BAJETI IJAYO KUTEKELEZWA KWA MAPATO YA NDANI.
SERIKALI imesema bajeti ya mwaka ujao, hususani utekelezaji
wa miradi yote ya maendeleo, itatekelezwa kwa fedha za ndani.
Waziri wa fedha na Mipango Dk.Philip Mpango |
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema miradi
mikubwa kama vile ujenzi wa reli ya kisasa ya kati na miradi mingine mikubwa,
ndiyo itajengwa kwa fedha za msaada kutoka nje kwa kuwa nchi haiwezi kukwepa
kuomba msaada kutoka nje.
Alisema hayo jana katika mji mdogo wa Holili mpakani mwa
Tanzania na Kenya, baada ya kuangalia shughuli za utendaji kazi katika mpaka
huo na baadaye kuzungumza na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) katika mji
huo.
Alisema makusanyo ya sasa ya Sh trilioni 1.7 kwa mwezi
yanayokusanywa kwa sasa nchi nzima, fedha zake zitaelekezwa kwa shughuli za
maendeleo kwa mikoa yote nchini. Waziri huyo alisema si kweli kwa kwamba
serikali ya Rais John Magufuli haitahitaji msaada wa fedha kutoka nje.
Akizungumzia bajeti ijayo, alisema fedha zake nyingi
zitatokana na makusanyo ya fedha za ndani na sio za msaada kutoka nje.
Waziri huyo alisema kwa asilimia kubwa bajeti ya miradi ya
maendeleo katika mikoa yote nchini, fedha zake zitakuwa ni za ndani
zilizokusanywa na kiasi kidogo cha fedha kitatoka nje.
Aliwataka watumishi wote wa umma, wanaokusanya mapato katika
maduhuli ya serikali, kuacha mara moja kushika na kukusanya fedha kizamani kwa
kutumia stakabadhi na kuandika kwa mkono ili kuepuka ushawishi wa kutumia fedha
hizo kwa njia isiyokuwa halali.
Alisema anasikitishwa na utaratibu wa ofisa uhamiaji wa
kitengo viza cha mji wa Holili, kukaa na fedha zaidi ya siku tano na kutoa
stakabadhi kwa mkono.
Waziri alikemea na kumtaka ofisa wa uhamiaji wa mji wa
Holili, kuacha mara moja kukaa na fedha za serikali kwa zaidi ya wiki, tofauti
na mtunza fedha wa TRA anayepeleka fedha benki kila siku.
Alisema utaratibu huo ulishapigwa marufuku miaka mitatu
iliyopita, lakini anasikitika unaendelea katika mji wa Holili. Alimwagiza Mkuu
wa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, kubadilisha hali hiyo kwa maslahi ya serikali.
Akizungumzia uadilifu, Waziri Mpango aliwataka wafanyakazi wa
TRA, kuacha kufanya kazi hiyo kwa kuwanyanyasa wafanyabiashara, kwani kufanya
hivyo ni kosa kisheria. Alisema uadilifu si wa mali tu, bali uko pia katika
kutenda kazi za kila siku.
Alisema pia wananchi wanapaswa kulipa kodi kwa kufurahia na
kuona kodi wanayolipa inawanufaisha, ikiwa ni pamoja na kufanya maendeleo
katika miradi mbalimbali.
Comments