VITUO VYA AFYA MKOANI RUKWA VIMELAUMIWA KUTOKOPA FEDHA KUTOKA MFUKO WA BIMA YA TAIFA YA AFYA
VITUO vya afya vya serikali mkoani Rukwa
vimelaumiwa kwa kushindwa kutumia fursa ya kuomba mikopo katika mfuko wa
bima ya afya ya Taifa kwa ajili ya kununua madawa,vitendanishi pamoja na
ukarabati wa majengo badala yake vituo vya watu binafsi na madhehebu ya dini ndio
wamekuwa wa kinufaika na fursa hiyo.
Meneja wa mfuko wa bima ya afya mkoani humo Saimon Mbaga alisema
hayo wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya mfuko wa bima ya Afya mkoani humo
katika kikao cha kamati ya ushauri ya maendeleo ya mkoa wa Rukwa RCC.
Alisema kuwa vituo vinavyo milikiwa na serikali mkoani humo
vimekuwa havitumii fursa hiyo tofauti na vituo vinavyomilikiwa na tasisi za
dini na watu binafsi kana kwamba wao hawana shida ya kuboresha huduma.
Mbaga alisema kuwa vituo vingi vinavyo milikiwa na serikali vina
hali mbaya katika suala la vifaa tiba pamoja na majengo lakini kitu cha
kushangaza havichangamkii fursa hiyo na kubaki havina vitendanishi na
miundombinu chakavu.
Alisema ili waweze kuboresha huduma zao wanapaswa kubadilika na
kuomba mikopo inayotolewa na NHIF ili waweze kuboresha huduma ili wagonjwa
waweze kupata matibabu ya kisasa.
Kwaupande wake mkuu wa mkoa huo Zelote Steven aliwaasa watendaji
wa mfuko huo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wajiunge na mfuko wa huduma ya
afya kwa jamii CFH, pamoja na mfuko wa afya ya Taifa NHIF ili waweze kupata
huduma.
Alisema kuwa kwa kuchangia kiasi cha shilingi 76,500 kwa watu
wazima na shilingi 70,400 kwa watoto wadogo wakazi wa mkoa wa Rukwa
wanaweza kujiunga na mfuko wa bima ya afya yaTaifa, Kinachotakiwa wapewa elimu
na kuona umuhimu wa kujiunga na huduma hizo.
Aidha alisema kuwa kwa wananchi watakaoshindwa kulipa kiasi
hicho hapo juu ,pia upo mfuko wa afya ya jamii CHF ambao unahitaji kiasi cha
shilingi 10,000 ni vizuri wananchi wakapewa elimu ili wajiunge na mfuko huo ili
wajihakikishie matibabu.
Comments