RAIS MAGUFULI AZINDUA UKUTA KUZUNGUKA MADINI YA TANZANIATE
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli amezindua ukuta unaozunguka migodi ya
madini ya Tanzanite wilayani Simanjiro mkoani Manyara uliojengwa na Jeshi la
Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa lengo la kudhibiti utoroshaji wa
madini na ukwepaji wa kodi.
Ukuta huo wenye urefu wa kilometa
24.5 umejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 5 na Milioni 646 ikiwa ni
utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa tarehe 20 Septemba,2017 na Mhe.Rais
Magufuli alipokuwa akizindua barabara ya KIA – Mirerani.
Mhe.Rais Magufuli ameipongeza JWTZ
kwa kukamilisha kazi hiyo kwa haraka na kwa gharama nafuu na amewapongeza
maafisa,askari na vijana 2,356 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) walioshiriki katika
ujenzi kwa uzalendo wao na kujituma ili kulinda rasilimali hiyo muhimu kwa
Taifa.
Mhe.Rais Magufuli amelikubali ombi la
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Venance Salvatory Mabeyo na
ameagiza vijana wa JKT walioshiriki katika ujenzi wa ukuta huo waajiriwe katika
vyombo vya ulinzi na usalama vikiwemo Polisi na JWTZ ilimradi wawe na sifa
zinazostahili.
Aidha,Mhe.Rais Magufuli
amewahakikishia wananchi wa Mirerani kuwa watanufaika zaidi na hatua ambazo
zinachukuliwa kudhibiti utoroshaji na ukwepaji wa kodi za madini ya Tanzanite
na amekabidhi gari jipya la wagonjwa aina ya Toyota Land Cruiser “Hard Top”
alilowaahidi wakati akiagiza kujengwa kwa ukuta huo.
Wakati huo huo Mhe.Rais Magufuli
amemshukuru Mzee Jumanne Ngoma aliyevumbua madini ya Tanzanite mwaka 1967 na
kutambuliwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl.Julius Kambarage Nyerere mwaka 1980, na
amempa Shilingi Milioni 100 kwa kutambua mchango mkubwa alioutoa kwa Taifa
kuvumbua madini hayo,yanayopatikana Tanzania pekee kote duniani.
Amesema utafiti uliofanywa katika
kitalu C umebaini kuwa kuna mashapo ya Tanzanite yatakayochimbwa hadi mwaka
2042 na kwamba lipo eneo jingine lenye Tanzanite nyingi zaidi na ambalo
Serikali italizungushia ukuta ili kulinda na kudhibiti utoroshaji madini na
ukwepaji wa kodi.
Mhe.Rais Magufuli amewataka
Watanzania kuunga mkono juhudi za Serikali kuinua uchumi,kutekeleza miradi ya
maendeleo na kudhibiti rasilimali za nchi na amewasihi kujiepusha na watu
wanaoshabikia mabaya kwa nchi wakiwemo wanaowaunga mkono wanyonyaji na uvunjifu
wa amani.
Kwa upande wake Mzee Jumanne Ngoma
amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutambua mchango wake wa kuvumbua madini ya
Tanzanite na amesema anaamini sasa madini hayo yatapata thamani inayostahili.
Nae Waziri wa Madini Mhe.Angellah
Kairuki amemshukuru Mhe.Rais Magufuli kwa maelekezo yake ya kujengwa kwa ukuta
na kulisimamia vizuri soko la Tanzanite ambapo malipo ya mrabaha kutoka kwa
wachimbaji ukiondoa Tanzanite One na STAMICO kwa miezi mitatu tu ya kuanzia
Januari hadi Machi mwaka huu yamefikia Shilingi Milioni 714 na hivyo kuzidi
malipo ya mwaka mzima wa 2015 (Shilingi Milioni 166.8),2016 (Shilingi Milioni
71.8) na 2017 (Shilingi Milioni 147.1).
Katika sherehe hizo Mhe.Rais Magufuli
amekabidhi tuzo na vyeti kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen.Mabeyo,maafisa na
askari wa JWTZ na vijana wa JKT walioshiriki ujenzi huo.
Habari zaidio ni www.p5tanzania.blogspot.com
Habari zaidio ni www.p5tanzania.blogspot.com
Comments