AUAWA KWA KUKANYAGWA NA TEMBO
MWANAMKE aliyefahamika
kwa jina la Maria Sekaye(60) mkazi wa kijijii cha Ilambila wilayani
Kalambo Mkoani Rukwa ameuawa baada ya
kukanyagwa na tembo.
Tembo hao wanaelezwa kuwa walikuwa njiani wakitokea katika
pori la akiba la Lwafu mkoani Rukwa kuelekea katika nchi jirani ya Zambia.
Akizungumzia tukio hilo diwani wa kata ya Mkowe Alfred
Mpandasharo alisema tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 4 za asubuhi wakati
mwanamke huyo akiwa ametoka kutembelea shamba lake lililokuwa limevamiwa na
mazao kuliwa na tembo hao.
Alisema Maria akiwa njiani kurejea kijijini ghafla alikutana
na kundi kubwa la tembo waliokuwa na hasira wakiwa wamechokozwa na vijana wa
kijiji hicho kutokana na kuwafukuza kwa makelele ili waondoke kijijini hapo
waache kula mazao katika mashamba yao na ndipo kundi la tembo lilimvamia na
kuanguka chini ambapo alikanyagwa na kufa papo hapo.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kalambo Julieth Binyura
aliwaonya wananchi wanaowafukuza hovyo tembo hao waache tabia hiyo kwani ni
hatari kwa usalama wao wasubiri watendaji wa maliasili ambao watafika kwa ajili
ya kuwafukuza kijijini hapo.
Bi.Binyura alisema kwa
kawaida katika vijiji vya Sundu,Mkowe
Ilambila na Katete huwa ni mapito ya tembo ambapo mara kwa mara wamekuwa
wakipita kuelekea nchini Zambia na baadaye kurejea tena nchini katika pori la
akiba la Lwafu.
Alisema ni vizuri wananchi wakaacha kufanya kilimo na kujenga
makazi katika mapito ya tembo hao kwa kuwa kawaida huwa hawaachi kupita hata
kama itachukua miaka mingi lakini kunasiku watarejea na kupita tena hivyo ni
hatari kwao.
Habari zaidi ni P5TANZANIA LIMITED
Comments