RAIS MAGUFULI ATEMBELEA WAGONJWA HOSPITALI YA TAIOFA MUHIMBILI WAKWEMO KINGUNGE NA MAPACHA WALIOUNGANA
Mapacha walioungana |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli leo amewajulia hali baadhi ya wagonjwa
waliolazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya Moyo ya Jakaya
Kikwete Jijini Dar es Salaam wakiwemo Mzee Kingunge Ngombale Mwiru na Mapacha
walioungana Maria na Consolata Mwakikuti.
Katika wodi ya Mwaisela,Mhe.Rais
Magufuli amemjulia hali Mzee Kingunge Ngombale Mwiru ambaye anatibiwa majeraha
baada ya kushambuliwa na mbwa wake nyumbani kwake Jijini Dar es Salaam.
Kingunge Mwiru |
Dkt.Ibrahim Mkoma wa hospitali hiyo
amemueleza Mhe.Rais Magufuli kuwa hali ya Mzee Kingunge inaendelea vizuri
ambapo Mzee Kingunge amemshukuru Mhe.Rais Magufuli kwa kumwona hospitalini hapo
na amemueleza kuwa sasa anajisikia nafuu baada ya kupata matibabu.
Pamoja na kumpa pole na kumuombea
apone haraka,Mhe.Rais Magufuli amesema anatambua mchango mkubwa wa Mzee
Kingunge katika siasa na maendeleo ya nchi.
Rais pia Katika wodi ya Sewahaji,amemjulia
hali Bw.Richard Kajumulo ambaye ni Kaka wa Mbunge wa Muleba Kusini Prof. Anna
Kajumulo Tibaijuka,Bw.Said Abeid Salim,Bi.Amina Ismail Shirwa,Mzee Hamad Lila
na amempa pole Naibu Katibu Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) Dkt.Zainab Chaula aliyefiwa na Mama yake mzazi wakati Mhe.Rais akiwa
wodini humo.
Wakati huo huo, Mhe.Rais Magufuli
amewajulia hali mapacha walioungana Maria na Consolata Mwakikuti ambao
wamelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa matibabu ya moyo.
Maria na Consolata wamemshukuru Mhe.Rais
Magufuli kwa kuwaona na kuwapa pole huku mapacha hao wakiongoza sala ya
kumuombea Mhe.Rais Magufuli na nchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Moyo ya Jakaya Kikwete Prof.Mohamed Janabi amesema matibabu kwa Maria na
Consolata ambao ni wanafunzi mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Kanisa
Katoliki Ruaha (RUCU) yanakwenda vizuri.
Aidha,Prof.Janabi amesema taasisi
hiyo imefanikiwa kutoa matibabu kwa wagonjwa wa moyo 14,000 katika mwaka
uliopita na kwamba inashika nafasi ya tatu barani Afrika kwa utoaji wa huduma
bora za matibabu ya moyo.
Aidha Mhe.Rais Magufuli amewashukuru
na kuwapongeza madaktari wa hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya Moyo ya
Jakaya Kikwete kwa kazi kubwa wanayofanya kutibu wagonjwa na amesema Serikali
itaendelea kutatua changamoto zinazowakabili ili kuboresha huduma zaidi.
Habari zaidi ni P5TANZANIA LIMITED
Comments