KWA MWAKA 2017 WAPO WENGI WALIOTUMBULIWA NA RAIS MAGUFULI,HAWA NI BAADHI YA VIGOGO



Katika mwaka 2017, mambo mengi yametokea ambayo yametikisa nchi kuanzia kwenye nyanja ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na hata kiutamaduni. Imekuwepo mijadala mikubwa sana kuanzia kwenye ajali za barabarani, uchumi wa nchi, utawala, na mambo mengine yanayogusa maisha ya wananchi.
Rais Dkt John Magufuli
Wakati zikiwa zimesalia siku 6 mwaka 2017 kuisha, na mjadala sasa ukiwa ni sikukuu za Christmas na Mwaka Mpya na suala la Wachagga kurudi makwao, tutakuwa hatujautendea haki kama, japo kwa ufupi hatutakumbushana masuala yaliyotokea kwenye siasa kwa mwaka huu.
Mwaka huu, neno “Kutumbua” lilishika kasi sana. Hii ni kutokana na Rais Magufuli ambaye alisema amejipa kazi ya kutumbua majipu, kuwafuta kazi viongozi ambao kwake yeye aliona hawaendani na kasi yake au kutokana na sababu nyingine yoyote. Idadi ya waliotumbuliwa ni wengi, na katika mjadala wetu wa leo, tutaangazia vigogo 12 waliotumbuliwa tangu Januari 1, 2017.
1. Mhandisi Felchesmi Mramba.
Januari Mosi 2017, Rais Dk. John Magufuli, alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Felchesmi Mramba. Hatua hiyo ilikuja siku moja baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), kutangaza kuridhia ombi la TANESCO la kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 8.5 kutoka 18 waliyoomba.
Kutokana na kutenguliwa kwa Mramba, Rais Dk. Magufuli alimteua Dk. Tito Mwinuka kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuwa Kaimu Mkurugenzi wa TANESCO.
2. Nape Moses Nnauye
Machi 23 mwaka huu, Rais Dkt John Pombe Magufuli alifanya mabadiliko ya baraza la mawaziri ambapo aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Moses Nnauye aling’olewa na nafasi yake kuchukuliwa na Dkt. Harrison Mwakyembe.
Kutumbuliwa kwa Nape kulikuja siku moja baada ya kupokea ripoti kutoka kwa kamati aliyokuwa ameiunda kwa ajili ya kuchunguza sakata la kuvamiwa kwa Ofisi za Clouds Media Group.
3. Prof. Sospeter Muhongo
Miezi 7 iliyopita (24 Mei, 2017),  Rais Dkt. John Pombe Magufuli alitengua uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini (sasa Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini), Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo. Licha ya kuwa barua kutoka Ikulu haikueleza sababu ya utenguzi wake, lakini wakati akipokea ripoti ya makinikia, Rais Magufuli alimtaka Waziri Muhongo ajiuzulu kwa kushindwa kusimamia suala la mchanga wa dhahabu unaosafirishwa kwenye makontena.
Lakini Waziri Muhongo nae aliandika barua kwenda kwa Rais Magufuli akieleza kwamba amejiuzulu nafasi yake ya uwaziri kufuatia mapendekezo yaliyotolewa na kamati iliyofanya uchunguzi wa makinikia.
4. George Simbachawene 
Septemba 7, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene aliandika barua ya kujiuzulu wadhifa huo baada ya kutajwa katika ripoti za uchunguzi wa biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi iliyoonyesha namna serikali lilivyopoteza matrilioni ya fedha kutokana na sababu mbalimbali.
Kujiuzulu kwake kulikuja muda mfupi tangu Rais Magufuli kuwataka viongozi wote aliowateua na wametajwa katika ripoti hiyo wakae pembeni ili kupisha uchunguzi ambao utakuwa huru na wa haki.
5. Mhandisi Edwin Amandus Ngonyani
Kama ilivyokuwa kwa Simbachawene aliyejiuzulu baada ya kutakiwa kupisha uchunguzi, aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani naye alijiuzulu Septemba 7 baada ya kutuhumiwa kutotekeleza majukumu yake kikamilifu alipokuwa akifanya kazi katika Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) lenye dhamana ya kusimamia madini.
6. Prof. Justin Ntalikwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli alitengua uteuzi wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Prof. Justin Ntalikwa kuanzia tarehe 26 Machi 2017.
Profesa Ntalikwa alifutwa kazi na Rais Magufuli siku chache baada ya kufanya ziara ya kushtukiza bandarini.
Mei 2017, Rais Magufuli alisema kwamba, alimfuta kazi kiongozi huyo kutokana na kueleza Kamati ya Bunge kiasi ambacho kilikuwa kipo kwenye makontena ya dhahabu ambacho hakikuwa sawa.
7.  Prof. Jumanne Abdallah Maghembe
07 Oktoba, 2017 alifanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri kwa kuongeza idadi ya Wizara, kuteua Mawaziri na Naibu Mawaziri wapya na kuwahamisha Wizara baadhi ya Mawaziri na Naibu Mawaziri.
Aliyekuwa Waziri wa Mali Asili na Utalii, Prof. Maghembe aliachwa nje ya uteuzi au mabadiliko hayo ambapo nafasi yake ilichukuliwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Andrea Kigwangalla.
8. Mhandisi Ramol Makani
Katika mabadiliko ya baraza la mawaziri yaliyofanywa na Rais Dkt Magufu Oktoba 7, 2017, Mhandisi Makani aliachwa nje na nafasi yake kuchukuliwa na Josephat Ngailonga Hasunga.
Mhandisi Ramol Makani alikuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii. Hakuna maelezo yoyote yaliyotolewa kuhusu kutumbuliwa kwa Makani.
9. Anastasia Wambura
Wambura alikuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo. Kiongozi huyo aliachwa nje ya mabadiliko ya baraza la mawaziri na nafasi yake ikachukuliwa na  Juliana Daniel Shonza.
10. Dkt. Charles Mlingwa
Mlingwa alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara ambapo Oktoba 26 mwaka huu Rais Magufuli alifanya mabadiliko na kumuondoa, kisha nafasi yake kuchukuliwa na Adam Kigoma Malima.
11. Jordan Rugimbana
Katika mabadiliko ya Oktoba 26, Rais Dkt Magufuli alimuacha nje, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Joardan Rugimbana na kumteua Bi Christine Solomon Mndeme kuchukua nafasi hiyo.
Licha ya kuwa Mndeme alipangiwa Mkoa wa Dodoma, Rais Magufuli alimtaka akaanzie kazi Mkoa wa Shinyanga, na hivyo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Tellack akahamishiwa Dodoma.
Kabla ya uteuzi huo, Bi. Mndeme alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini.
12. Halima Dendego
Dendego alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara. Katika mabadiliko yaliyofanyika, nafasi yake ilichukuliwa na Gelasius Gasper Byakanwa.
Kabla ya uteuzi huo, Byakanwa alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai.
Mbali na ambao uteuzi wao ulitenguliwa au kuachwa nje ya mabadiliko yaliyofanyika, wengine wengi walitumbuliwa lakini Rais alitangaza kuwa watapangiwa kazi nyingine. Baadhi ya wanaoangukia katika kundi hili ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba Erasto Mfugale na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Vijijini Mwantum Dau.
Rais alitengua uteuzi wa wakurugenzi hao baada ya kushindwa kujibu maswali yake mbele ya wananchi.
Habari zaidi ni P5TANZANIA LIMITED

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA FUPI YA ABDULRAHMAN KINANA ALIYEJUZULU UKATIBU MKUU CCM

FAHAMU HISTORIA YA JOKETI ALIYETUMBULIWA NA UVCCM

HISTORIA FUPI YA LAZARO NYALANDU ALIYEIBWAGA CCM NA KUHAMIA CHADEMA