MATUKIO YA WIKI MKOANI KATAVI NA TANZANIA KWA UJUMLA KUANZIA JANUARI 18-23,2016.



Tuesday, 19 January 2016
Posted By:Issack Gerald | At:Tuesday, January 19, 2016

Na.Issack Gerald-MPANDA
VIJANA watatu wakazi wa Mpanda mjini jana wamefikishwa katika mahakama ya Mwanzo mjini Mpanda, wakikabiliwa na shtaka la shambulio la kudhuru mwili.


Akisoma shtaka hilo Mbele ya hakimu David Mbembela, koplo Mtei kutoka jeshi la polisi Mpanda amewataja waliotenda kosa hilo kuwa ni Ramadhan Hamis mkazi wa Nsemulwa, Maneno Shaban mkazi wa Mikocheni na Mohamed Mussa ambapo wote kwa pamoja mnamo tarehe 14 Mwezi huu katika maeneo ya majengo mjini Mpanda, walimshambulia Abdallah Salum mkazi wa Misunkumilo na kumsababishia maumivu makali.
Koplo Mtei ameiambia mahakama kuwa mlalamikaji hakufika mahakamani kutokana na kulazwa katika hospitali ya wilaya ya Mpanda anakoendelea na matibabu kutokana na kipigo alichopigwa na washtakiwa hao.
Aidha, ameiomba mahakama hiyo isiruhusu dhamana kwa washtakiwa hadi pale taarifa kuhusu hali ya muhanga zitakapotolewa.
Washtakiwa wote wamekana shtaka na hakimu Mbembela amesema kutokana na ombi kutoka kwa askari ambaye ni afisa wa serikali na amekula kiapo cha kusema ukweli, hivyo mahakama imeridhia hoja iliyotolewa.
Kesi hiyo itatajwa tena tarehe 22 mwezi huu na washtakiwa wamerudishwa rumande.

Tuesday, 19 January 2016
Posted By:Issack Gerald | At:Tuesday, January 19, 2016

Na.Mwandishi wetu-DAR ES SALAAM
MKURUGENZI Mtendaji Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi Suleiman Lukanga,amesimamishwa kazi kwa tuhuma za kuridhia na kutekeleza uamuzi ulioisababishia serikali hasara na upotevu wa fedha.
 Taarifa ya kusimamishwa kazi sambamba na Mkurugenzi Mtendaji Manispaa ya Kigoma Bw.Boniface Nyambele imetangazwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa George Simbachawene katika mkutano na waandishi wa habari baada ya tangazo kutolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Rais Tamisemi Rebecca Kwandu.
Kwa upande wake Mkrugenzi Mtendaji Manispaa ya Mpanda Bw.Suleiman Lukanga anayekabiliwa na tuhuma za ununuzi hewa wa gari la kusomba taka kwa Sh milioni 92.75 na ubadhirifu wa fedha za ujenzi wa skimu ya umwagiliaji ya Kakese, Sh milioni 294.
Naye Mkurugenzi Boniface Nyambele wa manispaa ya Kigoma anayekabiliwa na tuhuma za uuzaji wa nyumba za halmashauri bila kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo, zinazomtaka awe na kibali cha waziri mwenye dhamana.  
Nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji Manispaa ya Mpanda itakaimiwa na Lauteri Kanoni ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi huku nafasi ya Mkurugenzi Manispaa ya Kigoma ikikaimiwa na Sultan Ndilowa ambaye ni Mkuu wa Idara ya Maji Manispaa ya Kigoma
Aidha,Waziri Simbachawene amewataka wakurugenzi watendaji wa mamlaka za serikali za mitaa nchini kuwa makini katika kutekeleza majukumu yao kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Amesema serikali haitasita kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wote,ambao watakiuka matakwa ya sheria, kanuni na taratibu na kutoweka mbele maslahi ya umma.

Tuesday, 19 January 2016
Posted By:Issack Gerald | At:Tuesday, January 19, 2016

Na.Boniface Mpagape-Mpanda
MTU mmoja mmoja mkazi wa Kasokola wilayani Mpanda Bw. Godfrey Kipyela, jana amefikishwa katika mahakama ya Mwanzo mjini Mpanda akikabiliwa na shtaka la kudhuru mwili.

Akisoma shtaka hilo, KIoplo Mtei wa jeshi la polisi Mpanda amesema mshtakiwa alitenda kosa hilo tarehe 13 desemba mwaka 2015, saa moja usiku maeneo ya Kasokola ambapo alimshambulia Bi. Maria January kwa kumpiga ngumi maeneo mbali mbali ya mwili na kumsababishia maumivu makali.
Hakimu wa mahakama ya Mwanzo mjini Mpanda Bw. David Mbembela baada ya kusikiliza maelezo ya mlalamikaji pamoja na ushahidi uliotolewa na mtoto mdogo mwenye umria wa miaka sita, amesema mlalamikaji anapaswa kuwasilisha mahakamani hati ya matibabu yenye muhuri kutoka hospitali alikopatiwa matibabu.
Kesi hiyo itasikilizwa tarehe 21 mwezi huu, na dhamana dhidi ya mshtakiwa inaendelea.

Posted By:Issack Gerald | At:Monday, January 18, 2016

Na.Issack Gerald-MPANDA
HALMASHAURI zote zilizomo ndani ya mkoa wa katavi zimetakiwa kufanya jitihada za kutatua  changamoto za miundombinu ya elimu ili kuhakikisha wanafunzi wote wanasoma vizuri.

Hayo yamesemwa na Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Katavi Bw.Said Mwapongo  wakati akizungumza na P5 TANZANIA MEDIA ofisini kwake kwa njia ya simu.
 Amesema tayari ngazi ya mkoa imekutana na ngazi za halmashauri lengo likiwa ni kuangalia utatuzi wa changamoto  hizo kutokana na ongezeko la wanafunzi katika sule mbalimbali.
Aidha  Bw mwapongo ameitaka jamii kuwapeleka watoto shule bila kisigizio  chochote cha kutokuwa na sare ya shule  na kuwa kwa mzazi au mlezi atakosa sare ya shule ampeleke  atapokelewa huku jitihada za kutafuta sare zikiendelea kufanyika.
Mkoa wa Katavi unaundwa na Halmshauri 5 ambazo ni Halmshauri ya Wilaya ya Mpanda,Halmshauri ya Manispaa ya Mpanda,Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo,Halmshauri ya Wilaya ya Mlele na Halmshauri ya Wilaya ya Mpimbwe

 

Tuesday, 19 January 2016

Posted By:Issack Gerald | At:Tuesday, January 19, 2016

Na.Issack Gerald-Katavi
Mkoa wa Katavi umepokea Zaidi ya Shilingi Milioni 80 kwa ajili ya kugharimia mpango wa serikali wa elimu bure kwa wanafunzi kuanzia Chekechea hadi  kidato cha nne.

Kaimu Afisa elimu Sekondari  Mwalimu Said Mwapongo amesema kuwa Mkoa wa Katavi umepokea zaidi ya milioni 80 na tayari zimesambazwa katika shule kwa ajili ya matumizi yaliyokusudiwa.
Afisa elimu Mwapongo,pamoja na kutoa wito kwa jamii,anatolea ufafanuzi wa michango hiyo ambayo imefutwa pamoja na ile inayopaswa kuchangwa.
Kuhusu wanafunzi waishio shule za bweni ambazo ni za Kata,Mwapongo amesema kuwa ziko kwenye mpango wa serikali wa kuziondolea michango inayotoka kwa wazazi kutokana na mpango wa wanafunzi waishio bweni kuwa katika mipango ya wazazi,walimu na bodi za shule.
Ufafanuzi huo wa Kaimu Afisa Elimu umekuja kufuatia malalamiko ya baadhi ya wazazi wakihoji kulikoni wanafunzi waendelee kuchangishwa michango ya vitu mbalimbali kama vyakula,pesa ya mlinzi na mpishi.
Mmoja wa wakazi kutoka kijiji cha Kabulonge Kata ya Litapunga Wilayani Nsimbo ambaye hakutaka jina lake litajweanasema yeye amekuwa na maswali mengi baada ya mtoto wake aliyeko katika Shule ya sekondari machimboni kuanmbiwa atoe michango wakati mtoto wake akipelekwa kuanza kidato cha kwanza.
Hata hivyo baadhi ya wazazi,walezi na jamii kwa ujumla imeonekana kutoelewa vizuri mchanganuo wa michango iliyofutwa na ilea ambayo jamii inapaswa kuendelea kuchagia.
Kwa Upande wake Afsisa elimu Sekondari Manispaa ya Mpanda Bi.Enelia Lutungulu amesema kuwa kesho wanatarajia kukutana na bodi za elimu kwa shule zilizo katika kata za Magamba,Kasokola na Shanwe kwa ajili kuweka sawa mazingira ya utekelezaji wa sera ya elimu bure.
Katika fedha hiyo Wilaya ya Mlele imepata zaidi ya Shilingi Milioni 32 kwa ajili ya elimu za msingi na  sekondari na huku hesabu ya kujua kiasi kilichopokewa kwa upande wa Wilaya ya Mpanda na Nsimbo kikiendelea kuchanganuliwa vizuri.
Idara ya elimu sekondari Mkoa wa Katavi kwa Ujumla imesema kuwa,wanaendelea kuweka mikakati ili kuhakikisha wanashika nafasi ya juu katika mithani ya taifa kwa ngazi ya shule za sekondari kama ilivyo kwa shule za Msingi ambapo Mkoa wa Katavi umeshika nafasi ya kwanza kwa mwaka 2015 huku Manispaa ya Mpanda ikishika nafasi ya kwanza kitaifa kwa miaka 2 mfululizo yaani mwaka 2014 na 2015.
Kwa mjibu wa barua ya tarehe 23 Novemba mwaka 2015 iliyoandikwa na Wizara ya Elimu na mafunzo ya ufundi na kusambazwa katika shule zote hususani za Sekondari Tanzania bara,inamtaka kila Mkuu wa shule kumpatia mwanafunzi fomu iliyotolewa na Wizara na siyo ile iliyokuwa ikiandaliwa na bodi au kamati za shule na lengo kuu likiwa kuondoa migogoro ya michango ya shule moja kutofautiana na shule nyingine Wakati huo huo barua ya Novemba 27 mwaka 2015 ikiainisha wajibu wa mzazi,mlezi,mwalimu,bodi au kamati za shule na jamii kwa ujumla.


Tuesday, 19 January 2016
Posted By:Issack Gerald | At:Tuesday, January 19, 2016

Issack Gerald-DAR ES SALAAM
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema,Serikali imepanga kufungua viwanda vya kusindika ngozi kwenye mikoa ya Shinyanga, Geita na Dar es Salaam ili kutoa soko kwa ngozi za wanyama wanaochinjwa kwenye machinjio ya mikoa hiyo.
 Majaliwa ametoa kauli hiyo jana jioni wakati akizungumza na baadhi ya Watanzania waishio Botswana kwenye kikao kilichofanyika kwenye kituo cha mikutano ya kimataifa (GICC), jijini Gaborone, Botswana.
Waziri Mkuu amekuwa nchini Botswana kwa ziara ya siku moja kumwakilisha Rais Dk. John Pombe Magufuli kwenye mkutano wa SADC Double Troika yaani kikao maalum cha Wakuu wa Nchi na Serikali na Wakuu wa Nchi wanaounda Chombo cha Ushirikiano wa Siasa,Ulinzi na Usalama.
Amesema Serikali imeamua kuongeza viwanda nchini, kama njia mojawapo ya kukuza uchumi,kuacha kuuza mali ghafi lakini pia ni fursa ya kuongeza ajira kwa Watanzania.
Wakati huo huo akijibu hoja zilizoainishwa kwenye risala yao, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali bado ina nia ya kuhamia Dodoma na kwamba itaendelea kutenga fedha zaidi ili wizara nyingi zijenge ofisi zao Dodoma.
Aidha Waziri Mkuu Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwataka Watanzania waishio ughaibuni kutafuta fedha za mitaji ambapo fedha hizo zinaweza kuwa zao au kupitia kwa marafiki zao ili waweze kuwekeza nyumbani Tanzania.
Awali akisoma risala yao kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa Chama cha Watanzania waishio nchini Botswana Bw. Neiman Kissasi amesema chama hicho kilianzishwa mwaka 1992 kikiwa na lengo la kuwaunganisha Watanzania waishio Botswana pamoja kujenga undugu wao na kusaidiana.
Katika risala yao, wameshauri wafugaji wa Tanzania waelimishwe na kuwezeshwa kufuga kisasa na kuondokana na ufugaji wa kurandaranda.
Vilevile, wameiomba Serikali ifungue fursa za kiuchumi kwenye mikoa mingine ya Tanga, Lindi, Mtwara, Pwani, Kigoma, Mbeya, Mwanza na Arusha badala ya kuziacha ziwe Dar es Salaam peke yake.
Waziri Mkuu amerejea jijini Dar es Salaam jana usiku.
 Chanzo cha habari : Ofisi ya Waziri Mkuu

 

Tuesday, 19 January 2016

Posted By:Issack Gerald | At:Tuesday, January 19, 2016

Na.Issack Gerald-Mpanda
WATU wawili wakazi wa kata ya Mpanda ndogo wilayani Mpanda mkoani Katavi, jana wamefikishwa katika mahakama ya mwanzo mjini Mpanda wakikabiliwa na shtaka la kujipatia fedha shilingi milioni tatu na laki nne kwa njia ya udanganyifu.

Mlalamikaji Bw. Lyango Joseph Mkazi wa Katumba ameiambia mahakama hiyo kuwa washtakiwa Mustafa Mfaume na Mohamed Salum walitenda kosa hilo la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kati ya mwaka 2014 na 2015.
Mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Bw. David Mbembela, mlalamikaji Bw. Lyango Joseph amesema kuwa, mshtakiwa namba moja ambaye ni Bw. Mustaph Mfaume mnamo tarehe 20 mwezi desemba mwaka 2014 alienda nyumbani kwa Lyango Joseph na kuomba shilingi laki nne kwa lengo la lengo la kufanyia shughuli za kilimo cha tumbaku katika maeneo ya Kapemba kwa ahadi kuwa akiuza tumbaku atarudisha fedha alizokopa bila riba.
Mlalamikaji Bw. Lyango Joseph ameiambia mahakama hiyo kuwa mnamo tarehe 16 mwezi januari mwaka 2015 mshtakiwa namba moja aliongeza tena ombi la kukopeshwa shilingi laki nne kwa lengo lile lile. Amesema mnamo tarehe 05 mwezi februari mwaka 2015 aliomba akopeshwe tena shilingi laki tatu kwa ahadi ya kurejesha atakapouza tumbaku.
Mlalamikaji ameendelea kuiiambia mahakama ya mwanzo mjini Mpanda kuwa, mnamo tarehe 23 mwezi April mwaka 2015 mshtakiwa Mustafa Mfaume, aliomba tna akopeshwe shilingi laki sita lwa lengo lile lile la kuendeleza kilimo cha zao la tumbaku.
Bw. Lyango amesema mwezi April mwishoni tarehe ambayo mlalamikaji haikumbuki, mshtakiwa namba moja Bw. Mustafa Mfaume alikwenda tena nyumbani kwa mlalamikaji Kanoge ambaye ni rafiki yake wa muda mrefu na kuomba tena shilingi laki mbili ili aendeshee kilimo cha tumbaku na alikopeshwa fedha hizo na mwishoni mwa mwezi Mei tarehe ambayo mlalamikaji haikumbuki mshtakiwa namba moja Bw. Mustafa Mfaume alimpeleka mshtakiwa namba mbili Bw. Mohamed Salum  na kuomba amdhamini apewe shilingi laki mbili lakini mlalamikaji Bw. Lyango Joseph alikataa kwa kuwa hamfahamu na ndipo Mshtakiwa Mustafa Mfaume akadai anamdhamini, na kutokana na ukaribu na urafiki wao alikubali na kumkopesha kiasi hicho cha fedha.
Mlalamikaji amesema kwa mara ya mwisho mshtakiwa Mustafa Mfaume alikwenda kwake tarehe 12 mwezi Mei na aliomba fedha shilingi milioni moja na laki mbili ili zitumike kwenye shamba lake la tumbaku na kuahidi atakapouza na kupata malipo atarejesha fedha hizo bila riba.
Mlalamikaji Bw. Lyango Joseph amesema mshtakiwa namba moja Bw. Mustafa mfaume alikuwa amejipatia jumla ya shilingi milioni tatu na laki mbili na mshtakiwa namba mbili Bw. Mohamed Salum alijipatia shilingi laki mbili na kufanya jumla kuu ya fedha walizojipatia kwa udanganyifu kuwa shilingi milioni tatu na laki nne.
Awali washtakiwa wote wawili walitiwa hatiani na mahakama hiyo na kuhukumiwa kifungo cha miezi sita jela kutokana na kukiri kosa la kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu toka kwa Bw. Lyango Joseph na hukumu hiyo iliwataka watakapomaliza kutumikia adhabu ya kifungo jela, warejeshe fedha kwa mlalamikaji lakini baada ya kutoka jela hawakutekeleza amri ya  mahakama ya kumlipa mlalamikaji.
Mlalamikaji katika shauri hilo Bw. Lyango Joseph ametoa pia vielelezo vya hati 6 walizoandikiana pamoja na nakala ya uamuzi wa mahakama uliowatia hatiani washtakiwa. Washtakiwa wamekubali vielelezo vyote vilivyotolewa mbele ya mahakama ya mwanzo mjini Mpanda.
Hakimu wa mahakama hiyo Bw. David Mbembela amesema kwa kuwa washtakiwa hawajapinga nakala ya uamuzi wa mahakama iliyowatia hatiani, hata hivyo hati 6 zilizotolewa mahakamani kama kielelezo mahakama imezikataa mpaka zithibitishwe na kamishna wa viapo ili ziweze kutambulika kisheria kuwa ni hati halali.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 03 mwezi Februari mwaka huu, kungoja ushahidi kutoka kwa washauri wa mahakama waliosikiliza kesi hiyo tangu mwanzo ambapo hata hivyo hamimu Mbembela amesema dhamana kwa washtakiwa zinaendelea.

Wednesday, 20 January 2016
Posted By:Issack Gerald | At:Wednesday, January 20, 2016

Na.Issack Gerald-Katavi

Watu wawili waliofahamika kwa majina ya Kupiwa Julius (28) na Lemmy Madirisha wote wakazi wa Mkazi wa Ilebura wamepigwa na radi na kufariki dunia papo hapo.

Kamanda wa Polisi Mkoani Katavi Dhairi Kidavashari amesema kuwa tukio hilo limetokea jana majira ya saa nane na nusu mchana katika kijiji cha Ilebura Tarafa ya Kabungu Wilaya ya Mpanda.
Amesema kuwa,katika tukio hilo,watu watatu waliojeruhiwa wametajwa kuwa ni Tatu Gerald (28),Stela John (38) na Philbert Paschal wote wakazi wa kijiji cha Ilebura.
Aidha kamanda Kidavashari amesema,kabla ya tukio marehemu na majeruhi kwa pamoja walikuwa shambani wakilima ambapo wakati wakiendelea kulima mvua ilianza kunyesha ambapo wote waliamua kwenda chini ya mti kujikinga na mvua na ndipo radi ilipopiga na kupelekea madhara hayo.
Ameongeza kuwa baada ya tukio hilo majeruhi wote wamepelekwa katika hospitali ya Wilaya ya Mpanda na wanaendelea na matibabu huku miili ya marehemu ikiwa imekabidhiwa kwa ndugu zao kwa ajili ya mazishi.
Hata hivyo,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi anawatahadharisha wananchi wote kuwa makini katika kipindi hiki cha masika pindi mvua zinaponyesha kwa kujihifadhi maeneo salama ilikuepukana na madhara kama haya ambayo huadhiri ustawi wa afya na uhai wa watu.

Wednesday, 20 January 2016
Posted By:Issack Gerald | At:Wednesday, January 20, 2016

Na.Agness Mnubi-Nsimbo.
WADAU wa Elimu katika halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo Mkoani Katavi wametakiwa kuelimisha wazazi na walezi juu ya Mfumo wa elimu bure.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mlele Kanali Mstaafu Issa Suleiman Njiku katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika jana katika Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, mara baada ya madiwani wa halmashauri hiyo kuhoji juu ya Mfumo wa elimu bure.
Amefafanua kuwa ni wajibu wa Mkurugenzi kuitisha kikao cha wadau wa elimu ili kuwaelimisha wazazi na walezi  juu ya Mfumo wa elimu bure.
Aidha amesema taarifa juu ya  elimu bure zibandikwe kwenye mbao za matangazo, ili kurahisisha kusambaza elimu hiyo na kuwataka madiwani wa halmashauri ya Nsimbo kutoa taarifa za walimu wanaotoza ada na mahitaji mengine ya wanafunzi ambayo yanagharimiwa na serikali.
Wakati huo huo,idara ya Maliasili na Misitu katika halmashauri ya wilaya ya Nsimbo imeagizwa kutatua mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa kata ya Urwila na kata ya Katumba, kuhusu kilimo katika eneo la Nzaga ambalo  ni chanzo cha mto.
Kanali Njiku ameongeza kuwa,wananchi wa Vijiji hivyo wanagombania kulima katika mpaka wa eneo la mto, kinyume cha sheria na kufafanua kuwa sheria inaelekeza shughuli za kibinadamu kuanza umbali wa mita 60 kutoka chanzo cha maji.
Kufuati hali hiyo, amewataka wananchi wanaoishi katika misitu na hifadhi ya serikali, kuhama na kuacha tabia ya kukata misitu na kuendesha shughuli yoyote katika hifadhi za serikali.


Wednesday, 20 January 2016
Posted By:Issack Gerald | At:Wednesday, January 20, 2016

Na.Issack Gerald-Sumbawanga
POLISI wilayani Sumbawanga Mkoani Rukwa inamshikilia mkazi wa kijiji cha Ulinji, Manispaa ya Sumbawanga mwenye umri wa miaka 28 kwa tuhuma za kumpa ujauzito dada yake mwenye umri wa miaka 14 anayesoma darasa la saba.

Inadaiwa kuwa mtuhumiwa ambaye amemtaliki mkewe, alirejea kuishi nyumbani kwa wazazi wake kijijini Ulinji miaka miwili iliyopita kabla ya kumpatia ujauzito mtoto huyo wa baba yake mkubwa.
Polisi imethibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kwamba alikamatwa na Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ulinji, Manispaa ya Sumbawanga, Linus Mbutu.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ulinji, amesema mtuhumiwa amekamatwa juzi na askari wa Mgambo wa kijiji hicho akiwa amejificha kwa saa tatu porini akikwepa kukamatwa.
Katika hatua nyingine,idara ya elimu wilayani Kalambo  mkoani Rukwa jana imefanya kikao cha kujadili upungufu wa madawati uliopo wilayani humo.
Akizungumza na  P5 TANZANIA MEDIA sambamba na mpanda radio kwa njia ya simu afisa elimu vifaa na takwimu wa halmashauri ya wilaya ya Kalambo  Bi. Toba Mwihanga  ameziomba taasisi mbalimbali kutoa msaada ili kutatua changamoto hiyo.
Bi. Mwihanga amesema mwaka 2014 walipokea madawati 100 ambayo hayakukidhi mahitaji ya wanafunzi.
Aidha ameitaka jamii kuendelea kushiriki katika ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu na vyoo,huku akiwataka watendaji wa kata kuhamasisha jamii juu ya elimu bure , na kuiomba serikali kuongeza walimu katika mkoa huo. 


Wednesday, 20 January 2016
Posted By:Issack Gerald | At:Wednesday, January 20, 2016

Na.Boniface Mpagape-Mpanda
MKUU wa Mkoa wa katavi Dk. Ibrahim Msengi amewataka wakazi wa mkoa huo,kuchukua tahadhari kutokana na uwezekano wa kuwepo kwa mafuriko kama ilivyotabiriwa na wataalam wa hali ya hewa.

Mkuu wa mkoa wa Katavi ametoa tahadhari hiyo wakati akizungumza na Mpanda radio ofisini kwake sambamba na P5 TANZANIA MEDIA.
Amesema wakazi wa mkoa wa Katavi wamekuwa wakijenga katika maeneo ambayo hayaruhusiwi kwa makazi na kuwataka wawe katika maeneo yasiyo hatarishi. 
Amewaagiza wakurugenzi, na wakuu wa wilaya zote mkoani Katavi   kwa kushirikiana na kamati zao za maafa kujiandaa kikamilifu kwa kutoa tahadhari kwa wananchi ili kukabiliana na maafa yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua za El-Nino.


Thursday, 21 January 2016
Posted By:Issack Gerald | At:Thursday, January 21, 2016

Na.Issack Gerald-Mpanda
Wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika Shule ya Msingi Sambwe iliyopo mtaa wa Kampuni  Kata ya Misunkumilo Manispaa ya Mpanda,wameiomba serikali kuwasaidia kumalizia ujenzi wa madarasa katika shule hiyo ili wanafunzi hao waondokane na adhaa ya kunyeshewa na mvua  inayoambatana na radi wakiwa chini ya miembe.
 Hayo yamebainishwa na wazazi hao wakati wakizungumza na P5 TANZANIA MEDIA Sambamba na Mpanda Radio Katika mtaa huo,kuhusu namna wazazi wanavyojitolea katika ujenzi wa madarasa shuleni hapo.
Aidha wamesema kuwa,baadhi ya watoto wamekuwa wakiugua magonjwa kama homa,maralia na mengineyo huku daftari zikilowana kutokana na wanafunzi kukosa mahala pa kujisitiri.
Baadhi ya Wazazi waliozungumza ni pamoja na Mussa Daudi,Huruma Washega na Peter Paul Masesela wote wakazi wa Mtaa wa Kmpuni ambao pia wamesema kutokana na kuishiwa pesa hawana namna zaidi ya kuitegemea serikali kutokana na uwezo wao kufikia kikomo.
Hata hivyo wameeleza kusikitishwa na serikali kuwafukuza wachimbaji wadogowadogo katika mgodi wa Kampuni ambapo wachimbaji hao kila mara wamekuwa sehemu mojawapo ya chanzo cha Mapato katika kuendesha maendeleo ya shule.
Katika hatua nyingine,wameiomba serikali kumuweka  katika mfumo wa malipo mwalimu Alex Sangu ambaye amekuwa akifundisha katika shule ya Sambwe kwa muda mrefu ikizingatiwa kuwa hawana tena uwezo wa kulipa kutokana na kipato chao kidogo kinachotosheleza kuendesha familia zao.
Hata hivyo Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Bw.Charles Kassian ,hakuwa tayari kuzungumza na P5 TANZANIA MEDIA sambamba na Mpanda Radio kuhusu maendeleo na hali ya shule zaidi ya kusema kuwa labda atazungumza baada ya mwezi mmoja kuanzia sasa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Kampuni Bw.James Simon amekiri wanafunzi kusomea chini ya miembe tangu shule zifunguliwe  Januari 11 mwaka huu ukizingatia kuwa ni msimu wa mvua za masika zinazoambatana na radi.
Hata hivyo Bw.Simoni,amewataka wananchi kuendelea kuwa wavumilivu wakati masuala mbalimbali yakiwemo kumlipa mwalimu wakati yakifanyiwa kazi ambapo wakati huo huo amesema kuwa siku ya jumatano ya wiki ijayo wanatarajia kuitisha mkutano wa hadhara kujadili maendeleo ya shule.
Shule ya Msingi Sambwe,ina walimu 2 walioajiriwa na seriklai huku mmoja akiwa ni wa kujitolea ambo shule hiyo iliyosajiriwa mwaka huu ina wanafunzi wapatao 150 kuanzia darasa la kwanza hadi la nne.
Hata hivyo Meya wa Manispaa ya Mpanda Bw. Philipo Mbogo ambaye ni miongoni mwa walioanzisha shule hiyo baada ya kuona kuwa watoto wanahangaika kwenda kusomea umbali mrefu,ameiambia P5 TANZANIA MEDIA na Mpanda Radio Kuwa suala la shule hii linafahamika na linafanyiwa kazi.
Siku ya jana,kamanda wa Polisi Mkoani Katavi Dhahiri Kidavashari,alitoa wito kwa wakazi Mkoani Katavi kujikinga na mvua sehemu iliyo salama ikiwa ni pamoja na kueupa kwenda chini ya miti ambapokwa kiasi wanafunzi hawa  hawatofauriani na mazingira kama hayo kwa kuwa hakuna madarasa.

 

Thursday, 21 January 2016

Posted By:Issack Gerald | At:Thursday, January 21, 2016

Na.Issack Gerald-Mpanda
Wachimbaji  wadogowadogo wa dhahabu katika mgodi wa Kampuni Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi wamesikitishwa na kitendo cha serikali kuwapiga marufuku uchimbaji wa madini katika mgodi huo kwa madai kuwa eneo hilo ni miliki ya makambi ya jeshi.

Hayo yamebainishwa na wachimbaji hao wakati wakizungumza na P5 TANZANIA MEDIA Sambamba na Mpanda Radio  mgodini hapo kuhusu namna wanavyoathirika kutokana na kufukuzwa katika mgodi huo.
Wamesema kuwa wanategemea mgodi huo kuendesha maisha ya kila siku ikiwemo kusomesha watoto na kulipia kodi ya nyumba.
Mwenyekiti wa mtaa wa Kampuni Bw.Simon James amesema kuwa,kufukuzwa kwa wachimbaji hao wapatao 200 kumepelekea vitendo vya wizi kuibuka ambapo jana mifugo ikiwemo nguruwe na mbuzi kadhaa wameibwa katika makazi ya watu.
Kwa mjibu wa maelezo ya wajimbaji hao walioanza kuchimba eneo hilo miaka ya 1980 wamesema kuwa wanategemea kuendesha maisha kutokana na mgodi huo.
Baadhi ya wachimbaji wadogo ambao wamezungumzia khusu wanavyoathiliwa na kufukuzwa katika mgodi huo ni pamoja na Athman Omary,Lucas Juma,Nuru Hassan na Faustin Method Kamatasimba
Kwa upande wake Mjumbe wa seriklai ya Mtaa wa Kampuni Bi.Flora Simon Mpenda,amesema kuwa kufukuzwa kwa wachimbaji hao kumeathiri mapato ya kuendesha shule ya Msingi Sambwe.
Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Mpanda Bw.Wilium Philipo Mbogo amesema kuwa suala hili lipo katika mamlaka husika kwa mazungumzo  ili lipatiwe ufumbuzi.
Wiki iliyopita,madiwani wa balaza la Manispaa ya Mpanda kupitia kikao chake cha januari 14 mwaka huu waliiomba Manispaa ya Mpanda kuweka mipaka kati ya eneo la  jeshi na makazi ya raia ili kuondoa migogoro ya ardhi.

Thursday, 21 January 2016
Posted By:Issack Gerald | At:Thursday, January 21, 2016

Na.Boniface Mpagape:Mpanda
SERIKALI Mkoani katavi inatarajia kutoa semina kwa viongozi wa serikali kuanzia ngazi za vijiji, kata na tarafa ili watambue vyema majukumu yao.

Mkuu wa mkoa wa katavi Dk. Ibrahim Msengi amesema hayo wakati akizungumza na P5 TANZANIA MEDIA Sambamba na Mpanda radio ofisini kwake. Amesema imebainika kuwa baadhi ya viongozi wa serikali katika ngazi hizo mkoani Katavi wamekuwa hawatambui vizuri majukumu na mipaka ya madaraka waliyonayo.
Amesema semina hiyo inayotarajiwa kufanyika hivi karibuni itawajengea uwezo wa kutambua uwajibikaji wao kwa wananchi na kurahisisha utendaji kazi.
Aidha Mkuu wa mkoa wa Katavi amesema semina hiyo itakuwa ni chachu ya kuleta mabadiliko katika ngazi za uongozi kwani wahusika watapaswa kutoa taarifa kuhusu utendaji wao na itakuwa rahisi kupima uwajibikaji wao katika shughuli za maendeleo.

Thursday, 21 January 2016
Posted By:Issack Gerald | At:Thursday, January 21, 2016

Na.Vumilia Abel-Nsimbo
JAMII wilayani Nsimbo mkoani katavi imeombwa kushiriki katika matengenezo madogo madogo ya miundombinu ya barabara.

Ushauri huo umetolewa na  mkurugenzi wa halmashauri ya Nsimbo Bw Michael Nzyungu wakati akizungumza na  P5 TANZANIA sambamba na mpanda radio Ofisini kwake.
Amesema, hali  ya  miundombinu ya barabara hairidhishi  kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha  na kuwa baadhi hazikusajiliwa wala kutengewa bajeti, na zipo katika mikakati ya kusajiliwa ili zipatiwe bajeti kwa mwaka wa fedha 2016 /2017.
Bw. Nzyungu  amezitaja  baadhi ya barabara zilizotengewa bajeti ni Itenka, Magamba, Kasalala, Sungamila, Katumba complex1 na  Katumba complex B, Urwila na Usense.
Aidha, amewataka madiwani na watendaji  waonapo dalili hatarishi ya kuharibika miundombimu hiyo watoe taarifa mapema ili hatua zichukuliwe.

Thursday, 21 January 2016
Posted By:Issack Gerald | At:Thursday, January 21, 2016

Na.Agness Mnubi-Nsimbo.
MAAFISA elimu sekondari katika halmashauri ya wilaya ya Nsimbo wamepewa siku 6 kuanzia jana, kuhakikisha wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza wanaripoti.

Akizungumza juzi katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Nsimbo, Mkuu wa Wilaya ya Mlele kanali mstaafu Issa Suleiman Njiku, amesema mahudhurio ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza si mazuri na kuwataka maafisa elimu kushirikiana na wenyeviti na watendaji wa vitongoji, vijiji na kata, kuhakikisha wanafunzi hao wanaripoti shuleni.
Aidha Kanali Njiku ameutaka uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Nsimbo kuhakikisha unatekeleza tamko la Waziri wa TAMISEMI juu ya kutatua changamoto ya upungufu wa madawati.
Amesema mkoa wa Katavi umetoa muda  hadi mwisho wa mwezi Machi, kuhakikisha halmashauri zote zinatekeleza agizo hilo, na halmashauri ambayo haitatekeza, Mkurugenzi atachukuliwa hatua za kisheria.

Thursday, 21 January 2016
Posted By:Issack Gerald | At:Thursday, January 21, 2016

Na.Issack Gerald-Katavi
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ndiyo kitovu cha nchi na kwamba kila Mtanzania ameelekeza jicho lake pale kwa sababu anasubiri kupata huduma ya msingi.

Ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na wakurugenzi, wakuu wa taasisi na watumishi wa Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwenye mkutano uliofanyika ofisi ya TAMISEMI mjini Dodoma.
Waziri Mkuu ameitaka ofisi hiyo ihakikishe inaisimamia vizuri mikoa na halmashauri ili Serikali iweze kupata matokeo mazuri na tarajiwa.
Waziri Mkuu alisema jukumu kubwa lililopo hivi sasa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ni kuhakikisha kuwa zinabuni vyanzo vipya vya mapato na kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imekusudia kuwahudumia ipasavyo Watanzania wenye uelewa tofauti na matakwa tofauti na kwa kuanzia Serikali imeanza kuwajenga watumishi wa Serikali kutambua kuwa wao ni wahudumu wa wananchi hivyo inawapasa kuwahudumia vema.
Awali akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na watumishi hao, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Bw. George Simbachawene alisema TAMISEMI wapo tayari kubadilika na kufanya kazi kama kauli ya Rais John Pombe Magufuli inavyotaka, yaani HAPA KAZI TU.
Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Bernard Makali alimpongeza Waziri Mkuu Majaliwa kwa kusimamia vizuri masuala ya elimu nchini wakati akiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya elimu.

Friday, 22 January 2016
Posted By:Issack Gerald | At:Friday, January 22, 2016

Na.Issack Gerald-Nkasi.
WANAFUNZI wapatao 1137 kati ya 2257  hawajaripoti shule kuanza kidato cha kwanza mwaka huu katika Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa licha ya serikali kutoa elimu bure.

Akizungumza na P5 TANZANIA MEDIA sambamba na  Mpanda Radio kwa njia ya mawasiliano ya simu Kaimu Afisa Elimu sekondari  Wilayani Nkasi Bw. Fortunatus Kaguo amesema kuwa,jumla ya wanafunzi 2257 walichaguliwa kuanza  kidato cha kwanza mwaka huu lakini hadi sasa walioripoti shuleni ni wanafunzi 1120 pekee huku wengine1137 wakiwa hawajulikani walipo.
Aidha Afisa elimu huyo amewataka wazazi  kuwapeleka watoto wao shule na atakayekaidi atachukuliwa hatua kali  za sheria.
Amefafanua kuwa wanamikakati ya kuanzisha oparesheni ya nyumba kwa nyumba ili kuwasaka wazazi ambao hawajawapeleka watoto wao shule.
 Hatua ya kukosekana kwa wanafunzi hawa kunafuatia ikiwa ni  muda mfupi baada ya Seriklai kutangaza mpango mkakati wa elimu bure kwa wanafunzi kuanzia Chekechea hadi sekondari kwa wanafunzi wa kidato cha nne.

Friday, 22 January 2016
Posted By:Issack Gerald | At:Friday, January 22, 2016

Na.Boniface Mpagape-Mpanda
TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa mkoani Katavi, imemfikisha katika mahakama ya wilaya ya Mpanda  Afisa mtendaji wa mtaa wa Kawajense akikabiliwa na shtaka la kushawishi na kupokea rushwa ya shilingi elfu thelathini.

Taarifa ya TAKUKURU Mkoa wa Katavi kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo na Kaimu mkuu wa TAKUKURU Mkoani Katavi Bw. Christopher Nakua imesema kuwa afisa mtendaji huyo Bi. Catherine Kipeta, mnamo Jumatatu ya tarehe 18 mwezi huu aliomba rushwa ya shilingi elfu thelathini kutoka kwa mwananchi ili asimpeleke kwenye baraza la kata kwa kosa la kufungua sehemu ya biashara,muda wa kufanya usafi.
Amesema TAKUKURU Mkoa wa Katavi ilifanya uchunguzi wa awali na kuandaa mtego na kumkamata mshtakiwa baada ya kupokea rushwa kutoka kwa mwananchi huyo.
Mshtakiwa amefikishwa katika mahakama ya wilaya tarehe 19 mwezi huu na kusomewa mashtaka mawili yanayomkabili ambayo ni kuomba rushwa ya shilingi elfu thelathini na kosa la pili ni kupokea rushwa, kinyume na matakwa ya mwajiri wake na kifungu cha 15 (1)  (a) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
TAKUKURU mkoa wa Katavi inatoa wito kwa wananchi wote kujiepusha na vitendo vya rushwa ambavyo husababisha kutopatikana kwa haki, kutowajibika kwa watumishi wa umma, kwenda kinyume na maadili, kanuni na viapo vya utumishi, uvunjaji wa haki za binadamu, wananchi kukosa imani na idara, taasisi, mashirika mbalimbali ya serikali.
Aidha,Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa mkoani Katavi imesema kila mwananchi ana wajibu wa kutoa taarifa ya vitendo vya rushwa katika ofisi hiyo iliyopo Mpanda mjini, au kupitia simu ya bure namba 113.
Wananchi wanapaswa kutetea haki, kuzuia rushwa kwani rushwa ni adui wa haki, na penye sheria pana haki, penye haki pana amani, penye amani pana maendeleo.

Friday, 22 January 2016
Posted By:Issack Gerald | At:Friday, January 22, 2016

Na.Mwandishi wetu-Dar es salaam
Watanzania wametakiwa kuacha ushabiki wa vyama vya siasa na badala yake wajikite kutatua matatizo ya kitaifa.
Hayo yamebainishwa leo na Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Josefu Sinde Warioba katika kongamamno la tafakuri ambalo limefanyika Katika ukumbi wa chuo kikuu cha Dar es salaa wakijadili hoja mbalimbali ikiwemo uchaguzi mkuu wa Tanzania  mwaka 2015.
Jaji Warioba amesema kuwa ni lazima kuondoa matatizo ya Rushwa,ukabila,udini huku akiwataka watanzania kuchagua viongozi wanaoona matatizo ya kitaifa kuliko kuchagua viongozi wanaojali masuala ya vyama vyao.
Hata hivyo baadhi ya wajumbe wa kongamano hilo,waligusia mambo mbalimbali yakiwemo yanayohusu siasa kipindi cha uchaguzi mwaka 2015,nafasi ya vyombo vya habari katika uchaguzi wa mawaka 2015 katika kuripoti hali ya uchaguzi,majukumu ya viongozi wa kitaifa kama rais,mawaziri ,tume ya taifa ya Uchaguzi na katiba ya Tanzania.
Kuhusu Katiba baadhi ya wajumbe wametaka katiba ya jaji Joseph Sinde Warioba iwe ndiyo katiba itakayojadiliwa huku wakitaka tume ya taifa ya uchaguzi kuwa huru ili kupata uchaguzi wa huru na haki katika kipindi cha uchaguzi.
Kongamano hilo limeshirikisha wasomi na wahitimu mbalimbali wa chuo kikuu cha Dar es Salaam ambapo mwenyekiti wa kongamano hilo alikuwa ni Jaji Joseph Sinde Warioba.
Asante kwa kunifuatilia kupitia P5TANZANIA.BLOGSPOT.COM,usisahau kumshirikisha mwenzako naye ahabarike,Ni mtangazaji wako Issack Gerald Bathromeo

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA FUPI YA ABDULRAHMAN KINANA ALIYEJUZULU UKATIBU MKUU CCM

FAHAMU HISTORIA YA JOKETI ALIYETUMBULIWA NA UVCCM

HISTORIA FUPI YA LAZARO NYALANDU ALIYEIBWAGA CCM NA KUHAMIA CHADEMA