MWANAMKE MKOANI RUKWA AMJERUHI MMEWE KWA KISU AKIDAI ANAKATIZWA STAREHE YA KUNYWA POMBE-Septemba 23,2017
Na.Issack
Gerald-Naksi
Mwanamke aliyefahamika kwa jina la Maria Mwanahiya mkazi wa kijiji cha
Ntatumbila wilaya Nkasi mkoani Rukwa amemjeruhi vibaya mume wake
kwa kumchoma kisu ubavuni kwa madai kuwa alipata hasira baada ya kukerwa na
kitendo cha mume wake kumlazimisha kuacha starehe zake ikiwemo kunywa pombe.
Tukio hilo limetokea jana
majira ya saa 10:30 usiku katika kijiji cha Ntatumbila wilaya
Nkasi mkoani Rukwa muda mfupi baada ya mwanamke huyo kurejea nyumbani kutoka
kilabuni alipokuwa anakunywa pombe.
Inaelezwa kuwa mwanaume huyo aliporudi nyumbani kwake kutoka
katika shughuli zake hakumkuta mke wake na wala mke hakuweka chakula kwa ajili
ya mmewe hali iliyomlazimu kumfuata mkewe kwenye kilabu ya pombe.
Alipofika kilabuni, alimlazimsha mkewe kurudi nyumbani lakini
mwanamke huyo aligoma,hata hivyo baadhi ya watu waliokuwa wanakunywa naye pombe
walimsihi arudi nyumbani, ndipo alipokubali kwa shingo upande akarudi na mmewe.
Baada ya kufika nyumbani ulizuka ugomvi mkubwa wa kurushiana
maneno kati ya wanandoa hao ambapo mwanamke huyo alikuwa akimwambia mumewe
aache kumfuata fuata anapokuwa kwenye starehe zake kwani yeye siyo
mtumishi wa nyumbani.
Wakati wakiendelea kufokezana kwa muda mrefu, ndipo mwanamke huyo
alipoamua kwenda jikoni kuchukua kisu na kumchoma mumewe ubavuni na
kumsababishia jeraha kubwa ambalo lilivuja damu nyingi.
Tukio hilo lilisababisha watu kujazana katika nyumba yao na kuamua
kumkamata mwanamke huyo na kumpeleka kituo cha polisi na mume wake
kumkimbiza hospitalini ili akapatiwe matibabu ili kuokoa maisha yake.
Afisa mtendaji wa kijiji cha Ntatumbila Daniel Kalumbilo ameiambia
amesema hilo ni tukio la pili kwa mwanamke huyo kumshambulia mumewe
kwa silaha za jadi ambapo aliwahi kumpiga mpini na kumuumiza kichwa mpaka
akafanyiwa upasuaji.
Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa George Kyando amethibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kuwasihi wanandoa kujitahidi kutatua migogoro yao kwa
njia ya amani na wanaposhindwa wawashirikishe ndugu wengine kuliko kupigana na
kuumizana.
Tukio hili limetokea siku mbili tu baada ya Mwanamke kumuua kwa
kumchinja mme wake huko katika kata ya Tinde wilayani Shinyanga,kutokana na
ugomvi wa simu ya mkononi,mke akimtuhumu mme kupigiwa na mchepuko wake.
Habari nyingine zaidi ni www.p5tanzania.blogspot.com au
kupitia P5Tanzania Limited
Comments