ASKARI MAGEREZA 11 WASIMAMISHWA KAZI
Jeshi la Magereza Tanzania limewasimamisha kazi askari wake 11 waliofikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji ya Aloyce Makalla (41) mkazi wa Kijiji cha Kerenge wiki iliyopita.
Taarifa
kutoka ndani ya jeshi hilo zinaeleza kuwa askari hao walisimamishwa kazi na
Kamishna Jenerali wa Magereza,Dk Juma Malewa juzi.
Mkuu
wa Magereza Mkoa wa Tanga,John Masunga alithibitisha kusimamishwa kwa askari
hao lakini hakutaka kuzungumzia suala hilo kwa undani zaidi akisisitiza kuwa
msemaji wa jeshi hilo ni Kamishna Jenerali pekee.
Askari
waliosimamishwa ambao walishafikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Korogwe
mwishoni mwa wiki mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Kassim Mkwawa ni Jonas Makere,Shadrack
Lugendo,Lazaro Stephen,Mussa Zuberi,Ramadhan Yusuf,Robert Alfred,Fhidirish
Osmas,Alfonce Revocatus,Mbesha Naftari,Hamis Msola na Michael Elias.
Taarifa
hiyo inaeleza kuwa hatua ya kuwasimamisha kazi askari hao imechukuliwa ikiwa ni
kupisha vyombo vya sheria kufanya kazi yake kwa uhuru zaidi na kwamba hatima
yao itategemea uamuzi wa mahakama hiyo.
Askari
hao wa Wilaya ya Korogwe walifikishwa katika mahakama hiyo wakikabiliwa na
shtaka la kumuua mwanakijiji huyo.
Ilidaiwa
mahakamani hapo na mwanasheria mwandamizi wa Serikali,Saraji Iboru kuwa Januari
22 mwak ahuu saa 9.30 katika kitongoji cha Mapangoni Kijiji cha Kerenge,
washtakiwa hao kwa pamoja walimuua mwanakijiji huyo.
Iboru
ambaye alikuwa akisaidiana na mwendesha mashtaka kiongozi,Shosa Naiman alidai
kwamba siku ya tukio,washtakiwa hao walikwenda nyumbani kwa Makalla wakimtuhumu
kwamba Januari 15 alimjeruhi askari mwenzao aitwaye Sajenti Stephen.
Washtakiwa
hao hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na uwezo
kisheria wa kusikiliza kesi za mauaji ambapo Hakimu Mkwawa aliahirisha kesi
hiyo hadi Februari 15 itakapotajwa tena.
Comments