WANAFUNZI WAKUMBWA UGONJWA WA AJABU


WANAFUNZI wa kike katika Shule ya Msingi Kabwe  mwambao mwa Ziwa Tanganyika  wilayani Nkasi mkoani Rukwa,wanaugua ugonjwa wa ajabu unaosababisha wapige kelele hovyo,kutetemeka na kisha kuanguka.
Mkuu wa Shule hiyo,Amon Kawana alisema ugonjwa huo ulianza kutokea shuleni hapo tangu mwishoni mwa mwaka jana ambapo mpaka sasa ni wanafunzi wapatao 20 wa kike wameshakumbwa na ugonjwa huo na kusababisha taharuki  shuleni hapo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kabwe,Richard Madeni alisema  wachungaji  na waganga wa jadi wamekuwa wakiwashughulikia  tatizo hilo  bila mafanikio yoyote.
Diwani wa Viti Maalumu,Christina Simbakavu alisema tatizo hilo  limedumu kwa  muda mrefu na sasa limekuwa kero kwa  wazazi,walimu pia wakazi  wa kijiji hicho .
Kaimu afisa elimu msingi wilayani Nkasi Mnyuke Msumeno amekiri kuwapo kwa tatizo hilo na wamemuagiza mwalimu mkuu wa shule hiyo atoe taarifa ya maandishi itakayomfikia mkurugenzi mtendaji ili waone uwezekano wa kupeleka wataalamu wa afya katika eneo hilo.
Aidha alisema tatizo hilo ni kubwa hasa kwa kuwa hutokea mara kwa mara hivyo na wanaisubiri taarifa hiyo ili wataalamu wa afya wafike eneo la tukio ili waweze kuja na majibu ya tatizo lenyewe ikiwa ni pamoja na namna ya kulitatua.
Kwa upande wake,Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Rukwa,Dkt Emanuel Mtika alisema kwa kuwa shule hiyo ni ya kutwa  na wasichana wanasumbuliwa  ni wenye umri chini ya miaka 16 na tayari  jitihada  kadhaa  ikiwemo wachungaji  kufanya maombezi  bila mafanikio  kuna uwezekano mkubwa  kuna mlipuko  wa ugonjwa wa malaria.

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA FUPI YA ABDULRAHMAN KINANA ALIYEJUZULU UKATIBU MKUU CCM

FAHAMU HISTORIA YA JOKETI ALIYETUMBULIWA NA UVCCM

HISTORIA FUPI YA LAZARO NYALANDU ALIYEIBWAGA CCM NA KUHAMIA CHADEMA