MKURUGENZI WA MIPANGO WA WAKALA WA HUDUMA ZA MISITU TANZANIA (TFS) NA MAOFISA MISITU WA MIKOA YOTE NCHINI WASIMAMISHWA KAZI


Na.Issack Gerald
Waziri wa Maliasili na Utalii Prof.Jumanne Maghembe amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Bw.Mohammed Kilongo na Maofisa wa Misitu wa Mikoa nchi nzima kupisha uchunguzi wa upotevu wa mapato ya Serikali.
                                                                             
Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe (kulia) akizungumza katika kikao na Idara ya Misitu na Nyuki pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika ukumbi wa Ngorongoro Makao Makuu wa Wizara hiyo Mpingo House Jijini Dar es Salaam jana  05 Januari, 2016.

Akizungumza jana na Waandishi wa Habari Makao Makuu ya Wizara hiyo Dar es Salaam, Prof. Maghembe amesema agizo hilo limekuja kutokana na ubadhilifu unaofanywa na Maofisa wa ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali yanayotokana na rasilimali za misitu katika Mikoa na Wilaya kwa kutowasilishwa katika mfuko Mkuu wa Serikali.
Ameagiza pia maofisa hao wote wanaokusanya mapato ya Serikali katika Wilaya watumie muda wa siku kumi kuanzia
jana kuhakikisha mapato yote yaliyokusanywa yanapelekwa benki ikiwa ni pamoja na kukabidhi vitabu vya kukusanyia mapato kinyume cha hapo watachukuliwa hatua
kali za kisheria.
Kwa mujibu wa Waziri Maghembe Bw.Mohammed Kilongo ambaye Idara yake ndiyo inatoa vitabu kwa ajili ya kukusanya
maduhuri ya Serikali katika Mikoa yote na Wilaya zote nchini analazimika kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi ambapo  ukikamilika sheria itachukua mkondo wake bila uonevu wowote.  
Katika hatua nyingine Waziri huyo wa Maliasili na Utalii amewaagiza pia Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS)
kutumia muda wa siku saba kurudi katika jengo la Wizara ya Maliasili na Utalii maarufu kama Mpingo House ambalo walihama mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka
jana na kwenda kupanga katika jengo la NSSF Mafao House lililopo Ilala.
Ameitaka pia Idara ya Misitu na nyuki kupitia Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kuhakikisha kuwa inaongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa kuziba mianya yote ya ubadhilifu pamoja na kuanzisha vyanzo vipya vya mapato na kuboresha vyanzo vilivyopo.
Akizungumzia mchango wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kwenye pato la taifa Mtendaji Mkuu, Bw. Juma Mgoo
amesema katika mwaka huu wa fedha,TFS imeweka makisio ya kukusanya Tsh.Bilioni 88 ambapo mpaka hivi sasa wameshakusanya zaidi ya asilimia 20 na makisio hayo.
Aidha Waziri Maghembe akizungumzia kuhusu uvamizi kwenye hifadhi za taifa na mapori ya akiba,amewataka wananchi
wote waliovamia maeneo ya hifadhi za taifa kwa ajili ya kuchunga mifugo kuondoka ndani ya siku saba zijazo, hku waliovamia mapori ya akiba kwa shughuli za kilimo na ufugaji wakitakiwa ndani ya miezi mitatu ijayo.
Na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Maliasili na Utalii

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA FUPI YA ABDULRAHMAN KINANA ALIYEJUZULU UKATIBU MKUU CCM

FAHAMU HISTORIA YA JOKETI ALIYETUMBULIWA NA UVCCM

HISTORIA FUPI YA LAZARO NYALANDU ALIYEIBWAGA CCM NA KUHAMIA CHADEMA