WAUAWA KWA KUKATWA MAPANGA KWA MADAI YA USHIRIKINA
Watu watatu wameuawa katika matukio tofauti likiwamo la wanawake wawili kuuawa kwa kukatwa mapanga kutokana na imani za kishirikina katika kitongoji cha Kilombero Wilayani Nkasi mkoani Rukwa. Kamanda wa polisi Mkoani Rukwa George Kyando aliwataja waliouawa kuwa ni Salome Kisinza(50) na Rahel Pawa(22) walikatwa mapanga sehemu mbalimbali za miili yao na watu wasiojulikana. Kyando alisema waliofanya mauaji hayo waliwavizia wakiwa wamelala ndani ya nyumba yao ambapo walivunja mlango na kuingia ndani na kuanza kuwakata mapanga. Alisema walimuua Salome na kumjeruhi Rahel baadaye walitoweka huku wakimwacha katika hali mbaya na alifariki dunia akiwa njiani akipelekwa hospitali. Kamanda Kyando alisema chanzo cha mauaji hayo inasadikiwa ni tuhuma za imani za ushirikina kwa kuwa Salome alikuwa akituhumiwa kumroga mume wake Jilala Mponeja ambaye amekuwa akiumwa kwa muda mrefu na anatibiwa kwa mganga wa jadi wilayani Kalambo mkoani humo. Katika tukio jingine lililotokea s...