WATATU WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA TUHUMA ZA MAKOSA MBALIMBALI LIKIWEMO SHAMBULIO LA MWILI.
Na.Issack
Gerald-MPANDA
VIJANA
watatu wakazi wa Mpanda mjini jana wamefikishwa katika mahakama ya Mwanzo mjini
Mpanda, wakikabiliwa na shtaka la shambulio la kudhuru mwili.
Akisoma
shtaka hilo Mbele ya hakimu David Mbembela, koplo Mtei kutoka jeshi la polisi
Mpanda amewataja waliotenda kosa hilo kuwa ni Ramadhan Hamis mkazi wa Nsemulwa,
Maneno Shaban mkazi wa Mikocheni na Mohamed Mussa ambapo wote kwa pamoja mnamo
tarehe 14 Mwezi huu katika maeneo ya majengo mjini Mpanda, walimshambulia
Abdallah Salum mkazi wa Misunkumilo na kumsababishia maumivu makali.
Koplo
Mtei ameiambia mahakama kuwa mlalamikaji hakufika mahakamani kutokana na
kulazwa katika hospitali ya wilaya ya Mpanda anakoendelea na matibabu kutokana
na kipigo alichopigwa na washtakiwa hao.
Aidha,
ameiomba mahakama hiyo isiruhusu dhamana kwa washtakiwa hadi pale taarifa
kuhusu hali ya muhanga zitakapotolewa.
Washtakiwa
wote wamekana shtaka na hakimu Mbembela amesema kutokana na ombi kutoka kwa
askari ambaye ni afisa wa serikali na amekula kiapo cha kusema ukweli, hivyo
mahakama imeridhia hoja iliyotolewa.
Kesi
hiyo itatajwa tena tarehe 22 mwezi huu na washtakiwa wamerudishwa rumande.
Comments