WAZIRI MKUU ASEMA HANA KINYONGO NA MTU YEYOTE,ASEMA ITIKADI ZA SIASA ZILIISHIA OKTOBA 25
Na.OFISI YA WAZIRI MKUU.
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema hana kinyongo na mtu yeyote kwa sababu alitangaza
msamaha siku aliyokabidhiwa cheti kuwa mbunge wa jimbo la Ruangwa na kusisitiza
kuwa siasa ziliisha tangu Oktoba 25, mwaka huu.
Waziri Mkuu Kasim Majaliwa akizungumza na Wakazi Mkoani Lindi |
Ametoa
kauli hiyo jana jioni wakati akizungumza na mamia ya wananchi waliofika
kumsikiliza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa mikutano wa
Likangala wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
“Sina
kinyongo na mtu yeyote na roho yangu iko huru, hivi ndiyo nilivyo.
Nilikwishatangaza msamaha kwa hiyo ninawaomba wale niliowakwaza nao pia
wanisamehe… lakini ninawasihi kuwa milango iko wazi, wawe huru kurudi wakati
wowote,” alisema huku akishangiliwa na wananchi hao.
“Ninawataka
twende pamoja ili tulete maendeleo ya Ruangwa, huku nikisisitiza kaulimbinu
yangu ya kampeni kwamba Ruangwa kwa Maendeleo Inawezekana. Wao warudi
tu, nitawahudumia wote bila kujali itikadi zao.”
Aliwaeleza
wakazi hao wa Ruangwa na vitongoji vyake kwamba amekuja kuwashukuru kwa
kumchagua na kumpa kura nyingi la sivyo asingefanikiwa kuwa mbunge wao.
“Kikubwa ninamshukuru Mungu aliyemuongoza Mheshimiwa Rais pamoja na Makamu wake
hadi wakanipa jukumu hili,” alisema.
“Kipekee
ninamshukuru Mungu aliyemuongoza Mheshimiwa Rais na kutupa sisi wana Ruangwa
tusaidiane kulibeba jukumu hili. Ninawahakikishia kuwa pamoja na jukumu hili la
kitaifa, sitawaacha wala sitawaangusha. Nitakwenda mikoa mingine hapa nchini
ili kuwasikiliza na kuwahudumia Watanzania huku nikijua kwamba mpo salama,”
alisema.
Aliwaeleza
wananchi hao kwamba bila kujali itikadi za vyama, ameunda timu ya madiwani 22
kutoka kata zote za jimbo hilo ambayo atafanya nayo kazi kwa karibu ili
kuhakikisha matarajio ya wana-Ruangwa yanatimia. Madiwani wanane kati hao 22
wanatoka UKAWA na 14 wanatoka Chama cha Mapinduzi (CCM).
Akigusia
mipango ya maendeleo kwa jimbo hilo, Waziri Mkuu alisema ameamua kuweka umeme
wa nishati ya jua kwenye shule zote na zahanati zote ambazo hazitafikiwa na
umeme wa gridi ya Taifa kwa sababu ziko pembezoni mwa jimbo hilo.
“Nafanya
hivi kwa sababu sipendi watoto wetu wakose masomo ya jioni kwa sababu ya kukosa
umeme au washindwe kufanya mafunzo kwa vitendo (practicals) kwa vile wamekosa
umeme,” alisema.
Mapema,
akiwa njiani kuelekea Ruangwa, Waziri Mkuu alisimama kwa muda kijijini kwao
Nandagala katika kata ya Mnacho, na kuwasalimia wananchi waliojitokeza kumpokea
kwa nderemo na hoihoi kibao.
Katika
mkutano wa hadhara ulioandaliwa kijijini hapo, Waziri Mkuu alikabidhiwa zawadi
mbalimbali yakiwemo mavazi ya kimila pamoja na silaha za jadi.
Aliwataka
wakazi hao wamvumilie kwa sababu ratiba sasa itabadilika na hawatamuona mara
kwa mara kama ilivyokuwa awali kwa vile anapaswa awahudumie Watanzania wote.
“Zile safari za jimboni zitapungua sana lakini mjue ni kwa sababu niko kwa
ajili ya Watanzania wote wa nchi hii,” alisema.
“Ninaomba
dua zenu ili niendelee kuwa mwadilifu na muwajibikaji,” aliwaomba na kususutiza
kwamba waendelee kumuombea yeye pamoja na viongozi wengine wa kitaifa ili
waweze kutimiza yale ambayo Watanzania wanatamani yatokee.
Comments