KATIBU TAWALA KIGOMA APEWA SIKU MBILI KUKABIDHI TAARIFA YA MAANDI YA UBADHIRIFU KWA WAZIRI MKUU MAJALIWA
Na.Ofisi ya mawasiliano ya Waziri Mkuu
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku mbili kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma,
Eng. John Ndunguru kukamilisha uchunguzi wake na kumpatia taarifa ya maandishi
juu ya tuhuma ubadhirifu wa fedha za umma unaohusisha uuzwaji wa jengo la
KIGODECO na viwanja 12 vya Manispaa ya Kigoma/Ujiji ambao unadaiwa kukiuka
taratibu.
Ametoa
agizo hilo leo mchana (Jumatano, Desemba 30, 2015) kwenye ukumbi wa NSSF, mjini
Kigoma wakati akizungumza na viongozi na watendaji mbalimbali wa mkoa huo
alipokuwa akifanya majumuisho ya ziara yake ya siku mbili mkonai humo.
Waziri
Mkuu Majaliwa amesema anazo taarifa kuwa jengo hilo liliuzwa kwa sh. milioni
370/- pamoja na jengo jingine la MIBOS kwa sh. milioni 50/- licha ya kupewa
barua na Mkuu wa Mkoa huo kusitisha uuzwaji wa jengo pamoja viwanja hivyo, bado
liliuzwa.
“Katibu
Tawala wa Mkoa kaa na Mkurugenzi wa Manispaa, Mhandisi wa Manispaa na Mhasibu
na unipatie taarifa kwa maandishi ifikapo Jumamosi hii,” alisema Waziri Mkuu
huku akishangiliwa.
“Nataka
kujua nani alifanya tathmini ya jengo, ni kwa nini jengo liliuzwa kwa thamani
hiyo, je ndiyo thamani halisi ya jengo? Ni kwa nini RC alipozuia, utaratibu
uliendelea? Je, utaratibu wa uuzaji ulifuatwa? Ni kwa nini viwanja viliuzwa
chini ya thamani,? Katibu Tawala kaa na watu wako na uniletee hiyo taarifa kwa
maandishi. Tukigundua kuna mianyamianya tutachukua hatua za kinidhamu,”
alisema.
Viongozi
walioagizwa kukutana na Katibu Tawala wa Mkoa ni Mkurugenzi wa Manispaa, Eng.
Boniface Nyambele; Mhandisi wa Manispaa, Eng. Boniface William na Mhasibu wa
Mapato wa Manispaa, Ndg. Bawili Mkoko.
Kuhusu
uuzwaji wa jengo na viwanja, imebainika kuwa Mkuu wa Mkoa huo, Luteni Kanali
(Mst), Issa Machibya alizuia uuzaji huo kwa barua ya tarehe 16 Juni 2015
akitaka viwanja hivyo vitumike kwa matumizi ya manispaa na mchakato huo
usitishwe hadi mwakani lakini agizo lake lilipuuzwa na jengo likauzwa kwa sh.
milioni 370 ambayo ni bei ya kiwanja pekee.
Tuhuma
nyingine zinazopaswa kuchunguzwa ni pamoja na matumizi ya sh. milioni 809 kwa ajili
ya ujenzi wa maabara. Kiasi hicho kilitolewa kutoka kwenye fedha za miradi ya
maendeleo (Capital Development Grants-CDG), Mradi wa Programu ya Kuendeleza
Sekta ya Kilimo na Mifugo (ASDP), Mradi wa Uendelezaji Miji (Tanzania Strategic
Cities Programme –TSCP) na Miradi ya Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (SEDP).
Inadaiwa
kwamba Mkurugenzi huyo kwa kushirikiana na baadhi ya watumishi wa idara ya
mipango na fedha walitumia ujenzi wa maabara kama kigezo cha kuchota fedha hizo
bila kutoa taarifa kwa wakuu wa idara husika ambao walikasimiwa fedha hizo.
Tuhuma
nyingine ni manunuzi hewa ya vipuri (spare parts) vyenye thamani ya sh. milioni
8 na manunuzi hewa ya stationeries yenye thamani ya sh. milioni 4.6/-. Haya
yanadaiwa kufanywa Julai 25, mwaka huu na Mkurugenzi huyo akishirikiana na
Mhasibu Mkoko.
Waziri
Mkuu amerejea jijini Dar es Salaam mchana wa leo huu.
Comments