbalimbali ikiwemo riadha na kucheza ngoma.
Hata hivyo Mkoani Katavi,kumekithiri matatizo ya watu kuuwawa mara kadhaa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Katavi ambapo watu hawa huuwawa na watu wasiojulikana lakini pia wengine kuuwawa na wanyama wakali kama simba.
Karibu watu 10 wamepoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha wengingi wao wakiwa ni wanaume.
Hata hivyo jeshi la polisi limesema kuwa,kupitia sherehe hizo,limewasihi wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi kuwabaini waharifu kabla ya  athari kutokea kwa binadamu.
Maadhimisho siku ya polisi  mkoani katavi yamefanyika yakiwa na kauli mbiu “UTII WA SHERIA BILA SHURUTI, KATAVI BILA UHARIFU INAWEZEKANA”.

 TUME YA ARDHI MPANDA YATOA TAARIFA YA UCHUNGUZI MIGOGORO YA ARDHI KWA BAADHI YA VIJIJI

Posted By:Issack Gerald | At:Saturday, January 09, 2016


Na.Issack Gerald-Mpanda
TUME ya uchunguzi wa migogoro ya ardhi imetoa taarifa baada ya kufanya uchunguzi katika vijiji vya Ikaka, Nkungu na Kapalamsenga wilayani Mpanda.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu maazimio yaliyofikiwa baada ya kupokea taarifa hiyo, Mkuu wa wilaya ya Mpanda Bw. Paza Mwamlima amesema miongoni mwa maazimio ni pamoja na halmashauri ya wilaya ya Mpanda kuwa na utaratibu wa kupima ardhi katika vijiji na iwe inatoa ushauri wa kitaalam kwenye kamati za ardhi za vijiji. 
Aidha, amemuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mpanda kupitia idara ya ardhi na maliasili afungue mashtaka, baada ya uongozi wa kijiji cha Kapalamsenga, uliokuwepo kukiuka sheria ya wanyamapori na kuuza eneo la Lyamgoloka kwa wananchi 52 mwaka 2013.
 Maeneo hayo ni miongoni mwa maeneo mengi yenye migogoro ya ardhi Mkoani Katavi ambapo mogogoro mingi wamekuwa wakilalamikiwa idara ya ardhi kwa kupima kiwanja kwa zaidi ya mtu mmoja.
Asante kwa kuendelea kuwa namii,endelea kuhabarika na P5 TANZANIA

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA FUPI YA ABDULRAHMAN KINANA ALIYEJUZULU UKATIBU MKUU CCM

FAHAMU HISTORIA YA JOKETI ALIYETUMBULIWA NA UVCCM

HISTORIA FUPI YA LAZARO NYALANDU ALIYEIBWAGA CCM NA KUHAMIA CHADEMA