RAIS AMUAPISHA NAIBU WAZIRI WA MADINI,AMTENGUA KAMISHNA WA MADINI NA KUTEUA MWINGINE
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Dkt. John Pombe
Magufuli leo amemuapisha Mhe.Doto Mashaka Biteko kuwa Naibu Waziri wa Madini na
kuiagiza Wizara hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria kuhakikisha
kanuni za sheria mpya ya madini namba 7 ya mwaka 2017 inasainiwa ifikapo Ijumaa
tarehe 12 Januari 2018.
Mh.Rais Magufuli ametoa agizo hilo muda mfupi baada ya Mhe.Biteko
kuapishwa Ikulu Jijini Dar es Salaam na ameelezea kutoridhishwa kwake na namna
viongozi na watendaji wa Wizara ya Madini wanavyotekeleza majukumu yao polepole
na bila kujali maslahi ya nchi.
Amemuagiza Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi
kushirikiana na Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu na Wakurugenzi wanaohusika katika
Wizara ya Madini kuhakikisha kanuni hizo zinasainiwa.
Pamoja na maagizo hayo Mh.Rais Magufuli ametengua uteuzi wa
Kamishna wa Madini Mhandisi Benjamin Mchwampaka na amemteua Prof. Shukrani
Elisha Manya kuwa Kamishna wa Madini na pia kukaimu nafasi ya Mtendaji Mkuu wa
Kamisheni ya Madini.
Kabla ya uteuzi huu Prof.Shukrani Elisha Manya alikuwa Mhadhiri wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Jiolojia.
Mh.Rais Magufuli amewataka watendaji wote wa Serikali kutekeleza
majukumu yao ipasavyo na ameonya kuwa hatosita kumfukuza kazi mtendaji yeyote
atayeshindwa kutekeleza wajibu wake kwa maslahi ya Watanzania.
Habari zaidi ni P5TANZANIA LIMITED
Comments