TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU KUZIMWA KWA 'CHANELI' ZA BURE KWENYE VING'AMUZI
Msemaji
Mkuu wa Serikali Dkt.Hassan Abbas amesema, kwa mujibu wa sheria iliyopo sasa vituo
vyote vya runinga ambavyo vimepewa leseni ya FTA (Free to Air) vinapaswa
kuonekana hata baada ya kifurushi kwenye kisimbusi kwisha.
Dkt.Hassan Abbas |
Ufafanuzi
huu unatolewa kufuatia uwepo wa malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wananchi
kuhusu kukosa huduma ya runinga za bure pindi vifurushi katika visimbusi (ving’amuzi)
vyao vinapomalizika
Dkt.Abbas
amesema hadi sasa kuna vituo 16 vya runinga vya ndani ya nchi vilivyopewa
leseni hizo vikiwemo vituo vya ITV,Clouds TV na Channel 10.
Amesema
ili mtumiaji atazame Runinga hata baada ya kufurushi chake cha malipo kwisha,kituo
cha runinga (mfano ITV) kinapaswa kuwalipa warushaji wa masafa (mfano Azam) ili
ITV iweze kuonekana kwa wananchi hata ambao hawajalipia visimbusi vyao.
Wakati
huo huo Dkt.Abbas ametahadharisha kuwa, endapo kituo cha runinga hakitawalipa
wasafirishaji wa masafa watakatiwa huduma na hivyo kuwafanya wananchi washindwe
kutazama runinga bure.
Kuhusu
TBC kuonekana katika visimbusi vyote hata bila malipo,msemaji amesema kila
kisimbusi kinatakiwa kuweka TBC kupitia sera ya ‘must carry’ ambayo inaiwezesha
kuonekana kwa wananchi bila malipo yoyote.
Kwa
sasa serikali haina mfumo wa kuwaadhibu wamiliki wa vituo vya runinga wenye
leseni za FTA lakini hawawalipi warusha masafa ili wananchi watazame runinga
hizo bure badala yake warusha matangazo hayo wanawakatia huduma kama
hawajalipwa.
Kuhusu
Dstv na Azam kukata matangazo ya runinga za ndani baada ya kifurushi kwisha Dkt
Abbas amesema suala hilo lipo Baraza la Ushindani hivyo wananchi wasubirie
majibu na kwamba asingependa kulizungumzia kwa sasa.
Habari zaidi ni P5TANZANIA LIMITED
Comments