BARAZA LA MADIWANI MKOANI MARA LAWAADHIBU WATUMISHI WANNE KWA MATUMIZI MABAYA YA MADARAKA-Agosti 17,2017
Baadhi ya madiwani Mkoani Mara |
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya
mji wa Tarime mkoani Mara leo Alhamisi, Agosti 17 limewakuta na hatia na
kuwachukulia hatua za kisheria watumishi wanne kwa kutumia vibaya madaraka yao
na kuisababishia halmashauri hiyo hasara ya mamilioni ya fedha.
Akitoa taarifa ya hatua
iliyochukuliwa na kamati ya maadili ya utumishi, mwenyekiti wa halmashauri
hiyo, Hamis Nyanswi amewataja waliochukuliwa hatua hizo kuwa ni Simion Nyadwera
aliyekuwa katibu wa idara ya afya ambaye alihamishiwa katika Halmashauri ya
Maswa anadaiwa kuchota Sh24 milioni na ametakiwa kurejesha kiasi hicho cha
fedha huku Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ikitakiwa
kumchunguza utumishi wake.
Nyanswi amemtaja mtuhumiwa mwingine
kuwa ni Laurenti Marwa aliyekuwa afisa utumishi Mwandamizi wa Halmashauri ya
Mji wa Tarime aliyedaiwa kushirikiana na watumishi 60 kuzisababishia hasara
taasisi za fedha na kuiingiza halmashauri hiyo kwenye mgogoro mkubwa.
Amesema kuwa Marwa atapunguziwa
mshahara wake kutoka ngazi ya mshahara ya TGTS F yenye kiwango cha mshahara wa
Sh1.3 milioni kwenda TGTS E, yenye kiwango cha mshahara wa Sh950,000.
Watumishi wengine ni Sabure Masanja
na Quinter Wayoga waliopewa onyo kutokana na makosa yao.
Watumishi hawa hawakuwa tayari
kuzungumzia uamuzi uliochukuliwa na baraza la madiwani licha ya kupigiwa simu
na kuita bila kupokelewa.
Mbunge wa Tarime Mjini, Esther
Matiko amewataka watumishi wa umma kuzingatia maadili ya kazi zao ili kuwafanya
wananchi kupata huduma wanayostahiki badala ya kukutwa na usumbufu usio kuwa wa
lazima.
Comments