ZIARA YA WAZIRI MKUU WILAYANI MLELE :FANYENI UKAGUZI KUBAINI WALIOKULA FEDHA ZA USHIRIKA NA KUWACHUKULIA HATUA


Na.Issack Gerald Bathromeo-Inyonga Mlele
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemtaka Mkuu wa Mkoa Katavi, Meja Jenerali (Mstaafu) Raphael Muhuga kupeleka wakaguzi wilayani Mlele na kubaini watu waliokula fedha za chama cha ushirika cha Ukonongo na kuwachukulia hatua.
Waziri Mkuu akiwa ziarani Inyonga wilayani Mlele baada ya kutawazwa kuwa Chifu wa Wakonongo(PICHA NA.Issack Gerald)
                                             

“Watakaobainika watiwe hatiani. Licha ya bodi ya ushirika huo kuvunjwa, hatuwezi kuacha suala hili limalizike kwa kuvunja bodi kwa sababu walioingia wanaweza kuiba kwa mategemeo ya kuvunjwa bodi,“ amesema.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kiwanja cha Inyonga wilayani Mlele.
Amesema kila mtumishi afanye kazi na awajibike kwa uadilifu na uaminifu mkubwa kwa mujibu wa taaluma yake ili kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo kwani hilo ndilo lengo la kuajiriwa kwake.
“Haiwezekani hapa kuna Ofisa Ushirika halafu Waziri Mkuu analetewa mabango ya kumtaka atatue tatizo la chama cha Ushirika. Hali hii inaonyesha hapa hakuna kazi inayofanyika,“ amesema.
Waziri Mkuu amesema wanahitaji watumishi watakaosikiliza maelekezo yanayotolewa na Serikali na kuyafanyia kazi kwa sababu malengo ya Mhe. Rais Dk. John Magufuli ni kuona nchi hii inabadilika hivyo wasioweza ni vema wakaandika barua za kuacha kazi.
“Msikubali kuhamasishwa kufanya mambo yatakayowaletea madhara. Fanyeni kazi ili tupate maendeleo. Hatuwezi kufananishwa na nchi ndogo ndogo, wenzenu wanafanya kazi nasi tupunguze maneno tufanye kazi,“ amesema.
Wakati huo huo Waziri Mkuu amesema Serikali imedhamilia kumaliza changamoto ya upatikanaji wa umeme nchini ambapo imetenga zaidi ya sh. trilioni moja kwa ajili ya kumalizia kazi ya usambazaji umeme nchi nzima ikiwemo wilaya ya Mlele.
Amesema watapeleka jenereta kubwa mbili zitakazofungwa katika kijiji cha Utende ambazo zitasambaza na kuwasha umeme katika kata ya Inyonga na maeneo mengine.
“Mwezi Novemba mwaka huu umeme utakuwa umewaka wilayani Mlele. Mkakati ni kuunganisha mkoa wa Katavi na gridi ya Taifa kutoka Tabora, kupita Sikonge hadi Inyonga,“ amesema.  
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji na mbunge wa jimbo la Katavi, Mhandisi Isack Kamwelwe amemuomba Waziri Mkuu kuwasaidia kupandishwa hadhi kwa kituo cha afya cha Inyonga na kuwa Hospitali ya wilaya kwa sababu wilaya yao haina hospitali.
Pia ameomba wilaya hiyo ipatiwe umeme wa Tanesco ili kupunguza gharama kubwa za kununua umeme kutoka kwa mfanyabiashara ambaye amefunga jenereta na anawauzia unit moja sh. 1000 wakati Tanesco wanauza sh. 100 kwa unit moja.
Awali Mkuu wa wilaya ya Mlele, Rachel Kassanda alisema wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa nyumba za watumishi hali inayosababisha mkuu wa wilaya na Katibu tawala wa wilaya kuishi kwenye nyumba za kupanga.
 Habarika zaidi na P5TANZANIA.BLOGSPOT.COM

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA FUPI YA ABDULRAHMAN KINANA ALIYEJUZULU UKATIBU MKUU CCM

FAHAMU HISTORIA YA JOKETI ALIYETUMBULIWA NA UVCCM

HISTORIA FUPI YA LAZARO NYALANDU ALIYEIBWAGA CCM NA KUHAMIA CHADEMA