CWT MKOANI RUKWA:WALIMU TIMIZENI WAJIBU WENU KABLA YA KUDAI HAKI
KIMCHAMA cha walimu CWT wilayani Kalambo
mkoani Rukwa kimewataka walimu kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kabla ya kudai
haki mbalimbali ikiwemo nyongeza ya mshahara.
Ushauri huo umetolewa na katibu wa chama
hicho Peter Simwanza wakati wa sherehe maalumu za kuwapongeza walimu wa shule
za msingi zilizopo katika kata ya Ulumi ambao wanafunzi wao walifaulu vizuri kwa
kupata kiwango cha alama A katika masomo ya kuhitimu darasa la saba pamoja na
shule zilizofanya vizuri.
Alisema baadhi ya walimu wamekuwa mbele
katika kudai haki zao mbalimbali ikiwemo nyongeza ya mshahara lakini hawatimizi
wajibu wao kwamujibu wa sheria.
Simwanza alisema walimu wilayani humo
wanapaswa kutekeleza sheria zote za kazi kwa mujibu wa mkataba wa ajira ndipo
wadai haki zao kwa mwajiri.
Katika hatua nyingine,aliwataka walimu kutokuwa
wanyonge wanapoona haki zao zimekiukwa kwa kuwa maslahi yao yapo mikononi mwao
lakini kwa kufuata sheria,kanuni na taratibu.
Naye Sabina Mwamwezi mwakilishi wa walimu
kitengo cha wanawake katika chama hicho aliwasihi walimu wa kike wilayani humo
kuhakikisha wanajali haiba katika suala la mavazi ili kulinda maadili ya
wanafunzi.
Kwa upande wake mwalimu Zainab Omary wa shule
ya msingi Ulumi ambaye wanafunzi walipata alama A wengi katika somo
analofundisha la kiswahili alisema mafanikio makubwa yalitokana na yeye binafsi
kulipenda somo hilo sambamba na kujituma katika kufundisha pia kuwapenda
wanafunzi wake.
Habari zaidi ni P5TANZANIA
LIMITED
Comments