RAIS MAGUFULI KUZINDUA MIRADI 9 YA MAENDELEO MIKOA YA KAGERA,KIGOMA,TABORA NA SINGIDA-Julai 18,2017

Rais wa Tanzania DK.John Pombe Magufuli

RAIS John Magufuli anatarajiwa kuzindua miradi tisa ya barabara na uwanja wa ndege ambayo itaunganisha mikoa ya Ukanda wa Kati na Magharibi nchini na nchi jirani kwa barabara za lami katika kuchochea harakati za maendeleo ya uchumi wa viwanda.

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Ujenzi, Joseph Nyamhanga alisema jana kwa simu kwamba uzinduzi wa miradi hiyo utafanyika katika mikoa ya Kagera, Kigoma, Tabora na Singida kuanzia kesho hadi 25, mwaka huu.

Nyamhanga alisema ufunguzi wa barabara ya Kigoma – Biharamulo – Lusahunga yenye urefu wa kilometa 154 utafanyika Biharamulo Mjini mkoani Kagera kesho huku uzinduzi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Nyakanazi – Kibondo yenye urefu wa kilometa 50 utafanyikia Kakonko mkoani Kigoma, Julai 21.

Alieleza kuwa uzinduzi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kidahwe –Kasulu yenye urefu wa kilometa 63 utafanyika Kasulu Mjini mkoani Kigoma, Julai 21 ambako pia ufunguzi wa barabara ya Kaliua – Kazilambwa yenye urefu wa kilometa 56 utafanyika Julai 23 Kaliua Mjini mkoani Tabora. Alisema ufunguzi wa barabara ya Urambo –Ndono – Tabora yenye urefu wa kilometa 91 utafanyika Julai 24, Tabora Mjini na ufunguzi wa barabara ya Tabora – Nyahua yenye kilometa 85 utafanyika siku hiyo hiyo.

Aidha, Katibu Mkuu alieleza kuwa ufunguzi wa Uwanja wa Ndege wa Tabora utafanyika Julai 24 na ufunguzi wa mradi wa Manyoni – Itigi – Chanya wenye urefu wa kilometa 89.3 utafanyika Itigi mkoani Singida Julai 25, mwaka huu.

Aidha, alisema ufunguzi wa Uwanja wa Ndege wa Tabora ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha miundombinu ya viwanja vya ndege na usafiri wa anga nchini.Alifafanua kuwa miradi yote ya barabara imejengwa kwa fedha za ndani isipokuwa mradi wa Uwanja wa Ndege wa Tabora.


Aliongeza kuwa kuzinduliwa kwa miradi hiyo kutafungua fursa za kiuchumi ndani na nje ya nchi na kuwataka wananchi kuilinda ili waone matunda yake katika kuelekea uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA FUPI YA ABDULRAHMAN KINANA ALIYEJUZULU UKATIBU MKUU CCM

FAHAMU HISTORIA YA JOKETI ALIYETUMBULIWA NA UVCCM

HISTORIA FUPI YA LAZARO NYALANDU ALIYEIBWAGA CCM NA KUHAMIA CHADEMA