CHUO KIKUU MTAKATIFU JOSEPH TAWI LA ARUSHA WAGOMA,WAKODI MABASI MATAtU KWENDA DAR ES SALAAM KUMWOMA WAZIRI NDALICHAKO.
WANAFUNZI 1,548 wa Chuo Kikuu cha St. Joseph tawi la Arusha, wamegoma kuingia darasani kwa siku tatu na kukodi mabasi matatu kwenda Dar es Salaam kumwona Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.
Katibu mtendaji wa TCU Prof.Yunus Mgaya
Lengo la safari yao hiyo ya Dar ni kujua hatma yao, baada ya
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), kufungia chuo hicho tawi la Songea.
Hata hivyo, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Yunus Mgaya,
alibainisha kuwa hatma ya chuo hicho, itatolewa rasmi kesho baada ya tume hiyo
kupitia mapendekezo ya tume ya wataalamu iliyoundwa mapema kwa ajili ya ukaguzi
wa chuo hicho, tawi la Arusha.
Kulikuwa na vurugu miongoni mwa wanafunzi juzi jioni, hali
iliyofanya uongozi kufikia uamuzi wa kufunga chuo hicho kwa muda usiojulikana.
Wakizungumza jana kabla ya kuanza safari kwenda Dar es Salaam kumwona Waziri
Ndalichako, wanafunzi hao walisema mmiliki wa St. Joseph ni mmoja, hivyo kama
tawi la Songea lina shida ni wazi matawi yote nchini yana shida.
Waliomba serikali kutoa ufafanuzi, kabla ya kuendelea
kupoteza fedha za umma walizopatiwa kama mikopo.
Wanafunzi hao ambao wengi wao hawakutaka majina yao yatajwe
gazetini, walisema wamekuwa wakilalamika mara kwa mara kuwa chuo hicho kina
upungufu mwingi, ikiwemo uhaba wa vifaa vya kufundishia.
Pia wanafunzi hao walihoji sababu za serikali, kutowaleta
wanafunzi wa tawi la Songea iwapo tawi lao la Arusha lipo salama, badala yake
wamepelekwa vyuo vingine, nje ya St Joseph.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Siles Balasingh, aliomba serikali
kutoa majibu haraka kwa wanafunzi hao wanaosomea ualimu wa masomo ya Sayansi,
waendelee na masomo yao, kwani wamepata wasiwasi baada ya kufungwa tawi la
Songea, japo hawana shida na chuo.
Alisema wao kama chuo, wamejitahidi kubandika chuoni hapo
tangazo la TCU kwamba tawi hilo halihusiki na matawi mengine, lakini wanafunzi
hawaelewi, wamegoma kuingia darasani, pia wameharibu mali za chuo.
Alisema walimu wanasikitika kuona vurugu zinatokea kwa sababu
hiyo, hivyo ikiwezekana wanamwomba waziri wa elimu afike chuoni hapo, kutoa
ufafanuzi ili wanafunzi wao hao wapatao 1,518 waendelee na masomo yao.
Hatma ya chuo kujulikana Ijumaa
Akihojiwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dar es
Salaam jana, Profesa Mgaya alisema mgogoro wa chuo hicho, ulianza muda mrefu
tangu mwaka 2014, hali iliyosababisha tume hiyo kufanya ukaguzi chuoni hapo.
Alisema leo tume hiyo inatarajia kukutana na timu hiyo na
Kamati ya Ithibati majira ya saa 3 asubuhi, kuijadili ripoti ya ukaguzi wa chuo
hicho na saa 9 mchana itaitisha mkutano wa dharura kujadili mapendekezo ya
taarifa hiyo na kutoa maamuzi dhidi ya chuo hicho.
Comments