TANZANIA NA KAMPUNI YA BARRICK WAFIKIA MWAFAKA SUALA LA MADINI
Majadiliano kati ya Tanzania na timu ya wawakilishi wa kampuni ya
Barrick Gold inayomiliki migodi ya madini hapa nchini,yamekamilika na
makubaliano kati ya pande hizo yametiwa saini leo mbele ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.John Pombe Magufuli Ikulu,Jijini Dar es Salaam.
Timu ya Barrick Gold Corporation ilikuwa imeongozwa na Mwenyekiti
Mtendaji wa kampuni hiyo Prof.John Thornton wakati timu iliyowakilisha Serikali
ya Tanzania imeongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba John
Aidan Mwaluko Kabudi.
Miongoni mwa mambo waliyokubaliana ni kutekeleza mwelekeo mpya wa
biashara ya madini ambapo kutakuwa na mgawanyo sawa wa faida (yaani Tanzania kupata asilimia 50 na Barrick
Gold Corporation kupata asilimia 50 ya faida) na
kuundwa kwa kampuni ya ubia wa usimamizi wa migodi ya madini iliyopo Tanzania
ambayo itakuwa na makao makuu yake Mwanza na ofisi ndogo Dar es Salaam nchini
Tanzania badala ya nchini Uingereza.
Mengine ni kufunga ofisi za uhasibu na fedha zilizopo Johannesburg
Afrika Kusini na kuhamishia Tanzania na kutekeleza masharti yote ya mabadiliko
ya sheria mpya ya madini na rasilimali za nchi ya mwaka 2017.
Aidha, Barrick Gold Corporation imekubali kuwepo kwa wawakilishi
wa Serikali katika bodi za migodi yake yote hapa nchini,kazi mbalimbali za
kwenye migodi kufanywa na kampuni za Kitanzania,Migodi kutoa ajira za kudumu
kwa wachimbaji,wachimbaji hao kuishi majumbani kwao badala ya kuishi kwenye
makambi ya migodi na mashauri yote ya kesi mbalimbali kufanywa hapa nchini.
Kampuni ya Barrick Gold pia imekubali kutoa Dola za Kimarekani
Milioni 300 sawa na takribani Shilingi Bilioni 700 kama malipo ya kuonesha nia
njema ya kufidia fedha zilizotokana na upotevu wa mapato kupitia biashara ya
kampuni hiyo.
Akizungumza baada ya kutia saini makubaliano hayo Prof.Thornton
amempongeza Mhe.Rais Magufuli kwa msimamo wake unaojenga misingi ya biashara ya
kuaminiana na uwazi,ambayo ni muhimu na ya namna yake kwa biashara katika karne
hii ya 21.
Prof.Thornton amesema Barrick Gold Corporation watazingatia
makubaliano haya na wanaamini kuwa yamefungua ukurasa muhimu utakaowezesha
kufanya biashara kisasa.
Kwa upande wake Mhe.Rais Magufuli amezipongeza timu zote mbili
yaani Tanzania na Barrick Gold Corporation kwa kazi kubwa ziliyofanya kufikia
makubaliano hayo na kwa kipekee amempongeza Prof. Thornton kwa nia yake thabiti
ya kukubali kufanyika kwa mazungumzo na kukubali mambo yaliyofikiwa.
Mhe.Rais Magufuli amesema makubaliano hayo yataisaidia nchi
kuzalishaji ajira zaidi kupata manufaa mbalimbali yanayostahili ikiwemo fedha
za kugharamia huduma za kijamii kwa wananchi na yanajenga msingi imara ambao
utaiwezesha Tanzania kunufaika na rasilimali zake za madini.
Mhe. Dkt. Magufuli amemuagiza Waziri wa Katiba na Sheria Prof.Kabudi
kuunda timu zitakazoshughulikia biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi
pamoja na migodi mingine ya dhahabu haraka iwezekanavyo ili nchi iweze
kunufaika ipasavyo.
Pia Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi
hizi badala ya baadhi yao kuzibeza kwa kuwa zina manufaa kwa taifa na wananchi
wake.
Comments