RAIS AWAAPISHA MABALOZI WAWILI AKIWEMO IGP MSTAAFU
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe
Magufuli amewaapisha Meja Jenerali Mstaafu Simon Marco Mumwi kuwa
Balozi wa Tanzania nchini Urusi na IGP Mstaafu Ernest Jumbe Mangu kuwa
Balozi wa Tanzania nchini Rwanda.
Hafla ya kuwaapisha Mabalozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar
es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza baada ya kuapishwa Mhe.Balozi Mumwi amemshukuru
Mhe.Rais Magufuli kwa uteuzi huo na ameahidi kuwa katika kipindi chake
atahakikisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi unaimarishwa na
Tanzania inanufaika na uhusiano huo ikiwemo kuvutia uwekezaji katika viwanda.
Kwa upande wake Mhe.Balozi Mangu pamoja na kumshukuru Mhe.Rais
Magufuli kwa kumuamini ameahidi kuongeza msukumo katika utekelezaji wa ajenda
muhimu za maendeleo kati ya Tanzania na Rwanda hususani ujenzi na manufaa ya
mradi mkubwa wa reli ya kati utakaoiunganisha bandari ya Dar es Salaam na nchi
nne za magharibi mwa Tanzania ikiwemo Rwanda.
Kwa upande Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika ya Mashariki Dkt.Susan Kolimba amewapongeza Mabalozi hao kwa kuteuliwa
kuiwakilisha Tanzania nchini Urusi na Rwanda na ameahidi kuwa wizara hiyo
itakuwa tayari wakati wote kutoa ushirikiano ili kufanikisha utekelezaji wa
majukumu yao ikiwemo diplomasia ya uchumi.
Makamu wa Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan amewataka Mabalozi hao
kufuatilia na kusimamia kwa ukaribu makubaliano mbalimbali ambayo Tanzania na
nchi hizo wameyafikia ikiwemo miradi ya maendeleo.
Habari zaidi ni www.p5tanzania.blogspot.com
Comments