RAIS MAGUFULI AMEPOKEA HATI 3 ZA MABALOZI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli leo amepokea hati za utambulisho za Mabalozi watatu waliopangiwa
kuziwakilisha nchi za Oman,Uholanzi na China hapa nchini.
Rais dkt John Pombe Magufuli |
Waliowasilisha
hati zao kwa Mhe.Rais Magufuli,Ikulu Jijini Dar es Salaam ni Mhe.Ali Abdullah
Al Mahruqi – Balozi wa Oman hapa nchini,Mhe. Jeroen Verheul – Balozi wa
Uholanzi hapa nchini na Mhe.Wang Ke – Balozi wa China hapa nchini.
Mhe.Rais
Magufuli amewapongeza Mabalozi hao kwa kuteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa
nchini na amewahakikishia kuwa Serikali yake itafanya kazi nao kwa ukaribu ili
kuendeleza na kukuza zaidi ushirikiano kati ya nchi hizo na Tanzania hususani
katika uchumi.
Mhe. Rais
Magufuli amemuambia Balozi Jeroen Verheul wa Uholanzi kuwa Tanzania inayo gesi
nyingi na itafurahi kupokea wawekezaji kutoka Uholanzi ikizingatiwa kuwa nchi
hiyo ina uzoefu na teknolojia kubwa katika sekta hiyo.
Kwa upande wa
Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke,Mhe.Rais Magufuli amesema uhusiano wa
Tanzania na China ni wa kihistoria na kidugu, hivyo ametoa wito kwa Balozi
huyo kuuendeleza na kuhakikisha fursa zenye manufaa kwa nchi zote zinatumiwa
ipasavyo ikiwemo kukuza uwekezaji, biashara,utalii na ushirikiano katika
usafiri wa anga.
Comments