RAIS MAGUFULI AHITIMISHA ZIARA YA SIKU 7 MIKOA YA KIGOMA,TABORA,KAGERA NA SINGIDA,YAFAHAMU YALIYOJILI KATIKA ZIARA HIYO-Julai 25,2017
Rais wa Tanzania John Magufuli akizungmza na wananchi wa Singida |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli leo tarehe 25 Julai, 2017 amekamilisha ziara yake ya kikazi ya siku 7
katika Mikoa ya Kagera, Kigoma, Tabora na Singida kwa kufungua barabara ya
Itigi – Manyoni Mkoani Singida.
Wakazi Mkoani Singida wakimsikiliza Rais wa TANZANI John Mafuguli alipofanya ziada katika mkoa huo Julai 25,2017 picha na Issack Gerald |
Barabara hiyo inayounganisha Mikoa ya Singida, Tabora na Kigoma
ina urefu wa kilometa 89.3 na imejengwa gharama ya Shilingi Bilioni 114.692,
fedha ambazo zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Akizungumza na wananchi wa Itigi katika sherehe za ufunguzi wa
barabara hiyo Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth
Magufuli, amesema Watanzania wana kila sababu ya kutembea kifua mbele kwa kuwa
barabara hiyo pamoja na nyingine saba alizozifungua katika ziara hii zenye
urefu wa jumla ya kilometa 707 zimejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 806,
fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa miradi mikubwa ya ujenzi wa
barabara imetekelezwa na inaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini
na kwamba Serikali imeamua kuanzisha Wakala wa Barabara Vijijini kwa lengo la
kuhakikisha barabara za vijijini zinajengwa kwa kiwango cha lami.
Kwa barabara ya Mkiwa – Itigi yenye urefu wa kilometa 57 na ambayo
tayari zabuni ya ujenzi ilishatolewa kwa mkandarasi ili aijenge kwa kiwango cha
lami kwa gharama ya Shilingi Bilioni 104, Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuupitia upya mkataba wa ujenzi wa barabara
hiyo kwa kuwa kiwango cha fedha kilichopangwa ni kikubwa ikilinganishwa na
gharama halisi.
Pia amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof.
Makame Mbarawa Mnyaa kujadiliana na Mkandarasi anayejenga barabara hiyo ili
aweze kuendelea kujenga barabara kutoka Itigi kuelekea Chunya hadi Makongorosi
Mkoani Mbeya.
Pamoja na wananchi wa Itigi Mkoani Singida, Mhe. Dkt. Magufuli
aliyetokea Tabora amezungumza na wananchi waliosimamisha msafara wake katika
vijiji vya Kigwa, Kizengi na Tura Wilayani Uyui na amewataka kuendelea kuchapa
kazi kwa juhudi na maarifa pamoja na kuzingatia uzalishaji mazao
yanayostahimili ukame kama vile uwele, mtama, viazi na muhogo ili kuepuka
tatizo la upungufu wa chakula.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi wote nchini
kuhamasisha wananchi kufanya kazi hususani shughuli za kilimo ambacho ni uti wa
mgongo wa Taifa, na ameonya kuwa kiongozi ambaye hatatekelezi agizo hilo
atakuwa hafai na ataondolewa.
“Nawaagiza Wakuu wa Mikoa na
Wakuu wa Wilaya hamasisheni watu kufanya kazi na kama kuna viongozi na
watendaji wasiotekeleza wajibu huo katika maeneo yenu waondoeni mara
moja” ameagiza Mhe. Rais Magufuli.
Viongozi wengine waliongozana na Mhe. Rais Magufuli katika ziara
ya leo ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Dkt. Hamis Kigwangalla, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu
Prof. Norman Sigalla King na Wabunge wa Mkoa wa Singida.
Mhe. Rais Magufuli amewasili katika Ikulu ndogo ya Chamwino Mkoani
Dodoma.
Comments