WIZARA YA AFYA ZANZIBAR KUSHIRIKIANA NA MSD KATIKA UAGIZAJI DAWA NA VIFAA TIBA
WIZARA ya Afya Zanzibar imetiliana saini makubaliano
ya ushirikiano na Bohari ya Dawa Tanzania (msd) katika masuala ya uagiziaji
dawa na vifaa Tiba kutoka viwandani moja kwa moja na hatua hiyo itaiwezesha
Zanzibar kupunguza gharama kubwa ya kuagiza dawa kutoka katika makampuni.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bi. Asha
Abdalla Juma alitia saini kwa upande wa Wizara hiyo na Mkurugenzi Mkuu Laurean Rugambwa Bwanakunu aliiwakilisha
Bohari kuu ya Dawa Tanzania katika sherehe zilizofanyika Wizara ya Afya
Zanzibari Mnazimmoja.
Akizungumza baada ya kutiliana sani
Bi. Asha Abdalla alisema ushirikiano huo utaisaidia Serikali na wananchi kwa
ujumla kuwa na uhakika wa upatikanaji dawa na kupunguza mzigo wa kutumia
gharama kubwa kuagiza dawa.
Alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa
maagizo ya Serikali kuhakikisha dawa
zote zinapatikana bila usumbufu katika
Hospitali na vituo vya afya na kufanikisha
malengo yake ya kuwapatia wananchi
huduma bora za afya.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya ameshauri
mashirikiano yaliyoanzishwa baina ya Bohari
Kuu ya Dawa Zanzibar na Bohari Kuu ya Tanzania yawe endelevu na kuwa
mfano kwa Taasisi nyengine za pande mbili za Muungano na ukanda mzima wa Afrika
Mashariki.
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa
Tanzania Laurean Rugambwa Bwanakunu ameihakikishia Wizara ya Afya kwamba
watatoa huduma bora kwani dawa wanazoagiza ni za uhakika na zenye ubora .
Alisema wamejipanga kikamilifu
kuhakikisha wanatoa dawa na vifaa tiba na hivi sasa wameingia mikataba na
viwanda vikubwa vya kuzalisha dawa
vya ndani na nje ya Tanzania kwa ajili
ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Amewapongeza maafisa wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar waliosimamia na
kufanikisha mpango huo kwa muda mfupi bila ya kuwa na urasimu katika
utekelezaji wake.
Ameishukuru Wizara ya Afya kwa
kuwaamini na kukubali kushirikiana nao katika kazi ya uagizaiaji wa dawa na
vifaa Tiba na amewahakikishia kwamba kazi hiyo wataifanya kwa pamoja katika
viwanda vya kuzalisha dawa.
Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu wa Bohari
ya Dawa Tanzania amewashauri wawekezaji wa Zanzibar kuwekeza viwanda vya dawa
kwa lengo la kupunguza kuagiza bidhaa hiyo kutoka viwanda vya nje.
Alisema kati ya viwanda vitano vya
dawa walivyoingia mkataba wa kununua dawa hakuna hata kiwanda kimoja kutoka
Zanzibar wakati wafanyabiashara wenye
uwezo wa kuwekeza katika sekta
hiyo wapo.
Habari zaidi ni P5TANZANIA LIMITED
Comments