WATOTO 62 WENYE MAHITAJI MAALUMU WAIBULIWA MPANDA,WAMO ALBINO WAWILI WALIOPELEKWA SUMBAWANGA KUSOMA
Na.Issack
Gerald-MPANDA
Jumla ya watoto 62 wenye mahitaji
maalumu wakiwemo wawili wenye ulemavu wa ngozi albino wamefichuliwa Wilayani
Mpanda wakiwa katika mazingira yanayowanyima haki zao za msingi ikiwemo
kupatiwa elimu kwa kipindi cha mwezi
Juni hadi Desemba mwaka huu.
Baadhi ya watoto wenye mahitaji maalumu Wilayani Mpanda.PICHA Na.Issacka Gerald |
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa
elimu Jumuishi Mkoani Katavi Bw.Raphael Fortunatus wakati akiwasilisha taarifa
ya kamati ya elimu Jumuishi Wilayani Mpanda mbele ya mratibu wa Elimu Jumuishi
katika Mikoa ya Rukwa na Katavi kupitia kikao cha kamati hiyuo ambacho
kimefanyika leo katika Ofisi za kamati hiyo zilizopo Wilayani Mpanda.
Bw.Fortunatus amesema,idadi hiyo
imepatikana katika kipindi cha Mwezi Juni hadi Desemba mwaka huu katika kata za
Kakese mkwajuni na mbugani ambapo wamepatikana watoto19,Kawanzige watoto 28 na
Mwamkuru watoto 15.
Aidha amesema kuwa walemavu wawili wa
ngozi albino walioibuliwa kijiji cha kakese ni Catherine Chemuka(11) na Peter
Chemuka (9) ambao wote wanaendelea na masomo katika shule ya Msingi Malangari
iliyopo Wilayani Sumbawanga huku wakiishi katika bweni kujikinga na wimbi la
mauji ya kikatiri dhidi yao.
Mbali na kuendelea na mikakati ya
kuwaibua zaidi watoto wenye mahitaji maalumu,kamati imetoa mafunzo kwa walimu
26 Wilayani Mpanda kuwajengea uwezo wa kuwasaidia watoto wanaoibuliwa.
Katika hatua nyingine Jumatatu ijayo
ya Desemba 21 mwaka huu,kamati hiyo inatarajia kumwandikia barua Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda ili kumwomba
afungue madarasa ya wanafunzi wenye ulemavu wa kusika viziwi katika shule ya
msingi Azimio waliozuiwa na
mkandarasi aliyefunga madarasa hayo akishinikiza kulipwa pesa zake ambapo hadi
sasa ni mwaka mmoja madarasa hayo hayatumiki huku kuanzia darasa la kwanza hadi
la saba wakisomea katika chumba kimoja kibovu ambapo walimu watatu huingia
kufundoisha kwa wakatik mmoja katika ubao mmoja.
Kwa upande wake mratibu wa elimu
jumuishi katika mikoa ya Rukwa na Katavi Bw.Joseph Ndomba,ameitaka kamati hiyo
kushirikiana kwa ukaribu na idara za serikali kutatua changamoto mbalimbali
zinazowakabili watoto wenye mahitaji maalumu.
Kamati hiyo yenye wajumbe wapatao
12,inajumuisha idara mbalimbali zikiwemo wakuu wa idara za maendeleo ya jamii katika
Manispaa ya Mpanda,viongozi wa dini,wazazi na walezi wenye watoto walemavu na
wasio na walemavu na Chombo cha habari cha Mpanda Radio Fm ambapo mwakilishi ni
Issack Gerald mwandishi wa habari wa kituo hicho.
Wakati huo huo kupitia kikao hicho
kamati imependekeza kukutana mara kwa mara kupanga mikakati ya kuibua watoto
waliofichwa wenye mahitaji maalumu ili wapatiwe elimu huku wazazi wakiaswa
kutoa ushirikiano na kuachana na tabia ya kuwaficha.
Kamati ya elimu jumuishi Wilayani
Mpanda inafanya kazi chini ya ufadhili wa mashirika matatu yaliyoungana na
kuunda umoja wao unaojulikana kama IFI.
Mashirika haya ni International Aids Services(IAS),Free
Pentekoste Church Of Tanzania(FPCT) na International Center Of Disabilities
Comments