WAVUVI RUKWA WAIPONGEZA ZAMBIA KUONDOA ZUIO BIASHARA YA SAMAKI
WAVUVI
wa samaki katika ziwa Tanganyika wilayani Kalambo mkoani Rukwa wameishukuru
serikali ya Zambia kwa kuondoa marufuku ya biashara ya samaki katika nchi hiyo.
Marufuku
hiyo ilikuwa imewekwa kwa takribani wiki mbili zilizopita kutokana na kuwepo
kwa mlipuko wa ugonjwa wa kipindu pindu nchini humo.
Shukrani
hizo wamezitoa jana na kusema marufuku hiyo ilikuwa imewaathiri kiuchumi
kutokana na kuwa soko kubwa la samaki wanaovuliwa katika ziwa Tanganyika
wilayani Kalambo mkoani Rukwa nchini Tanzania ilikuwa ikitegemea soko katika
nchi hiyo jirani.
Mmoja
wa wavuvi aliyejitambulisha kwa jina la Richard Sichone alisema serikali ya
nchi hiyo imeondoa marufuku hiyo baada ya jitihada za kukabiliana na ugonjwa
huo kuonesha mafanikio ambapo hivi sasa wavuvi hao wameanza kuuza samaki wao
nchini Zambia.
Alisema katika kipindi ambacho
serikali ya nchi hiyo ilikuwa imezuia uvuvi katika nchi hiyo pamoja na biashara
ya samaki kutoka nchi za Tanzania na Congo DRC kutokana na kipindu pindu
walikabiliwa na ugumu wa maisha kwa kuwa walikuwa wakiuza samaki kwa bei ya
hasara tofauti na walipokuwa wakiuza nchini Zambia.
Sichone
alisema katika nchi hiyo kuna makampuni 12 ambayo yamekuwa yakinunua samaki
tani 1,200 kila siku ambapo kilo moja wavuvi wamekuwa wakiuza kwa shilingi
5,000 za kitanzania lakini katika kipindi ambacho nchi hiyo ilipiga marufuki ya
biashara ya samaki soko lilishuka ambapo walikuwa wakiuza kilo moja kwa
shilingi 1,500 na kulikuwa kuna kampuni moja tu ya Premji iliyopo Kasanga
ambayo ilikuwa ina uwezo wa kununua tani nane za samaki.
Naye
Michael Sichilima mvuvi wa kijiji cha Kapele katika mwambao wa ziwa Tanganyika
wilayani kalambo alisema kitendo ilichokifanya serikali ya Zambia ni cha kupongezwa
kwani kimetoa fursa ya biashara si tu kwa wavuvi wa nchini humo lakini pia
wavuvi kutoka nchi jirani watanufaika.
Hata
hivyo wavuvi hao wanasema wanaheshimu sheria za nchi hiyo ili wasigeuke kuwa
kero nchini humo
Habari zaidi ni www.p5tanzania.blogspot.com
Comments