CWT NKASI-TUMECHOKA KUWAKINGIA KIFUA WALIMU WASIOKUWA NA NIDHAMU
CHAMA Cha Walimu Tanzania (CWT) wilayani Nkasi mkoani
Rukwa kimewanusuru walimu 19 kufukuzwa kazi kutokana na utovu wa nidhamu.
Akizungumza jana katika mkutano mkuu wa CWT uliofanyika
katika ukumbi wa Ngunga uliopo mjini Nkasi,mwenyekiti wa chama hicho Selis
Ndasi alisema kuwa walimu wanakabiliwa na changamoto kubwa ya utovu wa nidhamu
na kuwa inabidi wabadilike na kuwa kutokana na hilo ilikuwa walimu 19 wafukuzwe
kazi lakini walikingiwa kifua na chama hicho.
Alisema chama hicho kimechoka kuwalinda walimu wahalifu na kuwa
sasa wanatakiwa wabadilike wawe na nidhamu kazini na kutomkorofisha mwajiri na
watambue kuwa hivi sasa serikali ni chungu na ukifanya kosa moja unafukuzwa
kazi na kuwa kama wakiendelea kuzembea wengi watafukuzwa kazi.
Alisema miongoni mwa matatizo yanayo wakabili walimu ni utoro
kazini,uzembe,ulevi na kutowaheshimu waajiri wao na kuwa sheria inaeleza kuwa
mwalimu asikuwepo kazini siku tano mfululizo bila taarifa adhabu yake ni
kufukuzwa kazi.
Mkuu wa idara ya utumishi wa Walimu TSC Richard Kityega
alisema kuwa idara ya ualimu imekua ikikabiliwa na changamoto ya utovu wa
nidhamu na kuwa hadi sasa walimu 24 wameshafukuzwa kazi kwa makosa hayo na kuwa
wataendelea kuwawajibisha walimu kama hao kwa kuwafukuza kazi.
Hivyo aliwaomba wawakilishi wa chama hicho mahali pa kazi
kuwasaidia wanachama wenzao ambao ni Waalimu kuwaelekeza namna
wanavyostahili kuishi kwa kufuata kanuni za utumishi wa umma na
kuachana na mazoea na kuwa idara yao haimuonei mtu na hadi kufikia hatua ya
kumfukuza kazi Mwalimu kuna vitu vingi wanakuwa wamejiridhisha.
Naye Afisa elimu wa shule za msingi wilayani humo Misana
Kwangullah kwa upande wake alidai kuwa walimu kama watumishi wa umma wajitahidi
kufuata tu kanuni za utumishi na kuwa wale
watakaoendelea kuenenda kinyume na maadili sheria zipo na sasa zinafanya
kazi.
Mjumbe wa kamati tendaji ya (CWT) ngazi ya taifa Juma Saidia
aliwataka wawakilishi wa CWT mahala pa kazi kuwasimamia wenzao na kuwaonya
juu ya kufuata misingi ya ajira yao vinginevyo watakwisha.
Alisema lengo la kuwapo kwa Chama Cha Walimu si kutetea maovu
bali ni kuwalinda dhidi ya uonevu na kusimamia uwajibikaji na kuwa sasa chama
hicho hakitakuwa tayari kumtetea Mwalimu ambaye ataonyesha utovu wa nidhamu na
kushindwa kuwajibika vyema mahala pake pa kazi.
Habari
zaidi ni www.p5tanzania.blogspot.com au
ukurasa P5Tanzania Limited
Comments