GESI YAGUNDULIKA BONDE LA MTO RUVU
TANZANIA imedhihirisha kuwa ni tajiri mkubwa wa rasilimali ya
gesi asilia baada ya kugundulika kwa gesi nyingine katika bonde la mto Ruvu
yenye ukubwa wa ujazo wa futi trilioni 2.17.
Baadhi ya wakazi katika bonde la mto Ruvu |
Ugunduzi huo wa gesi asilia umefanywa na Kampuni ya Dodsal
Hydrocarbons and Power Tanzania Limited ambayo imekuwa inafanya shughuli za
utafutaji wa gesi na mafuta katika Mkoa wa Pwani.
Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Pilavullathil Surendran
alisema jana katika mkutano wa wawekezaji wa gesi na mafuta ulioandaliwa na
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuwa, thamani ya gesi
iliyoko katika eneo hilo inafikia Dola za Marekani bilioni sita sawa na Sh
trilioni 12.
Ugunduzi huo mpya unafanya hadi sasa Tanzania kuwa na amana
ya gesi yenye ukubwa wa futi za ujazo trilioni 57.27.
Kwa upande wake, Profesa Muhongo alithibitisha kugundulika
kwa gesi hiyo tangu Julai mwaka jana, lakini akaeleza kuwa Serikali imechelewa
kutangaza ugunduzi huo kama inavyoagizwa na Sheria ya Mafuta ya Mwaka 2015
kutokana na shughuli za uchaguzi.
“Sheria mpya inatutaka kabla ya waziri mwenye dhamana ya gesi
kutangaza ugunduzi mpya wa gesi na mafuta ni lazima athibitishiwe na mamlaka ya
udhibiti wa bidhaa za Petroli na Gesi (PURA). “Wizara yangu itawasiliana na
mwanasheria mkuu wa serikali ili kupata ushauri wa kisheria kuhusu jambo hilo
na bahati nzuri tayari PURA imeshaanza kushughulikia jambo hilo na naamini kuwa
nitatangaza ugunduzi huo mpya hivi karibuni,” alifafanua Profesa Muhongo.
Licha ya ugunduzi huo mpya tayari gesi imegundulika katika
maeneo ya kisiwa cha Songo Songo mkoani Lindi na eneo la Mnazi Bay huko Mtwara
na katika Wilaya ya Mkuranga, Pwani pia kumegundulika kiasi kikubwa cha gesi.
Comments