RAIS WA RWANDA PAUL KAGAME AFANYA ZIARA HAPOA NCHINI,APANGA MIKAKATI YA MAENDELEO NA RAIS MAGUFULI
Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mhe.Paul
Kagame leo tarehe 14 Januari, 2018 amefanya ziara ya kikazi ya siku moja hapa
nchini kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.John
Pombe Magufuli.
Katika Picha Rais Magufuli Kushoto na Kulia ni Rais Kagame |
Mhe. Rais Kagame amewasili katika
uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kupokelewa
na mwenyeji wake Mhe.Rais Magufuli na kisha kulakiwa na viongozi mbalimbali
wakiongozwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, na baadaye akaelekea
Ikulu ambako pamoja na kufanya mazungumzo ya faragha, viongozi hao wamezungumza
na wananchi kupitia vyombo vya habari.
Mhe.Rais Magufuli amesema katika
mazungumzo yao wamekubaliana ujenzi wa reli kwa kiwango cha kisasa (Standard
Gauge) kati ya Isaka nchini Tanzania na Kigali nchini Rwanda yenye urefu wa
takribani kilometa 400 uanze mwaka huu (2018), na wamewaagiza Mawaziri
wanaohusika na miundombinu kukutana ndani ya kipindi cha wiki mbili kuanza sasa
ili kuweka mipango ya utekelezaji ikiwemo upatikanaji wa fedha.
Mhe. Rais Magufuli ameongeza kuwa
wakati uamuzi huo ukifikiwa, Tanzania ambayo tayari imeanza ujenzi wa reli ya
kati (Standard Gauge) kuanzia Dar es Salaam – Morogoro hadi Dodoma yenye urefu
wa kilometa 726 na itakayogharimu Shilingi Trilioni 7.6, itaanza mchakato wa
kuunganisha sehemu iliyobaki ya kutoka Dodoma – Isaka yenye urefu wa takribani
kilometa 400 ili mizigo iweze kusafirishwa moja kwa moja kutoka bandari ya Dar
es Salaam hadi Kigali nchini Rwanda.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amebainisha
kuwa japo kuwa kumekuwa na ongezeko la mizigo ya Rwanda inayosafirishwa kupitia
Tanzania iliyofikia tani 950,000 kwa mwaka, biashara kati ya nchi hizi mbili
sio ya kuridhisha na hivyo amesema wamekubaliana kuboresha zaidi mazingira ya
biashara ikiwemo kuimarisha miundombinu ya reli na barabara na kuwahamasisha
wafanyabiashara wa Tanzania na Rwanda kufanya biashara zaidi.
Mhe. Rais Magufuli amemhakikishia
Mhe. Rais Kagame kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na
ushirikiano wake na Rwanda kwa manufaa ya wananchi, na kwamba ipo tayari
kumuunga mkono atakapochaguliwa kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) katika
kikao cha wakuu wa nchi na Serikali kinachotarajiwa kufanyika mwishoni mwa
mwezi huu wa Januari, 2018 Mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.
Kwa upande wake Mhe. Rais Kagame
amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa mwaliko wake na amempongeza kwa kazi nzuri
inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya
nchi yake na Tanzania.
Mhe. Rais Kagame amesema yeye na Mhe.
Rais Magufuli wameamua kufanya kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo na ameahidi
kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na Mhe. Rais Magufuli ili mipango yote
waliyojiwekea itekelezwe ikiwemo kuinua biashara na kuongeza ajira, na pia
ameshukuru kwa Tanzania kuwa tayari kumuunga mkono atakapochaguliwa kuwa
Mwenyekiti wa AU.
Mhe. Rais Kagame amemaliza ziara yake
ya kikazi ya siku moja hapa nchini na amerejea nchini kwake Rwanda.
Habari zaidi ni P5TANZANIA LIMITED
Comments