RAIS MAGUFULI ATUMA SALAAMU ZA RAMBIRAMBI KWA MKUU WA MKOA WA KAGERA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe
Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali
Mstaafu Salum Kijuu kufuatia watu 11 kupoteza maisha katika ajali ya gari
iliyotokea katika Kijiji cha Nyangozi, Wilaya ya Biharamulo Mkoani Kagera.
Ajali hii imetokea jana baada ya basi dogo la abiria aina ya
Nissan Caravan lililokuwa likitoka Kakonko Mkoani Kigoma kuelekea Kahama Mkoani
Shinyanga kuligonga ubavuni lori la mizigo kisha kugongana uso kwa uso na lori
jingine na kusababisha vifo vya watu 11 na wengine 6 kujeruhiwa.
Mhe.Rais Magufuli amepokea kwa huzuni na masikitiko makubwa
taarifa za vifo vya Watanzania hao na amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja
Jenerali Mstaafu Salum Kijuu kumfikishia pole kwa familia za Marehemu wote,
ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo hivyo.
Aidha,Mhe.Rais Magufuli amewakumbusha watumiaji wa barabara hasa
madereva kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani na ameviagiza
vyombo vinavyohusika kuongeza jitihada za kukabiliana na ajali za barabarani
ili kuokoa maisha ya watu na mali zinazopotea kutokana na ajali.
Habari zaidi ni P5TANZANIA LIMITED
Comments